WATOTO wanaoishi kwenye mazingira hararishi na wasiokuwa na
wazazi wa kuwasomesha mkoani Mbeya, wamepatiwa msaada wa vifaa na kulipiwa ada
ya shule, hali itakayowezesha wanafunzi wapatao 3,500 kuendelea na masomo.
Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya sh milioni 95 ulitolewa
jana na Shirika lisilokuwa la kiserikali lenye kutoa huduma za kijamii la
mkoani hapa, KIHUMBE kwa kushirikiana na Shirika la Kimarekani la Walter Reed.
Wakipokea msaada huo ambao ni viatu, sare za shule, madaftari,
kalamu na seti za vifaa vya hisabati pamoja na ada, walezi wa watoto hao
waliyapongeza mashirika hayo kwa msaada huo.
Mkazi wa eneo la Isanga, Raphael Sanga, alisema ni aibu kuona
watoto wengi wanaishi kwenye mazingira hatarishi wakati wazazi wao wapo na
ukichunguza utakuta wazazi hao walihamia mijini wakidhani kuna unafuu wa
maisha.
“Wazazi wanapaswa wajitambue wana wajibu wa kutunza familia zao,
tatizo kubwa la wazazi wengine ni kuhamia mijini wao na familia zao wakidhani
wataishi maisha bora zaidi kumbe matokeo yake wanashindwa kuwalea watoto wao na
kusababisha wakimbilie mitaani na kuishi maisha ya tabu,” alisema Sanga.
Naye Chiku Mdachi, mkazi wa Soweto, alisema msaada huo
utawasaidia zaidi watoto yatima kwani wataweza kuendelea na masomo.
Meneja wa Kihumbe, Ptolemy Samwel, alisema zaidi ya sh milioni
96 zimetumika kununulia vifaa mbalimbali huku sh milioni 39 wamezitumia
kuwalipia ada wanafunzi wa sekondari, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu
wanaosaidiwa na shirika hilo wakati wanafunzi 2500 wamepatiwa viatu vya ngozi
kwa ajili ya matumizi ya shule.
Samwel alisema wanafunzi waliosaidiwa ni kutoka wilaya za
Chunya, Rungwe, Mbeya vijijini na Jiji la Mbeya ambapo shirika hilo linafanyia
shughuli zake.
na
Christopher Nyenyembe , Mbeya
|
No comments:
Post a Comment