KITENDO cha wanafunzi kukimbia masomo ya sayansi kimechangia kwa kiasi kikubwa kitengo cha maabara katika hospitali ya mkoa kukosa wataalamu wa kutosha.
Mratibu wa Huduma wa Maabara Mkoa wa Mbeya,Dk.Ezikiel Tuya akizungumza na waandishi wa habari, alisema kitendo cha wanafunzi kukimbia masomo ya sayansi ni tatizo kubwa katika kitengo cha maabara.
Alisema, hali hiyo imepelekea kuwepo na upungufu wa wataalamu katika taaluma ya afya hasa vitengo vya maabara katika hospitali nyingi za hapa nchini.
Hali hiyo imekuwa ikichangia baadhi ya vifo vya wagonjwa kutokana na wagonjwa kushindwa kupata vipimo vya ugonjwa kwa wakati na stahiki.
Dk. Tuya ameiomba serikali kushughulikia hali ya ukosefu wa wataalamu wa maabara nchini ili kunusuru maisha ya watanzania wanaofariki dunia kwa kukosa huduma ya vipimo kwa wakati.
Changamoto nyingine inayoikabili huduma hiyo ni uhaba wa vitendea kazi ambapo vifaa hivyo vikipatikana vitarahisisha utendaji kazi kwa watumishi.
Hospitali hiyo ya Mkoa wa Mbeya, ilianza rasmi kutoa huduma za afya mwaka 2001 ambapo mwaka 2002 hospitali hiyo ilipokea vifaa vya maabara vyenye thamani ya shilingi milioni 200 kutoka kwa wafadhili. |
No comments:
Post a Comment