KWA UJUMLA MTOTO ANETH SASA ANAENDELEA VIZURI NA ANAKULA CHAKULA VIZURI PIA TAARIFA TULIZOPATA MUDA SI MREFU MAMA YAKE MZAZI YUPO NJIANI KUJA MBEYA TOKA KAGERA
HALI ya Mtoto Aneth Johanes (4) aliyelazwa katika Hospitali ya
Rufaa ya Mbeya kufuatia kuchomwa moto mkono wake wa kushoto na anayedaiwa
kuwa ni Shangazi yake inaendelea vizuri licha ya kufanyiwa upasuaji
uliolazimu kukatwa kwa mkono huo.
Kwa mujibu wa mama mdogo wa mgonjwa anayemhudumia
hospitalini hapo Silvia Salvatory alithibitisha kuendelea
vizuri kwa motto huyo ambapo alisema ilimlazimu kufanyiwa upasuaji
kutokana na mkono huo kukosa mawasiliano na kuonekana kuvunjika.
Alisema taarifa za awali zinaonesha shangazi yake huyo
Bahati Rukangara alianza kumtesa mtoto huyo muda mrefu mara baada ya
kumchukua kutoka kwa wazazi wake wanaoishi Bukoba Mkoani Kagera.
Aliongeza kuwa tangu amchukue kwa wazazi wake
Februari Mwaka huu amewahi kumjeruhi mkono wake wa Kulia hadi kuuvunja
ambapo hadi sasa mtoto huyo alikuwa akitegemea mkono wa kulia ambao nao
umekatwa.
Tukio hilo la kisikitisha lilitokea juzi majira ya saa nne
asubuhi baada ya majirani kusikia yowe la mtoto huyo akiomba msaada kutokana na
mateso na maumivu makali aliyokuwa akiyapata kutokana na adhabu hiyo kutoka kwa
Shangazi yake
.
Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya Thomas Isidori
alisema hali iliyopelekea kukatwa kwa mkono wa mtoto huyo ni siri kati
yake na daktari aliyemhudumia na kwamba sheria ya uuguzi inakataza
kutoa taarifa ambazo ni siri.
Isidori alipoulizwa sababu za mgonjwa huyo kufanyiwa upasuaji
mapema mno hadi kusababisha ulemavu alisema ni suala la kitaalamu ambalo hata
yeye hawezi kulijibu na ni sheria ambayo inawataka madaktari kutunza siri za
wagonjwa.
Hata hivyo muuguzi huyo alizuia kabisa waandishi wa habari
kupiga picha za motto huyo baada ya kufanyiwa upasuaji huo uliosababisha
kukatwa mkono kwa mgonjwa huyo.
Baadhi ya wananchi waliofika Hospitalini hapo kumjulia hali
mtoto Aneth aliyelazwa Wodi namba Nane ambao hawakutaka kutaja majina yao
walilaani kitendo cha madaktari kukimbilia kukata mkono mgonjwa badala ya
kujaribu njia zingine za kunusuru hali hiyo.
Habari kwa hisani ya Venance Matinya, Picha na Mbeya yetu
No comments:
Post a Comment