WAKAZI wa kijiji cha Ilundo kata ya Kiwira wilayani Rungwe sasa watajilaumu kwa kuukosa mradi mkubwa wa kiwanda cha matunda kufuatia vurugu walizozifanya mapema mwezi Mei mwaka huu
Kiwanda hicho ambacho ujenzi wake utagharimu shilingi 45,996,000 ikiwa ni fedha kutoka Mpango wa Maendeleo ya kilimo(DADP’s) sasa kitajengwa katika kijiji cha Iponjola kata ya Lufingo.
Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kupitia kikao chake lilipitisha maamuzi ya kuhamishwa kwa mradi huo huku likisisitiza kuwa hali hiyo huenda ikayakumba maeneo yote yanayoonekana kukithiri kwa migogoro.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Meckson Mwakipunga alisema Vurugu za kijiji cha Ilundo zilisababisha wadau kukosa imani ya eneo hilo kuwa na Amani na Utulivu kiasi cha kupeleka mradi unaogharimu fedha nyingi.
Mwakipunga alisema miongoni mwa matukio yaliyowakatisha tama ya kuwekeza katika kijiji hicho ni wanakijiji hao kuvunja jingo la zahanati iliyokuwa mbioni kufunguliwa pamoja na ofisi ya serikali ya kijiji cha kwa madai ya kutomtaka mwenyekiti wao.
“Kufuatia uharibifu wa mali za umma uliofanyika,kamati yangu ya Fedha,Utawala na Mipango baada ya kuliangalia suala hilo kwa kina na kutoridhika na mwenendo wa hali ya usalama unaoendelea mpaka sasa kijijini hapo”
“Iliazimia mradi wa ujenzi wa kiwanda cha matundauliopangwa kuanza utekelezaji 2011/2012 lakini ulikuwa bado usitishwe na badala yake kiwanda hicho kujengwa sehemu nyingine nje ya kijiji hicho” alisema.
Alitaja sifa za kijiji kulikohamishiwa mradi huo kuwa ni pamoja na huduma ya maji ya kutosha,miundombini ya barabara ya uhakika kwa mwaka mzima,umeme kwaajili ya kuendesha mitambo.
Sifa nyingine ni kufikika kwa urahisi na maeneo mengine kunakozalishwa matunda na pia uwezekano wa upatikanaji wa eneo la kutosha kwaajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu ikiwemo majengo.
|
No comments:
Post a Comment