Serikali
imezitaka Asasi zinazoshughulika na Vijana wanaoshi katika mazingira magumu na
hatarishi kuwajengea uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa.
Wito huo
umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro katika shirika la KIHUMBE
ambapo aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Norman Sigala alipokuwa
anazindua mpango wa kuwajengea uwezo wanafunzi 60 waliomaliza mafunzo ya
ushonaji na ufundi magari baada ya kupata msaada wa vifaa vipya vya kisasa
kutoka shirika la IMARISHA la Marekani.
Mkurugenzi
wa KIHUMBE Ptollemy Mwakanyamale amesema kuwa Asasi yao imekuwa ikitoa mafunzo
ya ufundi lakini wahitimu wake wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa ajira
kutokana na kukosa vifaa vya kufanyia kazi na mbinu za kisasa za kukabiliana na
soko la ajira.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa mradi wa IMARISHA Nchini Bi Colleen Green amesema
analipongeza shirika la KIHUMBE kwa mpango madhubuti wa kuwajengea maarifa
vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi hivyo wao wataendelea kutoa msaada
wa vifaa ili kuwafanya waweze kujiajiri au kuajiriwa ambapo wataondokana na
wimbi la ukosefu wa ajira nchini.
Aidha Bi
Joan Mayer Mratibu kutoka Shirika la USAID anayesimamia mikoa ya Iringa na
Njombe amesema kuwa mpango wa kuwajengea uwezo vijana hao utawafanya vijana hao
kumaliza mafunzo wakiwa na mitaji yao hali itakayowafanya kumaliza mafunzo
wakiwa wameimarika kiuchumi na kuwa na ufanisi mkubwa wa taaluma ya ufundi.
Mkuu wa Mkoa
amesema Asasi za aina hiyo zinasaidia kuondoa vitendo vya kihalifu lakini pia
kuimarisha mapambano dhidi ya Ukimwi ambapo vijana wengi wamekuwa wakiathiriwa
zaidi kutokana na ukosefu wa ajira.
Kandoro
amesema kuwa elimu ya ufundi inawapa wahitimu uwezo wa kuajiri hata watu
waliomaliza ngazi ya vyuo vikuu na wao watakua waajiri kutokana na kumaliza
wakiwa na ujuzi na mitaji yao kutokana na mbinu bora zilizobuniwa ili
kukabiliana na wimbi la vijana ambao wengi wamekuwa wakimaliza mafunzo ya
ufundi lakini wamekuwa wakikosa ajira.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment