WANANCHI wilayani Rungwe wamefurahishwa na kitendo cha mwekezaji
kukubali kujenga kiwanda cha kusindika gesi inayochimbwa wilayani Rungwe mkoani
Mbeya.
Hata hivyo licha kiwanda hicho kujengwa Rungwe Serikali
imesisitiza kuwa gesi hiyo ni mali ya watanzania wote na hakuna mwananchi wa
Rungwe mwenye haki ya kuikatalia isisafirishwe kwenda maeneo mengine ya nchi.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Chrispine Meela aliwahakikishia wananchi kuwa watanufaika na gesi hiyo sambamba na watanzania wengine kwa kuwa gesi
hiyo ni rasilimali ya taifa zima.
Meela ambaye alikuwa ametembelea eneo hilo kwa nia ya kujionea
maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi hiyo aliwaeleza wananchi kuwa
kiwanda hicho ni mali yao na watanzania wote ingawa kinasimamiwa na mwekezaji
ambaye ni Kampuni ya Tanzania Oxgen Limited (TOL) kutoka nchini Kenya.
Alisema kuwa muwekezaji huyo amekubali kufuata sheria na
taratibu zote za uwekezaji pamoja na kushirikiana na jamii inayomzunguka
eneo la mradi katika shughuli zote za maendeleo ya jamii.
“Tena jambo zuri zaidi ni kwamba Mwekezaji huyu amekubali
kufuata sheria na taratibu za uwekezaji pamoja na kutoa ushirikiano na
jamii inayomzungumza ambao ndio ninyi wakazi wa hapa Ikama na Wana-Rungwe wote,
hivyo tunao wajibu wa kukitunza kiwanda hiki kwa kuwa ni mali yetu,” alisema
Mkuu huyo wa Wilaya.
Awali Mkurugenzi wa TOL, McJohn Mbiri, alisema kuwa kiwanda
hicho kitakuwa chachu ya maendeleo ya wananchi wa Rungwe mara baada ya
kukamilika na kuanza kutumika, kwani kitakuwa na uwezo wa kutoa ajira kwa
vijana wenye uwezo wa kufanya kazi.
Alisema kuwa watahakikisha wanatengeneza na kuboresha
miundiombinu inayowazunguka wananchi hao ikiwemo barabara, uboreshaji wa
huduma ya Maji, kuwaingizia Umeme majumbani, kuwaboreshea vyumba vya madarasa
katika shule za msingi na Sekondari pamoja na Zahanati ambayo tayari ilishaanza
kujengwa.
“Niseme mbele ya wananchi wa Kijiji cha Ikama mkiwa chini
ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, hiki kiwanda siyo mali ya Wakenya ni mali ya
wana-Rungwe, na tutashirikiana na wananchi katika shughuli za kijamii ambapo
tayari tumeanza kujenga Zahanati kwaajili ya wanakijiji cha Ikama, baada ya
kumaliza zahanati hiyo tutakarabati vyumba vya madarasa vya shule ya msingi
Isebe na Serokndari ya Itageta,” alisema na kuongeza:
“Pia tutahakikisha umeme unawafikia wananchi wote, miundombinu
ya barabara ambayo ndiyo kiini cha Maendeleo itaboreshwa pamoja na kuboresha
miundombinu ya maji ili wananchi mpate maji afi ya bombani,” alisema Mbiri.
Alisema kuwa gesi iliyopo wilayani hapo ina uwezo wa
kuchimbwa kwa zaidi ya miaka 300 bila ya kuonesha dalili zozote za kuisha hivyo
wananchi wanatakiwa kujivunia uwepo wa kiwanda hicho kwani kitawanufaisha kwa
kizazi kilichopo na kijacho.
Wakazi wa kijiji hicho cha Ikama nao hawakusita kuzungumzia matumani
yao juu ya kuwapo kwa kiwanda hicho ambao walisema kuwa tayari wameanza
kujionea matunda ya kiwanda hicho ambapo ujenzi wa zahanati umeshaanza
jambo walilodai kuwa itawapunguzia mzigo wa kusafiri mwendo mrefu kufuata
matibabu vijiji jirani.
Daniel Mwandeko (60), alisema kuwa kitendo hicho cha kuwapo
kiwanda hicho kinawafanya waamini kuwa wataboresha maisha yao kupitia miradi ya
kijamii inayojengwa na kiwanda hicho kwenye maeneo yao.
“Binafsi nimefurahi kuona
maendeleo yanayotokana na kiwanda hiki, kwanza wakati wakiwa katika ujenzi wa
kiwanda chao tayari wameanza kutujengea Zahanati ya kijiji, hivyo tunaamini
kwamba tutazidi kuboreshewa na miundombinu mbalimbali, ila tu naomba sana
wazingatie suala la kutoa ajira kwa vijana wetu ambao ni wazalendo” alisema
Mzee huyo.
|
No comments:
Post a Comment