Mwenyekiti wa kijiji cha Shilanga, Romani Tubuke, alisema lilitokea hivi karibuni majira ya saa 9 alasiri wakati marehemu Salome Amosi (20) kupoteza maisha akiwa anafua nguo katika mto uliojirani na kijiji hicho.
Mzee
mmoja mkazi wa kijiji cha Shilanga Wilaya ya Mbeya Mkoani hapa amenusurika
kuzikwa akiwa hai akituhumiwa kumuua mkwewe kwa ushirikina.
Tukio lilitokea hivi karibuni majira ya
saa tisa alasiri ambapo Mzee huyo Pascal Mwanjelanje(75) alinusurika kuzikwa
akiwa hai akituhumiwa kumuua mke wa mtoto wake aliyejulikana kwa jina la Salome
Amosi (20).
kupona kwa mzee huyo kumetokana na
kugoma kwenda sehemu lilipochimbwa kaburi kwa ajili ya mazishi ya marehemu
baada ya kushtukia mchezo mchafu wa vijana waliokuwa wakichimba kaburi.
mzee huyo alishtukia kufuatia tukio la
awali lililotokea Novemba 6, Mwaka huu katika kijiji cha Mshewe Wilayani hapa
ambapo watu Sita akiwemo Mwenyekiti wa kijiji walipandishwa mahakamani
wakituhumiwa kumzika mtu akiwa hai wakimtuhumu kumuua mwanaye kwa ushirikina.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa
kijiji cha Shilanga, Romani Tubuke, alisema lilitokea hivi karibuni majira ya saa 9
alasiri wakati marehemu Salome Amosi (20) kupoteza maisha akiwa anafua nguo
katika mto uliojirani na kijiji hicho.
Alisema baada ya kupata kwa taarifa za
msiba huo familia iliandaa matanga kama kawaida ambapo siku iliyofuata vijana
wa kuchimba kaburi walianza kuchimba majira ya saa sita mchana ambapo kabla ya
kukamilisha walisitisha zoezi hilo na kisha kuandamana hadi walipowaombolezaji
na kuwasihi wanyamaze.
Alisema baada ya watu wote kukaa kimya
ndipo vijana hao walipohoji sababu ya kifo cha marehemu na kutaka majibu ya
kuridhisha ili wakaendelee na shughuli za machimbo ambapo walianza kumuuliza
bibi aliyemlea marehemu ambaye aliulizwa kama mjukuu wake amewahi kuwa na
tatizo lolote lakini alijibu kuwa mjukuu wake hakuwahi kusumbuliwa na ugonjwa
wowote.
Alisema kutokana na majibu ya bibi huyo
vijana hao walimsimamisha pia Mume wa Marehemu Moses Pascal(27) ambaye alisema
yeye binafsi hajui ugonjwa uliomuua mkewe zaidi ya kuletewa taarifa kuwa
amekufa mtoni akiwa anafua baada ya yeye kuachiwa mtoto nyumbani.
Hata hivyo vijana hao hawakuridhika na
majibu hayo na kuamua kumwita mzee Pascal Mwanjilanji wakitaka aeleze sababu za
kifo cha mkwewe lakini aligoma kuzungumza lolote na walipomwita kusogea eneo la
kaburi mzee huyo hakukubali ndipo vijana hao walipoamua kufukia kaburi kisha
kuubeba kinguvu mwili wa marehemu na kuhamishia katika kijiji cha Nungwe kwa
wazazi wa marehemu ambako walichimba kaburi lingine na kutaka kuzika.
Aliongeza kuwa kabla hayo yote
hayajafanyika taarifa zilipelekwa Jeshi la Polisi ambao walifika eneo la tukio
na kuwasihi watulie hadi Serikali itakapopima mwili wa marehemu ili kubaini
ugonjwa uliomsababishia kifo na kisha kuamua ni upande upi unapaswa kuzika na
siyo kung’ang’aniana mwili wa marehemu.
Baadhi ya ndugu wa marehemu walisema
kitendo cha kuhamisha mwili wa marehemu haukufanywa na wao bali ni vijana
waliokuwa wakichimba kaburi ambao hata wao hawakuhusishwa na ugomvi waliokuwa
nao zaidi ya wao kuamrishwa kuondoka eneo la msiba na kuhamia kwao.
Mzee wa mila wa kijiji cha Dimbwe,
Hezron Dimbwe alisema mwenye jukumu la kuzika ni upande wa wafiwa ambao ni ukoo
wa mwanaume aliye muoa na si vinginevyo hivyo kama serikali itaamua wasizike
Familia ya upande wa marehemu italizimika kulipa fidia kijijini kwa ajili ya
kufukia kaburi.
Naye Mume wa Marehemu, Moses Pascal (27)
mkazi wa Uyole Jijini Mbeya alisema mkewe alifikwa na umauti walipokuwa
wameenda kijijini kwao Shilanga kwa ajili ya kilimo lakini kabla ya kifo cha
Mkewe walikuwa wametoka Hospitali kumtibu mtoto wao majira ya saa Tisa alasiri.
Alisema baada ya kurudi nyumbani mkewe
aliaga kwenda mtoni kufua hivyo alimwachia mtoto abaki naye lakini baada ya
muda kidogo akapata taarifa za kifo chake na kwamba alifanya juhudi za
kwenda kumchukua hivyo hakukua na maongezo yoyote kabla ya kifo.
Akizungumzia kuhusishwa kwa baba yake na
kifo hicho alisema ni maneno ya uzushi kutoka kwa watu na kwamba huenda
anahusishwa kutokana na kubaki peke yake katika ukoo wao kutokana na wenzie
wote kufa hivyo kuhusishwa na ushirikina.
Aliongeza kuwa bado baba yake
anahusishwa kufuatia kifo chenye utata cha mtoto wake wa kwanza ambaye
alifariki baada ya kumwagikiwa na maji ya uvuguvugu jambo ambalo pia baadhi ya
watu walimtuhumu baba yake mzazi kuwa ni mshirikina.
Aidha hadi tunaingia mtamboni Mwili wa
marehemu ulikuwa upo katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya
Rufaa ya Mbeya kwa ajili uchunguzi ili kubaini sababu ya kifo cha marehemu ili
baada ya kupata majibu pande zote mbili zielezwe na kufafanuliwa na kukabidhiwa
kwa taratibu za mazishi.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment