Kamanda Diwani akiongea na waandishi wa habari
MTU mmoja ambaye
anasadikiwa kuwa ni jambazi ameuawa kwa kupigwa risasi na Askari wa Jeshi la
Polisi akiwa kwenye harakati za kuteka magari katika Eneo la Mlima Nyoka Jijini
Mbeya baada ya kutokea kwa majibizano ya kurushiana risasi.
Jambazi huyo ni
miongoni mwa watu waliokuwa wakitafutwa na Jeshi la Polisi Mkoani hapa
akituhumiwa kuhusika na mauaji ya Askari Polisi mwenye namba G 68 PC Jafari
yaliyotokea Februari 6, Mwaka huu katika eneo la Matundasi Wilayani
Chunya.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika Mkutano
alioufanya na waandishi wa Habari Ofisini kwake ambapo alisema tukio hilo
lilitokea jana majira ya Saa 10(kumi) Alfajiri usiku wa kuamkia Machi 26,
Mwaka huu.
Kamanda Diwani alisema
kabla ya tukio majambazi wapatao wanne tayari walikuwa wameweka mawe
barabarani kwa nia ya kuteka magari ili wafanye uporaji katika eneo hilo la
Mlima Nyoka ambalo limekuwa na matukio kadhaa ya watu kuporwa mali zao.
Alisema Jeshi la
polisi baada ya kupata habari za kutegwa mawe, askari walifika kwa wakati kwa
kuwa polisi walikuwa jirani na eneo hilo na kuweka mtego kwa kuwa majambazi
hawakuwa wameonekana kwa wakati ule.
Aliongeza kuwa baada
ya muda majambazi walipoona taa za gari walijitokeza tayari kushambulia lakini
kabla ya hapo polisi walitoa amri ya kujisalimisha kinyume chake wakaanza
kupiga risasi ovyo ndipo mashambulizi ya polisi yakafanywa.
Diwani alisema katika
mapambano hayo alijeruhiwa jambazi mmoja kwa risasi kiunoni na ubavuni kulia na
wengine watatu walifanikiwa kutoroka ambapo Marehemu alipowahishwa hospitali
kwa matibabu daktari alibaini kuwa amekwisha fariki.
Alisema jambazi
huyo alikutwa na silaha moja SMG yenye namba AB huku namba nyingine
zikiwa zimefutwa na magazine yake ikiwa na risasi ishirini na mbili (22) pamoja
na mapanga mawili([2).
Aliongeza kuwa baada
ya Marehemu kufanyiwa upekuzi maungoni mwake jambazi huyo alikutwa na
kitambulisho cha mkazi chenye namba B.0010453 chenye jina la Emanuel Blasius
Mdendemi aliyezaliwa mwaka 1984 eneo la Matamba wilayani Makete Mkoa wa Iringa
makazi yake ni Uwemba Mkoani Njombe.
“Jambazi huyu
amebainika kuwa ni miongoni mwa majambazi waliokuwa kwenye mtandao wa majambazi
uliokamatwa hivi karibuni kuhusiana na matukio waliyofanya Mikoa mbalimbali
ikiwemo Mbeya,Njombe na Iringa.aidha amebainika kushiriki katika tukio la
mauaji ya askari polisi PC Jafari wa kituo cha Mkwajuni – Chunya tarehe
06.02.2013.” Alisema Kamanda Diwani.
Aliongeza kuwa
ufuatiliaji wa majambazi waliotoroka unaendelea kufanywa ambapo pia
anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za wahalifu hao azitoe bila
kuchelewa kwa jeshi la polisi ili zifanyiwe kazi.
Pia
amewatahadhalisha majambazi na wahalifu wa makosa yeyote kuachana na
uhalifu kwa kuwa ni biashara isiyo na faida badala yake wafanye shughuli halali
kupata maendeleo ambazo fursa zake ni nyingi.
Picha na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment