.
Matunda ya nyanya yakionekana shambani
WAKULIMA
mbali mbali wa Mazao ya mbogamboga, maua na matunda wa Mikoa ya Nyanda za juu
kusini wametakiwa kuunganisha nguvu ili waweze kukidhi viwango vya uzalishaji
wa mazao ya mboga mboga, matunda na maua kwa ajili ya kusafirisha nje ya Nchi.
Wito
huo ulitolewa na Mkulima wa Nyanya wa Skimu ya Umwagiliaji ya Ilaji iliyopo
Wilaya ya Mbarali mkoani hapa, Daniel Wabare, alipokuwa akizungumzia Changamoto
zinazowakabili wakulima wa mazao hayo katika Sherehe za wakulima zilizoandaliwa
na Taasisi ya TAHA zilizofanyika katika kijiji cha Ilaji.
Wabare
alisema ili wakulima waweze kutumia fursa ya Uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Songwe kwa ajili ya kusafirisha mazao ya Mboga mboga, matunda na maua ni lazima
wakulima wanaounda Mikoa ya Nyanda za juu kusini yenye fursa hiyo wakaungana.
Alisema
ili usafirishe mzigo mkubwa kwa ndege ni lazima bidhaa ziwe za kutosha jambo
ambalo mtu mmoja hataweza kulimudu isipokuwa kwa kuunganisha nguvu, hivyo
akatoa wito kwa Wakulima wenzie kuunda umoja utakaowawezesha upatikanaji wa
masoko na uzalishaji wenye tija.
Wabare
alisema chini ya uangalizi wa Shirika la TAHA aliweza kujifunza teknolojia ya
kilimo cha nyanya cha umwagiliaji kwa njia ya matone wakati wa maonesho ya
Wakulima nanenane mwaka huu baada ya kutembelea banda lao na hatimaye kujaribu
kilimo hicho kilichomletea mafanikio makubwa.
Alisema
katika Shamba la Hekta moja ameweza kupanda Nyanya tangu mwezi wa nane ambazo
ameanza kuvuna mwezi huu huku matarajio yake ikiwa ni kupata matenga 560 yenye
thamani ya shilingi Milioni 8.4 ili hali alitumia mtaji wa shilingi Milioni 2.6
kwa msaada wa TAHA.
Kwa
upande wake Bwana shamba wa TAHA kutoka Makao makuu, Isaac Ndamanhyilu, alisema
shirika lake limekuwa likiwafundisha Wakulima teknolojia mbali mbali
zinazowasaidia kulima chenye tija kwa kulinga kuinua uchumi na kuinua vipato
vyao pamoja na upatikanaji wa masoko.
Alisema
baada ya kuwafundisha wakulima hao hutenga siku moja ambayo huwakusanya
wakulima kutoka skimu mbali mbali ili waweze kubadilishana uzoefu changamoto
wanazokutana nazo katika shughuli za kilimo cha mazao ya Horticulture ili
ziweze kutatuliwa na wataalamu wa Kilimo.
Katika
Sherehe za Jana zilizofanyika katika Skimu ya umwagiliajo ya Ilaji iliyopo
wilayani Mbarali iliwakutanisha wakulima zaidi ya 300 kutoka Skimu za
umwagiliaji za Wilaya za Mbarali na Mbeya ambazo ni Moto mbaya,
Ihahi,Ipatagwa,Chimala, Igomelo, Uturo na Simambwe.
Naye
Mgeni rasmi katika Sherehe hizo, Afisa Tawala wa Wilaya ya Mbarali, Alfred
Mzurikwao, ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulam Hussein Kiff,
alisema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za TAHA katika kuwaendeleza
wakulima kilimo chenye tija.
Alisema
TAHA inafanya kile kinachopaswa kufanya na Serikali pamoja na kutekeleza agizo
la Rais Kikwete kwa Wakulima wa Mikoa ya Nyanda za juu kusini ya kuhakikisha
inajikita katika kilimo cha Matunda, Mboga mboga na maua ili kutumia fursa ya
Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kusafirishia mazao yao.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment