Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Monday, May 19, 2014

MTOTO ALIYEIBIWA APATIKANA NA KUKABIDHIWA KWA WAZAZI WAKE

Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Ahmed Msangi akimkabidhi mtoto Yosia Jerome kwa mama yake Orester Shabani 


Mume na mke baada ya kukabidhiwa mtoto wao wakitoka katika ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya


Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya limemtia nguvuni mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Esther Amos(23) mkazi wa Nzovwe Jijini Mbeya kwa tuhuma za kuiba mtoto mchanga  jinsi ya kiume mwenye umri wa miezi miwili.

Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Ahmed Msangi amesema mtoto huyo Yosia Jerome aliibwa Mei 14 mwaka huu alipokuwa na mama yake aitwaye Orester Shaban(24) aliyekuwa akiuza mbogamboga katika soko la Ikuti Kata ya Iyunga Jijini Mbeya majira ya saa tatu asubuhi.

Mbinu aliyoitumia Esther ni kumrubuni mama wa mtoto kwenda kununua samaki huku akimkabidhi shilingi elfu kumi kuwa mbali ya njegere alizonunua kwa Orester pia angehitaji kupata samaki hivyo kumwachia mtoto ndipo alipotokomea naye kusiko julikana.

Kamanda ameongeza kuwa mama wa mtoto alitoa taarifa Polisi kituo cha Iyunga na Kati ambapo juhudi za kumtafuta mwanamke huyo zilianza na kufanikiwa kumpata Kijiji cha Mahenje Wilaya ya Mbozi nyumbani kwa Dada yake Esther.

Baada ya wasamaria wema kusikia taarifa za kuibiwa kwa mtoto wakazi wa Nzovwe walianza kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walianza kufuatilia taarifa za Esther aliyedaiwa kujifungua na yupo kwenye mapumziko ya uzazi kwa Dada yake wilayani Mbozi.

Askari walifuatilia mwenendo wa Esther na kufanikiwa kumkamata Mei 18 mwaka huu majira ya saa saba akiwa na mtoto na alipotakiwa kutoa maelezo alionekana kujikanyaga na hata alipotakiwa kumnyonyesha alishindwa kufanya hivyo badala yake alitoa chupa ya maziwa kwa ajili ya kumnyonyesha.

Baada ya Askari kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa waliitwa wazazi wa mtoto kwa ajili ya utambuzi wa mtoto na baada ya kumtambua Orester alizirai kutokana na kutoamini kile kilichotokea machoni pake kupatikana mwanae akiwa hai.

Mtuhumiwa alisafirishwa hadi Jijini Mbeya kwa mahojiano zaidi na Esther ambapo uchunguzi umebaini kuwa katika maisha yake kabla ya kuolewa amejaliwa kupata mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa na alipoolewa hakujaliwa kupata mtoto ndipo alipodanganya mume wake kuwa ana ujauzito ambapo amekwenda kwa Dada yake kujitazamia.

Mtoto Yosia alifikishwa Hospitali ya Wazazi ya Meta na kwamba Afya yake inaendelea vema.

Kamanda wa Polisi alimkabidhi mtoto kwa wazazi wake Ofisini kwake mbele ya Waandishi wa Habari na Maafisa wa Polisi ambapo alitoa wito kwa wazazi kuwa makini na watoto wao na kutowakabidhi watu wasiowafahamu pia waendelee kushirikiana na Polisi ili kukomesha uhalifu Mkoani Mbeya na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Kwa upande wake Baba wa Mtoto Jerome Nzowa amelishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano mkubwa hata kufanikisha kupatikana kwa mwanae akiwa hai na salama.

Na Ezekiel Kamanga
 Mbeya yetu

No comments: