*Polisi wajikanyaga mahakamani.
*Watoto wachanganywa mahabusu moja na watu wazima.
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbozi
Mahakama ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya imetakiwa kufuta mashtaka ya kesi ya jinai namba 143/2012, inayomhusisha Bwana Paulo Sichone na wenzake 12 kutoka Kijiji cha Myunga, Kata ya Myunga Wilaya ya Momba Mkoani hapa.
Kauli hiyo imetolewa na Wakili anayewatetea washtakiwa Mheshimiwa Edgar Bantulaki, mbele ya mahakama hiyo kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha jalada la mashtaka kwa zaidi ya siku 62, ambapo ni kinyume na sheria namba 201 iliyofanyiwa marekebisho na kuwa 225 akitolea mfano wa kesi namba 12/1979 iliyomhusu Deenan Crispin ambapo mwendesha mashtaka alishindwa kuleza maelezo mahakamani hivyo mshtakiwa kuachiwa huru.
Kwa mujibu wa kifungu hicho washtakiwa wanapaswa kuachiwa huru kutokana na washtakiwa kufikiswa mahakamani huku mwendesha mashtaka akitoa visingizio mbalimbali hali iliyopelekea washtakiwa hao kuendelea kusota mahabusu baada ya kuwanyima dhamana.
Mheshimiwa Wakili Bantulaki ameiambia mahakama hiyo kuwa wateja wake walifikishwa mahakamani hapo Agosti 13 mwaka huu na mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 27 mwaka huu, baada ya Mwendesha mashtaka kudai upelelezi umekamilika na kuomba Septemba 10 mwaka huu kesi hiyo kusikilizwa,hata hivyo kesi hiyo kesi hiyo iliahirishwa tena hadi Septemba 2 mwaka huu kwa madai kuwa jalada la kesi limepelekwa kwa Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa.
Aidha ilipofika Septemba 24 mwaka huu bado mwendesha mashtaka alitoa kisingizio cha kuwa jalada hilo halijarejeshwa na kesi kuahirishwa mpaka Oktoba 2 mwaka huu ambapo pia siku hiyo aliiambia mahakama jalada analo hivyo anaiomba tena mahakama kupanga tarehe ya kusoma maelezo ya awali na kupangwa kusikilizwa Oktoba 15 mwaka huu, ambapo siku hiyo mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa jalada halipo hivyo aliiomba tena mahakama kutaja tarehe nyingine ya kusikiliza kesi.
Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na wakili anaye watetea washtakiwa na kudai kuwa kwa mujibu wa sheria kama mwendesha mashtaka ameshindwa kuwasilisha maelezo kwa kipindi cha siku 60 kesi inapaswa kuondolewa mahakamani na kwamba hakubaliani na maelezo hayo.
Baada ya mabishano ya muda mahakamani hapo, mahakama ilitoa siku mbili kwa upande wa mashtaka kuwasilisha jalada na kama akishindwa basi atakubaliana na upande wa wakili wa washtakiwa na kupanga kesi hiyo kusikilizwa Oktoba 18 mwaka huu.
Wakati huohuo katika hali isiyokuwa ya kawaida watoto wawili wamejumuisha katika kesi hiyo ambapo wapo chini ya umri wa miaka 18 ambao ni Ezebius Sinzumwa(15) na Damasi Sinzuma (17) waliochanganywa katika mahabusu ya watu wazima na kwamba mahakama hiyo haikupaswa kusikiliza shauri hilo ili mahakama husika ndiyo isikilize.
Pamoja na ombi la wakili watoto hao bado wanajumuishwa ma watu wazima ambapo asasi ya haki za binadamu imelaani kitendo hicho kupitia mwenyekiti wake wa Mkoa Bwana Said Madudu.
No comments:
Post a Comment