Kwa muda wa siku mbili mfululizo, jumatano na alhamisi wiki hii,
jiji la Mbeya lilitawaliwa na dhahma ya moshi na milio ya mabomu ya kutoa
machozi sanjari na maji ya kuwasha, kufuatia kukosekana kwa maelewano baina ya
mamlaka za kiserikali kwa upande mmoja, na wafanyibiashara kwa upande wa pili.
Chanzo kikuu cha sintofahamu hii kilikuwa ni mashine za kuwekea kumbukumbu
sahihi za mahesabu ya kibiashara na utoaji risiti kwa bidhaa zinazouzwa (EFDs).
Filamu hii isiyo ya kufurahisha, kilikuwa tangazo la Mamlaka ya
Mapato nchini (TRA), kutangaza kuwa itakapofika novemba 15, kila mfanyibiashara
atatakiwa kuhakikisha kuwa amefunga mashine hiyo katika duka au sehemu yake ya
biashara. Agizo ambalo liliwalenga wale wote ambao mauzo yao ni zaidi ya
shilingi za kitanzania alfu arobaini na tano (45,000/=). Nirejee tena kwa
herufi kubwa kuwa agizo hili liliwalenga wafanyibiashara wote ambao MAUZO yao
na sio FAIDA yao kwa siku, ni kiasi hicho.
Kutokana na hali hiyo, wafanyibiashara wengi wakaanza kuhoji juu
ya hilo chini chini, na siku ya Jumanne, Mkuu wa Mkoa Bw. Abbass Kandoro, baada
ya kusikia manung'uniko ya wananchi wake chini chini, akaamua kuwaita viongozi
wa wafanyibiashara kuwasikiliza malalamiko hayo. Kikao baina ya pande hizi
mbili, kilifanyika katika ukumbi wa Mtenda, maeneo ya Soweto.
Wafanyibiashara hao wakamueleza Mkuu wa Mkoa juu ya mambo
kadhaa, kubwa zaidi likiwa ni gharama za mashine hizo, ambazo zinaelezwa kuwa
zinauzwa kwa gharama ya kati ya shilingi laki saba hadi nane, ambapo walihoji,
iweje mfanyibiashara mwenye mtaji wa milioni mbili kwa mfano alazimishwe
kununua mashine ya laki nane?
Wakahoji faida za mashine hizo ikiwa zitawasaidia kuongeza
biashara zao au laa, wakitolea mfano kuwa mtu anapolipia chumba, anajua kuwa
atakuwa akitunza bidhaa zake kwa kuziuza na kutengeneza faida, sasa je, mashine
hizo zitawasaidia kimapato kwa namna gani? Zitawasaidia kuongeza faida kwa
namna gani? Wapo ambao waliitaka serikali kama inataka kweli wao wazitumie
mashine hizo, basi iwanunulie na wao hawatisita kuzitumia.
Taarifa ambazo nimezipata toka katika kinywa cha Mkuu wa Mkoa
mwenyewe ni kuwa, aliyachukua malalamiko yao, kuwaahidi kuwa atayawasilisha
mahali husika, na angewaita tena ili kuwajulisha nini kimetoka huko juu, na
aliwaomba wafanye biashara zao kama kawaida.
Taarifa za upande wa wafanyibiashara zinaeleza kuwa, baada ya
mkutano huo na RC, viongozi wa chama cha wafanyibiashara, waliona ni vyema basi
wakawajulisha wenzao juu ya kilichoongelewa huko ambapo walienda wakakodi gari
la matangazo, wakalipia katika mamlaka husika na kuzunguka wakitangaza mjini
kuhusu uwepo wa mkutano wa wafanyibiashara katika viwanja vya Ruanda Nzovwe,
maarufu pia kama CCM Ilomba, lengo likiwa kujadili suala la EFDs na kupeana
mrejeshonyuma wa kikao na Mkuu wa Mkoa.
Hadi hapo kila kitu kilikaa shwari hadi pale ilipotimu siku ya
jumatano asubuhi, ambapo baadhi ya wafanyibiashara walianza kukusanyika katika
eneo ambako mkutano ungefanyika. Lakini wakati wakiendelea kukusanyika, ghafla
gari za doria zikaanza kuonekana maeneo ya Mwanjelwa na Kabwe hadi huko Ruanda
Nzovwe na kilichofuatia hapo, ndio kile ambacho kimesharipotiwa mara nyingi.
Ilikuwa ni mwendo wa mabomu na machozi, maji ya kuwasha, fukuzana za kila kona,
virungu kwa waliokamatwa na kila aina ya mvurugano unayoweza kuieleza.
Zaidi kuhusu tukio hili, unaweza kusoma kwa kubonyeza
http://www.jukwaahuru.com/vurugu-jijini-mbeya-mkuu-wa-mkoa-aongea-na-jukwaa-huru-na-kuzielezea-a-z/
, na baada ya kujikumbusha yote haya, hebu tutafakari kwa pamoja kuwa je,
tatizo hasa lilikuwa ni mashine, Polisi, TRA, wafanyibiashara au nani hasa?
Tukumbuke tu kuwa, tukio la Mbeya mjini, lilikuja ikiwa ni chini
ya wiki moja toka mgomo wa wauza ndizi katika wilaya ya Tukuyu kuanza. Mgomo
huo nao ulisababishwa na wao kupinga kuingezewa kodi katika mikungu ya ndizi
ambapo mkungu mmoja ambao awali ulikuwa unaweza kuununua kwa shilingi 2500
utatakiwa ulipiwe ushuru wa shilingi 1000.
Nionavyo mimi, tatizo haliko kwenye EFDs au kiwango cha kodi
ambacho kinapendekezwa kutozwa. Wala hakiko katika utunzaji wa kumbukumbu za
kibiashara ili kurahisisha watu wa TRA kufanya makusanyo stahiki ya kodi. Kwa
mtazamo wangu, tatizo ni "mbona viongozi na watengaji wakubwa katika mamlaka
mbalimbali hususan serikalini, hawana mashine za kutunzia kumbukumbu za ahadi
zao kwa wananchi?"
Ndio, ikiwa viongozi wangekuwa na mashine za kutunzia kumbukumbu
za ahadi zao kwa wananchi, na kisha kukawepo na mashine (sheria) za kuwawezesha
wananchi kutumia kumbukumbu hizo kuwawajibisha viongozi hao, basi hakungekuwa
na malalamiko ya EFDs kwa wafanyibiashara leo hii.
Tatizo linakuja kuwa, walalahoi hawa au waganga njaa hawa,
wanalazimishwa kuhakikisha wanakuwa na mashine za kutunzia kumbukumbu kwa minajili
ya kuziwezesha mamlaka kuzidi kuwakamua kodi, ambazo baadae hawaoni kama
zinawanufaisha kwa kiwango cha kutosha.
Muuza ndizi sokoni, analipa ushuru kila siku katika soko,
analipa kodi kedekede tangia anapozinunua huko mashambani, kuzisafirisha hadi
kuzipanga, lakini mahali anapoziuza, mifereji ni michafu na ili isafishwe ni
lazima alipie mchango. Akitaka kwenda kujisaidia, anatakiwa kulipia pia huduma
hiyo ya kwenda haja, taka zikizidi sokoni anatakiwa alipie ili zikakusanywe na
kwenda kutupwa. Huyu mnapotaka kumuongezea ushuru, mnamtaka nini kama sio
ubaya?
Hebu waangalie wale wafanyibiashara pale Mbeya. Analipia kodi ya
pango, anapoenda kujisajili kupata namba ya mlipa kodi, anatakiwa apeleke
mkataba wa upangaji sehemu yake ya biashara, na anatakiwa alipie kodi kile
kiasi anachomlipa mwenye nyumba, na wala sio mwenye nyumba anayelipwa ndio
alipie kipato hicho. Analipa ushuru wa eneo analofanya biashara kila siku,
analipia kodi bidhaa anapozinunua, analipa kodi anapozisafirisha, analipa kodi
anapozipanga tu dukani kwake. Huyu mnapotaka anunue mashine inamsaidia kwa lipi
hapo?
Hivi sasa biashara nyingi sana zimekuwa zikienda kombo,
ikielezwa kuwa serikali licha ya kupitisha bajeti, haijaingiza hela kwenye
mzunguko, na ndio maana kwa mfano serikali hiyo inadaiwa karibu na kila
aliyekuwa akiipa huduma. Hawa watu watoe wapi laki nane za kununua EFDs?
Lakini mtu huyu huyu akiumwa anajilipia matibabu, mtaa anaokaa
barabara ni mbovu kupita maelezo, hakuna mitaro ya maji ya kueleweka, hakuna
mifumo mizuri ya utoaji wa maji machafu. Akiumwa akienda hospitali, analazimika
kwenda kununua dawa, akiumwa mwanae ndio hivyo hivyo, akiumwa baba, mama au
ndugu yake yeyote hali ni hivyo hivyo. Hizi kodi za awali anazolipa zinakwenda
wapi? Akinunua mashine, itamsaidia vipi kukuza biashara yake zaidi ya kuweka
kumbukumbu za kuwawezesha TRA kuzidi kumkamua kodi zaidi?
Nionavyo mimi, tatizo kubwa ni kutokuwepo kwa uwiano wa kodi
ambazo tayari zinakusanywa hivi sasa, na upatikanaji wa huduma katika maisha
halisi. Mafanikio mengi yamekuwa kwenye hotuba ya waziri wa fedha
anapowasilisha bajeti na sio katika eehemu ambazo walipa kodi wenyewe wanaishi,
na hili ndio tatizo kubwa.
Ikumbukwe kuwa, mfanyibiashara ni ndugu wa mwananchi wa kawaida
na mfanyakazi. Na kwamba kama huyu mwananchi wa kawaida angekuwa anaziona kodi
zake na za mfanyibiashara zimemletea matunda, hakika angesimama mstari wa mbele
kumshurutisha ndugu yake huyo kununua mashine kwa maslahi zaidi ya wananchi.
Mfanyakazi naye pia angefanya hivyo hivyo, na mwisho wa siku, wafanyibiashara
wangezinunua na kuzifanyia kazi.
Inapotokea kuwa mfanyibiashara anapogoma anaungwa mkono na kundi
kubwa la walio kando ya biashara zenyewe, inamaanisha kuwa hata hawa wasio
wafanyibiashara wanaona kabisa kuwa ndugu zao wanaonewa. Na bahati mbaya sana
ni kuwa, mifano ya namna hii ipo haijasahaulika. Simulizi la zile mashine za
kudhibiti mwendo, ziliishia wapi kama sio ajali kuzidi kuua ndugu zetu hadi leo
hii? Magari yalifungiwa hadi kila moja likawa na kidhibiti mwendo, lakini leo
tuko wapi?
nionavyo mimi, Watanzania tayari wanalipakodi nyingi mno, na
kuwaambia eti wawe na mashine za kutunzia kumbukumbu za biashara zao, ambayo
kimsingi inamaanisha mashine ya kumbukumbu za wanavyokamuliwa kodi na kubakia
watupu, ni kuwataka ubaya zaidi. Kwanza viongozi watuonyeshe mashine za
kutunzia kumbukumbu za ahadi zao, kisha mashine zinazowawezesha wananchi
kuchukua hatua kama hawaridhishwi na utekelezaji wa ahadi walizoahidiwa awali,
ndipo wafanyibiashara nao washurutishwe kumiliki mashine za EFDs.
Kama hatuwezi kuuona kwanza uwiano wa kiuhalisia wakodo ambazo
tayari zinakusanywa na maendeleo ambayo tuliahidiwa, basi tutarajie kuwa hili
la EFDs litakuwa moja ya mambo yatayoleta migogoro zaodo katika zama hizi
ambapo wakubwa wanalazimisha kuwa zinunuliwe na wafanyibiashara.
Kama viongozi hawaoni umuhimu wa wao kuwa na mashine za kutunza
kumbukumbu za ahadi zao, na kama hawaoni umuhimu wa kuktengenezea mwananchi
mashine (sheria) ya kuweza kuchukua hatua dhidi ya kiongozi ambaye anamletea
mambo ya kipuuzi na majibu ya ajabu ajabu pindi anapomhpomhoji, basi sioni
umuhimu wa waganga njaa hawa kulazimishwa kumiliki mashine za kutunza
kumbukumbu za hesabu za biashara zao. Haziwaongezei chochote katika ufanisi wa
biashara zao wala ubora wa huduma za msingi.
--
Ramadhani
Msangi
Founder
& CEO - Jukwaa Huru Media
P.
O. Box 693, Mbeya - Tanzania
Hotline:
+255 767 412 176
URL: www.jukwaahuru.com
|
No comments:
Post a Comment