WAFANYABIASHARA wa Jiji la Mbeya
walifunga maduka yao wakipinga kulipa mabadiliko ya sheria ya kodi ya
2014, ambayo walidai kuwa imeongeza ututiri wa kodi na kuendelea kuwakamua.
Wakizungumza baada ya kukutana katika mkutano
wao uliofanyika ndani ya ukumbi wa Mkapa, Jijini hapa, ulioshirikisha watendaji
wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Mbeya na jeshi la polisi,
wafanyabiashara hao walisema kodi hiyo hailipiki na hawako tayari kulipa.
Awali baadhi ya wafanyabiashara walitoa
malalamiko yao mbalimbali kuhusu suaala la sheria mpya ya kodi ya mwaka 2014
kuwa inaongeza kero kubwa kwa wafanyabiashara na itasababisha kukwamisha ustawi
wao.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Masaga Salum,
alisema mabadiliko hayo ya sheria ya kodi hayawatendei haki wafanyabiashara kwa
kuwa hawakushirikishwa katika mchakato wa kuandaliwa kwa sheria hiyo.
“Haiwezekani serikali ikawa inatoa misamaha ya
kodi kwa wawekezaji wakubwa toka nje ya nchi , huku ikitumia nguvu kubwa
ya ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo wa hapa nchini ambao ndio
wapiga kura wanaowaweka madarakani ”
Mfanyabiashara mwingine, Tekla Mushi, alisema
mbali na sheria mpya kuongeza viwango vya kodi mara mbili, lakini pia bado
kumekuwa na mlundikano wa kodi kwa wafanyabiashara .
Alitaja baadhi ya kodi hizo ambazo alidai kuwa
zinakwamisha ustawi wa wafanyabiashara kuwa ni kodi ya zimamoto, taka, Kosota,
Leseni, pamoja na ushuru wa Halmashauri na Mabango ya biashara.
“Mwenyekiti tulitaka pia ufafanuzi juu ya
TRA kutulazimisha wafanyabiasha kuonesha mikataba ya kodi za nyumba na mara
baada ya kuonyesha hutukadilia kodi badala ya kumbana mwenye nyumba”
alisisitiza Mushi.
Mchungaji Enock Mwandandila, alisema ongezeko la
kodi halikuakisi hali halisi ya biashara na vipato vya wafanyabiashara na
kutaka watunga sera kuangalia upya suala hilo kwani linaweza kuleta vurugu na
kusababisha machafuko nchini.
“Serikali inapaswa kutambua kuwa wafanyabiashara
hawana kinua mgongo pindi umri wa kufanyakazi unapofikia ukomo, hivyo ongezeko
la kodi hiliwezi kutekelezeka na tunaomba iundwe tume ya maridhiano ili kufikia
muafaka”.
Hata hivyo, akijibu hoja za wafanyabiashara hao,
Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya, Anniny Lema, alisema suala la ulipaji kodi
ni la kisheria na kwamba lawama kwa Mamlaka hiyo ni sehemu ya changamoto.
“Sisi ni daraja tu kati yenu na serikali,
kikubwa mmetoa maoni yenu, kikubwa tutayafikisha sehemu husika na kama
kutahitajika marekebisho wao ndio wenye uwezo wa kufanya hivyo” alisema Lema.
Kaimu Meneja huyo, alidai kuwa kwa mujibu wa
sheria ya fedha ya mwaka 2014 viwango vya ulipaji kodi kwa wafanyabiadhara
wadogo vimeongezeka zaidi ya viwango vilivyokuwepo mwaka 2013/14.
Alisema kuwa kwa wafanyabiashara wanaofikia
makisio yanayozidi sh. Mil 4 hadi Mil 7.5 zamani walikuwa wakilipa shilingi
laki moja kwa mwaka na sasa watalazimika kulipa shilingi laki mbili.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment