Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bwana Clement Mshana kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Radio Tanzania Bwana David Wakati.
Mzee Wakati aliaga dunia jana, Alhamisi, Desemba Mosi, 2011 kwenye Hospitali ya Regency kwa matatizo ya ugonjwa wa sukari.
Katika salamu za rambirambi, Mheshimiwa Rais Kikwete amesema kuwa amesikitishwa na kuhuzunishwa na habari za kifo cha Mzee Wakati kwa sababu marehemu alikuwa mtangazaji hodari, mzalendo, mwenye mapenzi mengi kwa nchi yake na aliyetumia taaluma yake kwa ujenzi wa nchi yake.
“Nilimfahamu binafsi Mzee David Wakati. Alikuwa kielelezo cha utangazaji ulio bora katika nchi yetu na hata nje ya mipaka ya nchi yetu. Alikuwa mwana-taaluma hodari na aliyetumia taaluma yake vizuri kwa weledi na uzalendo katika ujenzi wa nchi hiyo. Ametoa mchango mkubwa kwa nchi hiyo na ameacha pengo kubwa kwa taaluma ya utangazaji.”
“Nakutumia wewe rambirambi, na kupitia kwako natuma rambirambi kwa wanafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu pamoja na wadau wote wa taaluma ya utangazaji. Napenda kuwahakikishieni nyote kwa dhati ya moyo wangu kuwa naelewa machungu yenu katika kipindi hiki kigumu lakini yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake kwa Bwana Mshana.
Amemalizia Rais Kikwete: “Aidha, napenda kuwahakikisheni kuwa moyo wangu uko nanyi katika wakati huu wa maombolezo, na msiba wenu ni msiba wangu. Naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu Wakati. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
02 Desemba, 2011
1 comment:
Kwa mkongwe kama Mzee Wakati, ingekuwa vyema mwandishi mhusika wa blog hii aandike habari fupi kuhusu yeye nani, alianza lini nk. Hii ni kufaidi vijana au watoto wanaokua sasa ambao hawakumjua. Alikuwa mmoja wa wanahabari wa miaka 1950 na kitu- aliyehusika na harakati za Uhuru, na mtangazaji aliyefanya kazi BBC idhaa ya Kiswahili miaka ya zamani, nk.
Post a Comment