Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Monday, March 12, 2012

POLISI WATOFAUTIANA UKAMATAJI WA DAWA ZA KULEVYA MBEYA




BAADHI ya askari wa jeshi la Polisi mkoani Mbeya wameingia katika mgawanyiko mkubwa kutokana na ukamataji na utoaji taarifa wa dawa za kulevya.

Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo mkoani hapa, zimeeleza kuwa kutokana na kuwepo kwa taarifa za upotevu wa dawa za kulevya zinazokamatwa katika mipaka ya Tunduma na Kasumulu huku wahusika wakishindwa kuchukuliwa hatua, askari wa vyeo vya chini nao wameamua kujiingiza katika mchezo huo mchafu.

Awamu hii askari wa jeshi hilo wakiongozwa na Coplo Simon wa wilayani Kyela wiki iliyopita walikamata dawa za kulevya aina ya Cocain na mtuhumiwa Simon Kairuki kutoka nchini Kenya eneo la Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi kisha kuziandikia taarifa na kupeleka ofisi ya kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya.

Imeelezwa kuwa baada ya kufika na dawa hizo katika ofisi hizo kwa ajili ya kuzikabidhi ndipo ikabainika kuwa dawa hizo hazikutimia kutokana na kiasi kilichokuwa kimeandikwa katika taarifa ya awali.

Dawa hizo zilipopimwa hazikukutwa kilo tatu kama ilivyokuwa zimeandikwa wilayani Kyela bali zilikutwa Kilo moja na gramu nane tu hali ambayo iliwalazimu askari wa ofisi ya kamanda wa polisi mkoani hapo kususia mtuhumiwa na dawa hizo.

Baada ya kutoelewana katika mzigo huo, askari kutoka Kyela waliondoka na dawa hizo sambamba na mtuhumiwa na kurudi wilayani Kyela ambako wameendelea kumtunza mtuhumiwa huyo.

Kikosi kazi cha mtandao wa kalulunga.blogspot.com kilimtafuta Kamanda wa kikosi maalum wa kuzuia dawa za kulevya mkoani Mbeya ASP Mboya ambaye alithibitisha kukamatwa kwa dawa hizo za kulevya na kutokea utata huo.

‘’Mimi nipo safarini Jijini Dar es Salaam lakini ni kweli dawa hizo za kulevya zilikamatwa na kutokea utata unaousema na tulichoshauriana ni kwamba wampeleke mahakamani mtuhumiwa kwasababu kiasi chenyewe ni kidogo na utata ulitokea kwasababu waliandika bila kupima lakini walipopima wakagundua kuwa dawa hizo hazikuwa na uzito kama walivyodhani’’ alisema ASP Mboya.

Alisema licha ya yeye kueleza hayo atafutwe kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi kwa taarifa zaidi juu ya sakata hilo.

Leo kikosi kazi chetu kimetua katika ofisi ya kamanda Nyombi na kuambulia patupu ambapo ilielezwa kuwa alikuwa bado hajarejea mkoani Mbeya kutoka kwenye mkutano wa maafisa wa Jeshi hilo uliokuwa ukifanyika mjini Moshi.

Katibu Muhtasi wa Kamanda Nyombi alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa amuone Staff One ambaye pia hakupatikana ofisini kwake.

Mwandishi alipokuwa akitoka katika ofisi hizo aliomba kuandika jina katika kitabu cha wageni lakini alikataliwa ambapo alipofika getini alikutana na kikosi cha askari wakiwa wamebeba dawa hizo na kuingia nazo katika ofisi ya Polisi mkoani hapa zikiwa zimeshikiliwa na askari aliyejulikana kwa jina la Kachara.

Uchunguzi umebaini kuwa awali dawa hizo wilayani Kyela baada ya kukamatwa zilipimwa katika mzani aina ya Latil (mzani wa saa) ambao ulionesha kuwa zilikuwa na uzito wa kilo tatu lakini zilipopimwa na mzani unaoaminika wa Posta zilikutwa chini ya uzito huo.

Mwenyekiti wa mtandao wa madhehebu ya dini yanayojihusisha na upambanaji wa dawa za kulevya nchini Mchungaji William Mwamalanga alipohojiwa amesema kuwa ameshitushwa na taarifa hizo za kupungua kwa uzito wa dawa hizo kwani taarifa za awali zilionesha msafirishaji huyo alikuwa na kilo tano.

Alisema kuwa kwa sasa kazi ya kupambana na dawa hizo ni ngumu sana kutokana na sheria ya dawa hizo ambayo inamtaka msafirishaji wa dawa hizo kuhukumiwa katika mahakama kuu.

‘’Unajua kikwazo kwa sasa ni sheria ambayo inawapa mwanya mkubwa walanguzi na wasafirishaji wa dawa hizo huku ikiwa imekaa kimya kuhusu wakamataji wanaohusika kubadilisha dawa hizo na kuweka unga wa mihogo’’ alisema Mchungaji Mwamalanga.

Sanjari na hayo ameiomba Serikali kuwaachilia huru watuhumiwa wote wa dawa za kulevya ambao dawa zao zinaonekana kuwa zilichakachuliwa kwasababu sheria inamuumiza msafirishaji huku ikiwaneemesha wanaohusika kuchakachua dawa hizo.

Na Gordon Kalulunga, Mbeya

No comments: