Baadhi ya madereva wa Bodaboda wakifuatilia kwa makini zoezi la kutunuku vyeti lililokuwa likifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe.
IMEELEZWA kuwa mafanikio ya jambo lolote
duniani linatokana na kuwaelewesha vijana kwa kuwa ndilo kundi kubwa
ambalo likisahaulika ni rahisi kupata matokeo tofauti na matarajio.
Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Wilaya Rungwe
Crispin Meela wakati wa Zoezi la kuwatunuku Vyeti na Leseni za kuendeshea
pikipiki maarufu kwa jina la Bodaboda vijana 300 wa Wilaya ya Rungwe katika
Hafla iliyofanyika katika Jengo la Halmashauri Tukuyu Mjini.
Meela alisema baada ya kugundua kuwa vurugu
nyingi hutokea kutokana na vijana wengi kutokua kwenye makundi na shughuli
maalumu za kufanya akaamua kuandaa mafunzo kwa Madereva wa Bodaboda ili wapate
Leseni na vyeti ili wajue sheria za barabarani.
Alisema baada ya kupatiwa mafunzo vijana
hao tayari ni kundi maalumu ambalo limeshatambuliwa na ni rahisi kulisaidia kwa
kuwaanzishia miradi mbali mbali itakayowasaidia kuepukana na vitendo viovu hasa
vurugu zinazotokana na Siasa.
Alisema kwa kuanzia atahakikisha Asilimia
tano za Makusanyo ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya Mfuko wa Vijana
zitasaidia kuanzisha Sacoss ambayo kabla ya hapo watapatiwa elimu juu ya
uendeshaji wake ikiwa ni pamoja na kuchagua viongozi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Rungwe,Noel Mahyenga alisema mradi wa Boda boda ni kichocheo kikubwa
cha Wilaya hiyo baada ya vijana wengi kujishughulisha na kuwa tayari kuchangia
shughuli za maendeleo ndani ya Wilaya.
Aliongeza kuwa tayari
Halmashauri imeshapata kundi la Vijana ambalo limejikusanya pamoja hivyo
itarahisisha kuwawezesha na kuwapatia msaada kutokana na kuachana na kazi
zisizo rasmi.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment