Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, January 7, 2015

WADAU WAOMBWA KUJITOKEZA UBORESHAJI HOSPITALI YA MKOA WA MBEYA.

Mganga mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Glori Mbwile, akimkaribisha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya pamoja na wageni waliowatembelea. 
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya pamoja na wageni wao kutoka Benki ya NMB Mbeya.

Afisa Uhusiano wa Serikali wa Benki ya NMB Kanda ya Mbeya, Focus Lubende, akifafanua baadhi ya mambo kwa watumishi wa hospitali ya mkoa wa Mbeya.
Meneja wa NMB Kanda ya Mbeya, Lecresia Makiriye, akizungumza na Watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kuhusu lengo lao la kutembelea Hospitali hiyo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina akipokea msaada wa magodoro kutoka kwa meneja wa NMB Kanda ya Mbeya.
 Mganga mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Mbwile akipokea msaada wa magodoro kutoka kwa Meneja wa NMB kanda ya Mbeya.
Baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya wakisaidiana na uongozi wa hospitali kupokea msaada wa magodoro kutoka kwa wafanyakazi wa NMB.
Baadhi ya Wauguzi wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya wakifuatilia kwa makini zoezi la makabidhiano wa magodoro.


WADAU wa Maendeleo mkoani Mbeya wametakiwa kujitokeza katika kuchangia uboreshaji wa Hospitali ya Mkoa ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa na vitanda katika Wodi mpya ya watoto.

Aidha imeelezwa kuwa wadau wa sekta binafsi kushiriki katika shughuli za maendeleo ni utekelezaji wa adhma ya Serikali ya uanzishwaji wa mfumo shirikishi baina ya serikali na sekta binafsi(PPP).

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Seif Mhina, alipokuwa akipokea msaada wa magodoro kwa ajili ya kulalia wagonjwa kutoka Benki ya NMB Kanda ya Mbeya.

Dk. Mhina alisema wadau zaidi wanatakiwa kujitokeza kuchangia ukarabati na maboresho ya Hospitali ya Mkoa wa Mbeya ili iweze kutoa huduma kwa wananchi kwa kiwango sahihi na kwa wakati muafaka baada ya miundombinu muhimu kukamilika.

Alisema kutokana na msaada wa magodoro 17 uliotolewa na wafanyakazi wa Benki ya Nmb, hivyo uongozi wa Hospitali unapaswa kutoa kipaumbele cha matibabu  kwa watumishi wa benki hiyo kwa kuwekewa mfumo maalumu utakaowawezesha kutopanga foleni kusubiri matibabu.

“Labda ni waagize watumishi wenzagu kuanzia leo watumishi wa Nmb wakifika Hospitalini hapa kwa lengo la kutibiwa wapewe kipaumbele ikiwezekana wakaingizwa kwenye mfumo wanaotibiwa wagonjwa wa bima ya afya” alisema Dk. Mhina.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Glori Mbwile, akitoa shukrani kwa msaada wa magodoro alisema bado kunachangamoto ya ujenzi wa njia za kupitishia wagonjwa pamoja na kununulia vifaa katika Wodi ya watoto.

Alisema wodi mpya ya watoto inahitajika kuwa na vitanda 80,magodoro na vifaa vingine vinavyopaswa kuwemo wodini vyenye thamani ya shilingi Milioni 160 hivyo msaada zaidi wa wadau unahitajika ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Awali akizungumza kabla ya kukabidhi msaada wa magodoro, Meneja wa Kanda wa Benki ya NMB, Lecrisia Makiriye, alisema mara nyingi benki huangalia maeneo ambayo wateja wake wanapatikana kama katika sekta za elimu na afya ili kusaidia kupunguza changamoto zinazokuwepo.

Alisema Wafanyakazi wa Benki waliamua kuchangishana na kununua magodoro 17 pamoja na fedha taslimu shilingi Milioni 2 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa njia za kupitishia wagonjwa.

“Tunawiwa kuona taasisi zinazohudumia umma tunazichangia ili kupunguza changamoto kwa kuisadia Serikali ndiyo maana tukanunua magodoro haya machache ingawa tunaona bado hayajamaliza tatizo pamoja na fedha za kujengea njia za kupitishia wagonjwa” alisema Meneja huyo.

Mwisho.
Na Mbeya yetu

No comments: