Wakulima nchini wameaswa kutumia mbegu
zilizofanyiwa utafiti wa kitaalamu ili kuepuka kutumia mbegu feki
zinazokwamisha juhudi za kufikia maisha bora.
Hayo yameelezwa na Bwana Shamba wa Kampuni
ya kuzalisha mbegu ya Highlands Seeds Growers, Idd Kapteni kutoka Chuo cha
utafiti wa Kilimo Uyole kilichopo Mkoani Mbeya, wakati wa mafunzo ya matumizi
bora ya mbegu za kisasa kwa Wakulima wa Mahindi wa Vijiji 12 vya Wilaya ya
Makete Mkoani Njombe yaliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Kapteni amesema Wakulima wamekuwa wakilalamikia
mbegu kutokuota vizuri mashambani kwao licha ya kununua mbegu bora kama
Serikali inavyoagiza pamoja na kufuata kanuni za Kilimo kutokana na mawakala
kutowaelekeza juu ya matumizi bora ya mbegu za kisasa.
Amesema ili kuondoa umaskini wa Mtanzania na
Mkulima kulima kilimo chenye tija ni pamoja na matumizi ya mbegu bora
zilizofanyiwa utafiti na Taasisi ya Serikali na kuthibitishwa pamoja na
kukaguliwa kwa kumuongezea kipato.
Akizungumzia mbegu bora amesema ni pamoja na UH
6303 na UH615 kutoka kampuni ya Highland Seeds ambazo zimefanyiwa utafiti kwa
ajili ya kumudu mazingira ya Tanzania ambazo zinahimili magonjwa na hale ya
Hewa iliyopo Nchini.
Amesema Mbegu hizo baada ya kufanyiwa utafiti
huzalishwa na taasisi za Serikali ambazo ni Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na
Jeshi la Magereza kabla ya kumfikia Mkulima ili kujiridhisha na matokeo
yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Kilimo wa Wilaya ya
Makete, Beda Kusenge, amesema Mkulima anapowaza kuzalisha kitu mbegu ni suala
la msingi na la kwanza kuzingatiwa hivyo suala la matumizi ya Mbegu bora ni
agizo la Serikali linapaswa kuungwa mkono na kila mkulima ili kuendeleza
dhana ya kilimo kwanza kwa vitendo.
Amesema katika uzalishaji Mbegu ina asilimia 30
ukiacha mbolea, madawa na gharama za utayarishaji wa Shamba, na kuongeza kuwa
baada ya kuzingatia hilo Mkulima atarajie mavuno kuanzia asilia 30 bila
kipingamizi cha aina yoyote.
Naye Wakala mkuu wa Mbegu za Mahindi kutoka
kampuni ya Highlands Seeds Growers anayesambaza Wilaya ya Makete, Tito Tweve
amesema Mawakala wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo miundombinu mibovu
ya kumfikishia mkulima mbegu pale walipo.
Amesema kutokana na umbali wa maeneo na
miundombinu mibovu ya barabara hulazimika kuongeza bei ya Mbolea na Mbegu hali
inayosababisha Mkulima kushindwa kumudu kununua Mbegu bora na hatimaye
kulazimika kutumia zisizofanyiwa utafiti.
Ameongeza kuwa pia baadhi ya watu wamekuwa siyo
waaminifu kwa maisha ya Watanzania kwa kuchakachua Mbegu na kuwauzia Wananchi
na kusahau kuwa kufanya hivyo ni kuendelea kumnyonya Mkulima asuyekuwa na
hatia.
Aidha baadhi ya wakulima waliohudhuria mafunzo
hayo wametoa wito kwa Serikali kuwabana wanaochakachua mbegu na kuziuza kwa
kile walichodai kuwa wengi wao hawajui kusoma wala kugundua ubora wa mbegu na
kuishia kushangaa zikishindwa kuota mashambani.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wakulima
watatu watatu kutoka Vijiji 12 vya Halmashauri ya Wilaya ya Makete pamoja
na Mabibi na Mabwana Shamba wao pia walipatiwa mafunzo namna ya kufuata kanuni
bora za upandaji wa mahindi sambamba na kugawiwa kilo mbili mbili za Mbegu za
mahindi aina ya UH 6303 kwa ajili ya mfano kwa kila Mkulima aliyekuwepo.
Mratibu wa mafunzo kwa wakulima,Award Mtandilah
amesema wakulima wanamwitikio mkubwa wa kutumia mbegu bora ambapo wengi wao
wanatoka sehemu za mbali ambazo ni Vijiji vya Isapulano, Ivirikinge,Luvulunge,
Ivalalila, Iwawa, Nduramo, Maleutsi,Kisinga, Ugabwa, Hevelo, Mago, Lupalilo na
Ludihani.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment