SERIKALI imetakiwa kudhibiti biashara inayofanywa na kampuni za wageni za Ving’amuzi ambazo zimeendelea kuwanyonya wananchi hasa wenye vipato duni.
Hayo yameelezwa na wadau mbalimbali waliohudhuria warsha ya elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya utangazaji kutoka analojia kwenda Dijitali katika ukumbi wa Mkapa uliopo Jijini Mbeya.
Mbali na jambo hilo walilalamikia kodi kubwa kwenye usajili na uendeshaji wa televisheni jambo ambalo pia Serikali inapaswa kuliangalia kwa kina na kwamba hawajaridhishwa biashara hiyo kuendeshwa na wawekezaji kutoka nje ya nchi badala ya wazawa ambao wangeweza faida hiyo kuitumia hapahapa nchini tofauti na ilivyo hivi sasa.
Warsha hiyo ambayo ilihudhuliwa na wakuu wa wilaya za mkoa wa Mbeya, Madiwani, waandishi wa habari, walemavu, Viongozi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), viongozi kutoka wizara ya Mawasiliano na wananchi wa kada mbalibali, walisema kuwa kumekuwa na biashara holera.
Walisema biashara hiyo ya Ving’amuzi inafanywa kwa kugawanya vitu ili kampuni hizo ziendelee kupata faida ambapo zinauza King’amuzi peke yake, waya peke yake na antenna pia inauzwa peke yake wakati vitu hivyo vinafanya kazi moja na zinapatikana mahala pamoja.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye Warsha hiyo alisema kuwa wadau waliopata ufafanuzi wa masuala hayo wanapaswa kuwa walimu wa wananchi wengine kuhusu mabadiloko hayo ya utangazaji kutoka analojia kwenda Dijitali.
Akisoma risala kwa niaba ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya, Katibu tawala wa mkoa huo Mariam Mtunguja alisema kuwa wadaun wanaopata nafasi za warsha hizo ni muhimu kuuliza maswali wanayohisi kuwa wanaweza kuulizwa na wenzao.
Kwa upande wake Meneja wa TCRA Kanda ya Nyanda za Juu kusini Deograsias Moyo alisema kuwa mabadiliko hayo yatawaathiri watumiaji wa televisheni hivyo elimu kwa umma juu ya mchakato huo ni muhimu sana ikizingatiwa kuwa mwisho wa urushaji wa matangazo kwa njia ya analojia kwa nchi za Afrika Mashariki ni Desemba 31, mwaka huu.
Naye Afisa Mawasiliano Tanzania kutoka makao makuu (TCRA) alisema kuwa kidunia mfumo wa kidijitali unapaswa uwe umefungwa ifikapo mwaka 2015 lakini nchi za Afrika Mashariki zilikubaliana kuwa iwe Desemba na Tanzania ikaridhia ili kuepuka kuwa jalalala la bidhaa za analojia.
Habari na Kalulunga picha na Joseph Mwaisango |
No comments:
Post a Comment