Baadhi ya viongozi wa madereva toka wilaya zote za mkoa wa Mbeya walihudhuria kikao hicho
Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania
(UWAMATA) kanda ya Mbeya wamelalamikia Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama
Barabarani na Mamlaka ya udhibiti wa nchi kavu na Majini(SUMATRA) Mkoa wa Mbeya
kwa kuwanyanyasa wawapo kazini.
Malalamiko
yao yalitolewa jana na Mwenyekiti wa Madereva kanda ya Mbeya, Damas Mwandumbya,
katika mkutano baina yao na viongozi uliofanyika katika ukumbi wa Miami
uliopo Ilomba Jijini Mbeya mbele ya Mgeni rasmi Kaimu Kamanda wa
Polisi Mkoa Robert Mayala ambaye piani Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa
Mbeya.
Mwandumbya
akisoma risala yao kwa mgeni rasmi alisema wanaotuhumiwa kula rushwa ni pamoja
na Askari Polisi wa kikosi cha Usalama Barabarani wa Wilaya za Rungwe na Mbeya
ambao waliwataja kuwa ni Jane,Vaileth, Shabani, Denis, Hezron na
Azimio pamoja na Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo,
ambaye imedaiwa kuwapa malengo Askari wake ili mgao afikishiwe Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mbeya.
Aliongeza
kuwa Mgao mwingine wa pesa hizo umetajwa kwenda kwa Mkuu wa Usalama Barabarani
nchini na kila Dereva anapokamatwa au kusimamishwa hulazimika kutoa shilingi
elfu tano katika kila kituo anachosimamishwa ndipo gari huendelea na safari.
Alisema
hali hiyo husababisha Madereva kujaza abiria kupita kiasi ili kukidhi
malengo ya waajiri na kumudu kulipa Askari wa Usalama Barabarani na kama
wasipotoa hukamatwa na kutozwa faini au kupelekwa mahabusu hali inayowafanya
kufanya kazi katika mazingira magumu.
Aidha
Madereva hao walimtuhumu Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa Mbeya kwa kuwafukuza
ofisini kwake na kuwa na lugha chafu inayowadhalilisha madereva hali
inayopelekea kugoma au kutishia kugoma kutokana na kauli za kiongozi huyo kwa
lengo la kushinikiza kuondolewa Mkoani Mbeya.
Mbali
ya shutuma hizo kwa Jeshi la Polisi pia Madereva hao walitupia lawama SUMATRA
kwa kuruhusu magari ya aina ya Noah ambayo yameanza kusafirisha abiria
bila kukidhi vigezo hali inayosababisha baadhi ya magari ya abiria aina ya
Hiace kushindwa kufanya kazi kutokana na magari hayo kufanya kazi kiholela huku
Jeshi la Polisi na SUMATRA wakifumbia macho.
Akijibu
risala yao ambayo ilijaa tuhuma, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya Robert Mayala
aliwapa fursa wanaotuhumiwa kujieleza mbele ya mkutano huo uliojumuisha
madereva ili kujiridhisha na majibu.
Mkuu
wa Usalama Barabarani, Butusyo Mwambelo, alikanusha kuwafukuza madereva ofisini
kwake bali alidai kuwa viongozi wanatetea wahalifu hali hiyo isipodhibitiwa
itasababisha ajali ambazo zinaweza kuepukika.
Aidha
alikiri kupokea changamoto na mapungufu aliyoelezwa na madereva hayo kwa madai
kuwa atayafanyia kazi na yeye mwenyewe atajirekebisha ili kuendelea kudumisha
hali ya usalama barabarani pamoja na abiria.
Kwa
upande wake Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mbeya, Robert Mayala, alisema amepokea
malalamiko yao na kwamba Jeshi la Polisi litakutana na Askari wanaolalamikiwa
hasa wa Wilaya ya Rungwe na amemwagiza Mkuu wa usalama Barabarani kurekebisha
kasoro zote ili kila upande ufanye kazi kwa amani.
Alihitimisha
kwa kuwataka Madereva kutii sheria bila shuruti ili kuepusha ajali na kuwataka
madereva wakatae kutoa rushwa na Askari atakaye walazimisha watoe taarifa kwake
kwa hatua zaidi.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment