MZEE JAMES SILINJANJE MWOLO (76) MKAZI WA MAJENGOJIJINI MBEYA
SERIKALI iliyopo madarakani imetakiwa kuacha porojo kwenye majukwaa kuhusu kutoa huduma kwa wazee nchini kwani kwa kufanya hivyo ni kujichimbia kaburi siku za usoni
Wakizungumza katika Kongamano la Wazee lililoandaliwa na Asasi isiyo ya Kiserikali ya Tumaini La Wazee Tanzania (TUWATA) ambalo limefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Catholic Youth Centre Jijini Mbeya wamesema serikali imefikia hatua ya kuwasahau wazee amabao kwa uhalisia wameiweka serikali madaraka.
Mzee aliyejitambulisha kwa jina la James Silinjanje Mwolo (76) mkazi wa Majengo Jijini Mbeya kwa uchungu mwingi amesema tangu mfumo wa vyama vingi uanze nchini Tanzania suala la wazee halijatiliwa maanani hata kidogo ukilinganisha na enzi za Mwalimu Nyerere.
Ameongeza kusema wakati akiwa kama Mhandisi wa Vyuma daraja la Pili kulikuwa na haki ambazo wazee walikuwa wakipewa kutoka serikalini kama tiba na chakula tofauti na ilivyo sasa.
Wazee wengine kwa ujumla wao wamesema serikali imewatupa hususani katika suala la tiba wafikapo hospitali usumbufu umekuwa mkubwa, wengine wakilazimishwa kutoa pesa kidogo ili waweze kupewa huduma kwa haraka zaidi hali ambayo wameiita ni “matusi” kwa serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Pia wazee hao wamesema inashangaza kuona serikali imetilia mkazo zaidi kwa watoto huku ikiwasahau wazee bila kujua ama kwa kujua kuwa baadaye watafikia hatua ya kuwa wazee, na ambao hawawalei watoto wengine wamefunguliwa mashtaka kutokana na kosa hilo.
Wazee hao kwa uchungu mwingi wamesema kungekuwepo pia sheria ya kuwabana wasiowatunza wazee ili haki itendeke nchini. |
No comments:
Post a Comment