SHAHIDI wa tatu katika Kesi
inayowakabili Maaskari wawili na Raia watatu ya unyang’anyi wa kutumia Siraha,
Pasupuret Sreedhar ambaye ni raia wa India na Mhanga wa tukio hilo ameiambia
Mhakama jinsi washtakiwa walivyofanikiwa kuwateka na kuwapora mali zao.
Akizungumza katika kesi hiyo huku
akiongozwa na Wakili wa upande wa Jamhuri, Basilius Namkambe mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Michael Mteite, Shahidi huyo ambaye
hakuweza kuzungumza Kiswahili kabisa hali iliyopelekea Mahakama kumtafuta
Wakili maarufu Mkoani Mbeya, Sambwee Shitambala kuwa Mkalimani wake aliweza
kuwatambua Watuhumiwa wote watano.
Shahidi huyo aliiambia Mahakama hiyo
kuwa Mnamo Januari Mosi Mwaka huu aliwasili Jijini Dar Es Salaam akitokea kwao
Nchini India akitumia usafiri wa ndege wa Shirika la Oman akiwa na lengo la
kufuatilia mradi wa Uchimbaji dhahabu katika Migodi ya Chunya Mkoani Mbeya
inayoendeshwa na kampuni yao ya Otro Mining.
Alisema Januari 3,Mwaka huu alisafiri
kutoka Dar Es Salaam kuja Mbeya akitumia Shirika la Ndege la Precision ambapo
aliwasili majira ya Saa Saba na Nusu Mchana na kupokelewa na rafiki yake Isaya
Mkindi ambaye walielekea naye moja kwa moja hadi Mbeya Hotel alikopata chakula
cha Mchana.
Alisema baada ya hapo alipewa Dereva
aliyemtaja kwa jina la Ezekia ambaye alimpeleka Mwanjelwa kununua Mablanketi
mawili kisha kurudi katika Ofisi ya Rafiki yake huyo ambapo ilipofika majira ya
Saa 10:45 jioni walianza safari ya kuelekea Chunya akiwa na rafiki yake pamoja
na dereva Ezekia.
Alisema wakiwa njiani walipofika katika
Milima ya Kawetere kilomita 20 kutoka Mbeya Mjini walikuta magari mawili yakiwa
yameachana kwa mita 200 ambapo walilipita gari moja na ndipo walipokaribia gari
lingine wakakutana na vijana Wanne ambao mmojawapo aliwasimamisha na kuomba
msaada wa Spana ya kufungulia tairi ya gari yao wakidai kuwa inapancha.
Baada ya kueleza hivyo Wakili wa
Serikali aliiomba Mahakama imruhusu Shahidi huyo kama anaweza kuwatambua
Watuhumiwa jambo ambalo alitekeleza kwa kuwagusa Mshtakiwa namba moja, Tatu,
Nne na Tano kisha kuendelea na kutoa maelezo kuhusu kilichoendelea baada ya
kuombwa spana.
Shahidi huyo aliendelea kusema kuwa
baada ya Dereva wake kuwajibu kuwa hawana spana ndipo Mtuhumiwa namba tatu
ambaye ni Askari Magereza alipotoka na kurudi akiwa na pingu mkononi na
kumfunga Dereva kisha kumshusha kwenye gari na kuelekea naye kwenye gari yao
ndogo.
Aliongeza kuwa baada ya kufanya hivyo
walimshika yeye huku wakimuoneshea panga na kumwamuru asiongee neno lolote
kisha kuhamisha mizigo kwenye gari na kupeleka kwenye gari yao ambayo li
Kompyuta za Mkononi mbili, begi, mablanketi na Simu za Mkononi ambazo kabla
hawajachukua alikuwa ameshawasiliana na Mwenzie aliyoko Chunya aliyemtaja kwa
jina la Jamir Amar.
Alisema akiwa ameshikwa na kuongeleshwa
na watu hao simu yake ilikuwa ikisikika na wenzie ambao waliweza kutoa taarifa
katika Jeshi la Polisi ambalo lilifanikiwa kuwakamata muda mfupi baada ya watu
hao kutokomea na vitu vyao na baada ya wao kuachwa akiwemo Dereva aliyekuwa
amefungwa pingu kuachiwa.
Hata hivyo Wakili wa utetezi katika kesi
hiyo Ladislaus Lwekaza alimuuliza Shahidi huyo kama kweli aliwaona watuhumiwa
wakiwa eneo la tukio na siyo kalishwa maneno alijibu anawafahamu kwa sababu
aliwaona wakifanya tukio kwa sababu ilikuwa jioni kabla jua halijazima.
Wakili Lwekaza aliongeza kuwa
akiruhusiwa kuwabadilisha watuhumiwa mkao wao anaweza kuwatambua Shahidi huyo
alijibu anaweza hivyo akatakiwa kutoka nje ili waweze kuwachanganya ndipo
awatambue jambo ambalo lilipingwa na Wakili wa Serikali kuwa haijawahi kutokea
utambuzi ukafanywa wakati kesi inaendelea kusikilizwa na kuongeza kuwa jambo
hilo hufanyika kipindi cha upelelezi.
Kutokana na hoja hizo Hakimu Mteite
alikubaliana na hoja ya upande wa Mashtaka hivyo kutupilia mbali maombi ya
upande wa mashtaka ya kumtaka Shahidi atoke nje ili wamchanganyie watuhumiwa
kwa ajili ya kuwatambua na kuamuru kuendelea na maswali mengine.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Mshitakiwa
namba moja ambaye ni Askari Polisi PC James mwenye namba F8302 wa Wilaya ya
Mbeya ambaye kabla ya kufikishwa mahakamani alivuliwa Uaskari baada ya
kuhukumiwa kijeshi.
Wengine kuwa ni mshtakiwa namba mbili
kuwa ni Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya, Askari Magereza mwenye
namba B 500 Sajenti Juma Mussa(37) wa Gereza la Ruanda Mbeya,Mbaruku Hamis(29)
Mkazi wa Iyela na Amri Kihenya(38) Mkazi wa Iyela.
Akisoma mashtaka yao Mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, Basilius Namkambe alisema watuhumiwa
hao walitenda kosa hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo
la Mlima Kawetere barabara ya Mbeya Chunya.
Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda
kosa hilo kwa kulizuia gari aina ya Pick Up lililokuwa likiendeshwa na Ezekia
Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye alikuwa na mtu aliyekuwa
akifahamika kwa jina la Sreedhar Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia wakitumia
magari madogo mawili ambayo ni GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari linguine
ambalo lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 aina ya Grand Mark II.
Hata hivyo Kesi hiyo iliahirishwa hadi
Februari 13, Mwaka huu itakapoendelea tena kwa upande wa mashtaka kuwaleta
mashahidi wake.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment