Mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi muungano akiwa nje ya shule akichezea mchanga maana walimu wamegoma
ZAIDI ya asilimia 80 ya Shule za msingi za Mkoa wa Mbeya, zimeanza kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais wao wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Gratian Mukoba lililowataka walimu kubaki majumbani kwao mpaka serikali itakapoyapatia ufumbuzi madai yao.
Imeelezwa kuwa kitendo cha walimu hao kugoma na kushindwa kuingia darasani, kilipelekea wanafunzi wa shule za msingi mbalimbali za Halmashauri ya Mbozi ndani ya Mji mdogo wa Tunduma kuandamana kwa lengo la kudai haki ya kufundishwa ambayo ni haki yao ya msingi.
Wanafunzi hao wa shule 14 za msingi zilizopo katika halmashauri ya Mji wa Tunduma,waliandamana hadi nyumbani kwa Diwani wa eneo hilo Frank Mwakajoka (CHADEMA) ili waeleze matatizo yao ambapo jitihada za kumpa ziligonga mwamba na ndipo walipoamua kwenda kituo cha polisi.
Akizungumza kwa njia ya simu mmoja wa shuhuda aliyejitambulisha kuwa ni Namanyise Adamu, alidai kuwa baada ya wanafunzi hao kufika katika ofisi za polisi walipokelewa na kufanya mazungumzo ambayo maamuzi yake hayakuafikiwa na wanafunzi hao.
Alisema, ndipo kundi hilo la watoto lilipoamua kuondoka na kuelekea katika ofisi za halmashauri ya Mji mdogo wa Tunduma ambapo wakiwa katika safari hiyo kundi la vijana lilivamia maandamano hayo na kudai kuwa ni wazazi ambao walikuwa wanaungana na watoto wao na kuelekea kwenye ofisi za Halmashauri ya mji wa Tunduma na kuiba mali kadhaa kisha kuchoma nyaraka zilizokuwemo.
Aidha, kundi hilo la vijana linadaiwa kupora kompyuta 5 za ofisi, pikipiki yenye namba STK 6264, kumbukumbu na nyaraka mbalimbali sambamba na kuvunja milango ya ofisi zote, kuvunja vioo vya magari ya kubebea taka aina FAW SM 8726, na kuiba betri mbili za gari hilo na gari dogo aina ya Nissan lenye namba SM 2858 mali ya mamlaka hiyo.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani akizungumzia tukio hilo alisema maandamano ya wanafunzi ambayo ni ya amani licha ya kukiuka sheria hayawezi kuhalibu mali za watu na serikali kwa ujumla hivyo polisi wanafanya uchunguzi kuwatia nguvuni wote waliovamia maandamano hayo na kufanya uharibifu huo.
“Tukio hili haliwezi kuvumiliwa kutokana na kuwa maandamano ya wanafunzi hayawezi kupelekea kuvunjwa kwa ofisi za serikali na wala kuiba mali zake bali kuna watu ambao wametumia mwanya huo ili kupora mali hivyo polisi itafanya kazi yake,”alisema.
Aidha Kamanda Diwani alisema mbali ya uharibifu wa mali za Mamlaka ya mji wa Tunduma hakuna madhala mengine yaliyotokea ikiwa ni pamoja na majeruhi au vifo.
Mbali na vurugu hizo, pia Shule nyingi za msingi za Mkoa wa Mbeya zimeonekana kuwa na wanafunzi darasani ambao kazi kubwa waliyokuwa wakiifanya ni kucheza kutokana na walimu wao ambao walipaswa kuwafundisha kutoripoti kwenye vituo vyao vya kazi wakiishinikiza serikali kuwatekelezea madai yao.
Moja ya madai wanayodai kutekelezwa na serikali ni pamoja na mishahara ya walimu iongezwe kwa asilimia 100 ya mshahara wa sasa huku posho ya kufundishia kwa walimu wanaofundisha masomo ya sayansi iwe asilimia 55 ya mshahara wa kila mwezi.
Walimu wanaofundisha masomo ya sanaa kwa asilimia 50 ya mshahara wa kila mwezi huku walimu wanaofundisha kwenye maeneo yanayotambulika kuwa ni ya mazingira magumu walipwe posho ya mazingira magumu kwa asilimia 30 ya mishahara yao.
Kadhalika, walimu hao wameshangazwa na kitendo cha serikali kushindwa kukutana na viongozi wa CWT Taifa ili kujadili juu ya nyongeza ya mishahara na posho mbalimbali za walimu kuanzia Julai 2012 huku ikiongeza posho kwa wabunge wakati walimu wanaidai mabilioni ya fedha kwa miaka mingi, lakini imeshindwa kuwalipa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya,Katibu wa CWT Mkoa Kasuku Bilago, alisema mpaka sasa zaidi ya asilimia 80 ya shule za msingi za Mkoa wa Mbeya zimetekeleza agizo lao la walimu kutoingia darasani kufundisha mpaka serikali itakapo tatua matatizo yao.
Kasuku, alisema CWT kinaamini kwamba serikali ina fedha za kutosha kuwalipa walimu wote, lakini kinachokwamisha mpango huo ni genge la watu wachache kutafuna fedha hizo.
Aidha, Kasuku alisema anashangazwa na kauli zinazotolewa na Naibu waziri wa Elimu Philipo Mulugo za kudai kuwa mgomo wa walimu ni batili wakati mgomo huo umefuata taratibu zote za kisheria.
“Nadhani kiongozi huyu hazifahamu vizuri sheria na taratibu za kazi na ndio maana anakulupuka na kudai kuwa mgomo huu ni batili , ninamuomba Naibu waziri aende darasani akasome na kuelewa sheria na kanuni za kazi zinasemaje haswa kwenye masuala ya mtumishi anapodai haki yake,”alisema
No comments:
Post a Comment