Habari na Joachim Nyambo,Mbeya.
MWEKA hazina katika halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Ferdnand Manyere(52) anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za serikali kiasi cha shilingi 87,245,420.43.
Taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoani Mbeya Athuman Diwani kwa vyombo vya habari leo(Agosti 5) inaeleza kuwa afisa huyo anashikiliwa kwaajili ya kuhojiwa juu ya ubadhirifu huo.
Kamanda Diwani alisema mnamo Agosti 2 mwaka huu jeshi hilo lilipokea taarifa juu ya ubadhirifu wa kiasi hicho cha fedha kutoka halmashauri ya wilaya ya Mbarali na ndipo walianza kulifanyia kazi na hatimaye kumkamata mtuhumiwa mmoja.
Alisema ubadhilifu huo unadaiwa kufanyika kati ya Aprili na Juni mwaka huu na kubainisha kuwa fedha hizo zilikuwa za miradi mbalimbali na malipo ya wazabuni.
“Mtuhumiwa mmoja Ferdnand Manyere ambaye ni mweka hazina wa halmashauri ya wilaya hiyo amekamatwa na aanaendelea kuhojiwa na polisi.”imeeleza taarifa hiyo
Kamanda huyo amesema baada ya upelelezi kukamilika jeshi hilo litatoa taarifa kwa umma juu ya matokeo na hatua zilizochukuliwa.
Hivi karibuni katika kikao maalumu cha kupitia taarifa ya mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali(CAG) mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro aliitaja halmashauri ya wilayaa ya Mbarali kuwa miongoni mwa halmashauri zisizo na nidhamu katika matumizi ya fedhaa za miradi mbalimbali.
No comments:
Post a Comment