Hayo yalisemwa juzi na Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya Mjini Raymond Mwangwala alipokuwa akijitambulisha mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo Sokomatola Jijini hapa.
Mwangwala alisema ili chama kionekane na wananchi waendelee kuwa na imani nacho ni kujenga mahusiano mazuri kati ya chama na vyombo vya habari ili wananchi wapate kujua nini chama kinataka kuwafanyia.
Aidha Katibu huyo aliongeza kuwa amekuja na mbinu mpya kutoka Dodoma ambako alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana kabla ya kuhamishiwa Mbeya na kuongoza wakubwa ambao ni wananchi na wanachama wote wa wilaya ya Mbeya Mjini.
“ nimekuja na mikakati yangu ya kuhakikisha kuwa chama kinarudi katika hali yake hivyo nahitaji kupata nguvu kwenu waandishi wa habari kwani nitahakikisha nakuwa jirani na vyombo vya habari na lolote litakalotokea nitawaita tuelezane pamoja na kushauriana kwakuwa na nyie ni wawakilishi wa wananchi,” alisema Mwangwala.
Aliongeza kuwa amekuja na mikakati ya kuendesha chama kisasazaidi kwa njia ya mitandao na kushirikiana na wadau mbalimbali kama wafanyabiashara na wajasiliamali pamoja na kufanya mikutano ya hadhara ili mradi wananchi waone chama kipo.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Mbeya Dr.Mary Mwanjelwa alimsifu katibu huyo kwa kukisalimisha chama kwa vyombo vya habari na kuongeza kuwa ushirikiano aliouanza na vyombo vya habari usije ukaishia njiani kama nguvu za soda.
Alisema pamoja na kwamba jimbo la Mbeya Mjini linaongozwa na chama cha upinzani (CHADEMA) hivyo wanaomba ushirikiano na vyombo vya habari kwa ushauri ili wajue walipokosea ili waweze kulikomboa jimbo kwenye uchaguzi ujao.
Aidha alitoa wito kwa waandishi wa kutotoa habari ambazo zitaleta mtafaruku katika jamii kwa sababu za itikadi za vyama kwakuwa sasa tuko kwenye mfumo wa vyama vingi.
No comments:
Post a Comment