Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Saturday, May 5, 2012

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi ajiuzulu akimlaumu Prof Maghembe kumkwamisha kiutendaji

Mkuu wa wilaya Mbozi aliyeachia ngazi Gabriel Kimoro


Katika kile kinachoonyesha uwepo wa mpasuko baina ya watendaji wa kiserikali, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, Gabriel Kimolo, amejiuzulu wadhifa wake huo huku akitupa lawama kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe kuwa sababu ya yeye kujiweka kando na uongozi wilayani hapo.
Profesa Maghembe, alikuwa akiongoza Wizara hiyo hadi leo mchana alipotangazwa kuhamishiwa Wizara ya Maji, kufuatia mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa Bw. Kimolo, miongoni mwa sababu za kujiuzulu kwake ni pamoja na kitendo cha yeye kukashifiwa na baadhi ya wafanyibiashara wanunuzi wa kahawa wilayani hapo, ambao walifikia hatua ya kumtamkia kuwa hawawezi kuongea na yeye mbwa bali wanaongea na mfuga mbwa, wakimaanisha Waziri maghembe ambaye inadaiwa alikuwa akiwakumbatia.
Kimolo, ambaye anakuwa kiongozi wa kwanza wa wilaya kuachia ngazi katika kipindi cha miaka 20, ya utawala wa CCM, amesema kuwa amekuwa akikosa ushirikiano na Wizara ya Kilimo kwa ujumla juu ya msimamo wake wa kupinga ununuzi wa kahawa mbivu (Red Cherry), kama ambavyo imekuwa ikifanywa na baadhi ya wafanyibiashara wanaopata ridhaa toka Wizarani humo.
Januari 7 mwaka huu, Waziri maghembe, alikutana na baadhi ya wakulima na wadau wa zao la kahawa ambapo msimamo wa serikali ulieleza kuwa hawako tayari kuendelea kuwaona wakulima wakiuza kahawa mbichi kwa wachuuzi hao hali ambayo Bw. Kimolo amesema ilisababisha yeye kuonekana kutothaminiwa msimamo wake na Serikali ya Wilaya na ya Mkoa.
Kadhalika katika maelezo yake ya kujiuzulu, amesema kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa uteuzi unaofanywa na Rais, yeye uteuzi wake ulianza mwaka 2006, na kukoma mwaka 2010 ambapo hadi sasa hakuna uteuzi mpya uliofanywa na Rais jambo ambalo linamfanya ashindwe kupanga mikakati ya kazi kwa maendeleo ya wilaya yake.
Amesema kuwa, hivi sasa ni mwaka mmoja na nusu amekuwa akifanya kazi kwa matukio ya dharura na maagizo toka juu na hivyo kumfanya aonekane kutowajibika vilivyo katika nafasi yake na kwamba ameamua kujiuzulu akiamini kuwa uamuzi wake utalinda heshima yake.
Aidha, inaelezwa kuwa Bw. Kimolo amekuwa ni mtu wa karibu sana na Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa na kwamba kitendo chake cha kujiuzulu kina baraka kutoka kwa kiongozi huyo mstaafu ambapo katika ziara yake aliyoifanya hivi karibuni wilayani Momba katika mji mdogo wa Tunduma, aliteta naye jambo muhimu.
Hata hivyo, tetesi za kutokuwemo katika uteuzi ujao zinaelezwa kuwa ni moja ya sababu zinazomfanya mkuu huyi kuachia ngazi mapema ili kujijengea mazingira ya maandalizi ya kuikubali hali hiyo kabla haijatokea wakati wa uteuzi ambao unatarajiwa kufanywa na rais wakati wowote kuanzia sasa.
Bw. Kimolo mwenyewe, amefafanua zaidi kuhusu uamuzi wake huo akisema kuwa kumekuwa na baadhi ya viongozi wababaishaji na kusababisha serikali ionekane inashindwa kuwatumikia vyema wananchi na kwamba yeye ameamua kuachia ngazi na anakwenda kushughulika na mambo yake binafsi.
Alipotakiwa kueleza kama dhamira yake imejikita zaidi katika siasa, amesema kuwa wakati ukifika kuingia katika mchakato wa kisiasa atafanya hivyo kwakuwa yeye kama mtu yeyote ana uamuzi wake na katiba inamruhusu kufanya hivyo.
"Nimechoshwa na kejeli na mizengwe dhidi ya serikali. Wafanyibiashara wanadiriki kusema kuwa hawako tayari kuzungumza na mbwa bali wanazungumza na mwenye mbwa. Siwezi kufanya kazi katika mazingira ya aina hii. Wananchi waelewe hivyo. Nitabakia kuwa raia mwema na mwananchi wa kawaida kama wengine" alisema Bw. Kimolo.
Amesema kuwa, tayari amemuandikia barua Rais, Waziri Mkuu na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kuwajulisha juu ya uamuzi wake huo.

kwa hisani ya Rashidi mkwinda Mbozi

No comments: