BAADA ya maonesho ya Wakulima (Nanenane) kufikia kilele Agosti 8, Mwaka huu baadhi ya wadau wa sekta ya kilimo Mkoani Mbeya wameanza kutoa maoni yano kutokana na tathimini ya maonesho yalivyokuwa.
Aidha wakulima wa Mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu kusini wametakiwa kutumia vyema elimu wanayoipata katika sherehe za Maonesho hayo na kutafsiri kiuhalisia katika shughuli zao za kilimo kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao yao .
Pia wadau hao wamewatupia lawama Maofisa Ugani kwa kuitokuwa wabunifu badala yake kuendeleza teknolojia za kilimo na mifugo zilizopitwa na wakati ambazo hazimsaidii mkulima kuendana na soko la ushindani.
Pamoja na hayo wakulima wamehimizwa kuondokana na kilimo cha mazoea badala yake watumie maonesho hayo kwa kujifunza na kuelewa namna ya kuanzisha kilimo bora kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo katika maeneo yao pamoja na kuhakikisha wanaungana kwa makundi ili kuongeza uzalishaji na kuwasaidia kupata soko la uhakika ndani na na nje ya nchi.
Mmoja wa wadau wa kilimo Mkoani Mbeya,Akizungumzia mafanikio na changamoto zinazowakabili wakulima wa mikoa hiyo hasa katika sherehe za wakulima nanenane wakati akifanya mahojiano maalumu na gazeti hili, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoani hapa Julius Kaijage alisema wakulima wa mikoa hiyo bado wanakabiliwa na changamoto nyingi licha ya halimashauri zao kuwawezesha kushiriki maonesho hayo kwa gharama nyingi.
Alisema umefika wakati kwa wakulima hao wakaondokana na mtazamo kuwa maonesho ya nanenane kuwa ndio sehemu pekee ya kuonyesha mbinu za uzalishaji wa mazao katika maeneo yao badala yake waende kwenye uhalisia wenyewe.
Aliongeza kuwa asilimia kubwa ya mabanda yaliyoko katika maonesho hayo yamekuwa yakionyesha namna ambavyo wakulima walivyo weza kufikia malengo ya uzalishaji wa kisasa lakini imekuwa tofauti na uhalisia wenyewe kama wanavyo jieleza kwenye mabanda hayo.
Kaijage alisema ni vema sasa viongozi na wataalamu kwa ujumla wakatafakari namna ya kumpatia elimu mkulima ambayo itaweza kumsadia katika shughuli zake za kilimo badala ya kusubiri maonyesho kwani kutasaidia pia kukuza na kuongeza thamani ya mazao.
Alisema mara baada ya maonesho hayo kufikia kilele kunatakiwa kuwepo na mabadiliko kwa wakulima wenyewe kutokana na elimu iliyopatikana kwenye maonyesho hayo.
Aidha mwenyekiti huyo amewataka wakulima hao pia kuungana kwa pamoja ili kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuinua kipato chao.
Katika hatua nyingine Mdau mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Kunzugala aliwataka maafisa ugani katika mikoa hiyo kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima moja kwa moja katika maeneo yao badala ya kukaa maofisini wakisubiri taarifa.
Alitanabaisha kuwa tatizo kubwa la maofisa kilimo wengi wamekuwa wakishinda maofisini badala ya kwenda kwa wakulima kutoa elimu hali inayochangia kudidimia kwa sekta ya kilimo kwa asilimia kubwa kitendo ambacho kinawafanya wakulima wengi kutotumia kanuni bora za kilimo kutokana na kukosa uelewa.
Kwa hisani ya Venance Matinya, Mbeya.
|
No comments:
Post a Comment