Wananchi wa mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya wawapokea Viongozi wa wilaya, pichani ni moja kati ya mabango yaliyoonekana katika msafara wa mapokezi.
Bwana Andason Minja (Ninja) akiwa ameshika tama huku baada ya kurushiwa tuhuma nzito za kufuja mradi wa maji kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya vijijini Bi Juliana Malange.
Aliyeshika kipaza sauti ni Mwenyekiti wa kijiji cha Mbalizi Bwana Elia Mkono akukimfafanulia jambo Mkuu wa wilaya ya Mbeya Bwana Evans Balama, katika mkutano na wananchi wa mji mdogo wa Mbalizi wilaya ya mbeya vijijini.
Baada ya mkutano kuvunjia Ulinzi ukaimarishwa kwa lengo la kumnusuru na kipigo kutoka kwa wananchi wa wilaya ya Mbeya vijijini Mkurugenzi wa wilaya hiyo Bi Juliana Malange. Mkuu wa wilaya ya Mbeya Bwana Evans Balama(katikati) akiwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya vijijini(Kushoto) Bi Juliana Malange akipembelezwa kupanda juu ya meza kujibu tuhuma zinazomkabili za kufuja mradi wa maji, ambapo alikana tuhuma hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeaya Bwana Evans Balama akiwa hutubia wananchi wa Mji mdogo wa Mbalizi Mbeya vijijini, ambapo alitumia fursa kujibu maswali ya wananchi na kuwaomba radhi kwa mateso wanayoyapata baada ya mradi wa maji kufunjwa.
Wananchi wa Mji mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, wakiwa na mabango yanayoitaka waliofuja mradi wa maji kuurudisha.
* Anatuhumiwa kuwa na mtandao wa wezi kwenye mradi wa maji.
* DC awapigia magoti wananchi,nusura msafara upopolewe mawe.
Na, Godon Kalulunga, Mbeya
Wananchi wanaoishi mji mdogo wa Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini, wanamuomba Rais Jakaya Kikwete kumfuta kazi haraka ama kumwondoa wilayani humo Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Juliana Malange kutokana na kufuga genge la wezi.
Hayo waliyasema jana katika mkutano wa hadhara uliokuwa umeitishwa na Mkuu wa wilaya hiyo Evance Balama kwa nia ya kutatua kero ya maji ambayo wanatozwa kwa amri Shilingi Elfu kumi na Mamlaka ya maji iliyopelekwa kinyemela na Serikali kijijini hapo.
Wananchi hao walimweleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa tatizo hilo limesababishwa na Mkurugenzi huyo ambaye amekiweka Kijiji hicho kama shamba la Bibi la kuchumia fedha bila kushirikiana na wananchi huku akitumia wapambe wake kupora miradi ya wananchi na kujimilikisha ukiwemo mradi huo.
Kabla ya mkutano huo, msafara wa Mkuu huyo wa wilaya ulipokelewa kwa kelele za maji, maji, maji na mabango mbalimbali yakimshutumu Mkurugenzi huyo wa wilaya na watendaji wake wanaosimamia mamlaka ya maji iliyopelekwa kupora mradi wa maji inayoongozwa na Andason Minja.
Baadhi ya mabango hayo yaliandikwa ‘’Tumechoka na bili hewa, ,Hivi maji ni ya Minja na Mkurugenzi, Minja + Gadafi= na uuaji, Wazee wetu walichimba mitaro, Minja tupe maji yetu’’
Wananchi hao zaidi ya Elfu ishirini waliokusanyika katika viwanja vya mahubiri kutoa kero zao walimuuliza Mkuu huyo maswali zaidi ya ishirini ambayo yote hayakupatiwa majibu badala yake Mkuu huyo wa wilaya aliomba radhi kwa yale yote waliyotendewa kabla na baada ya kuhamishiwa yeye katika wilaya hiyo.
‘’Mkuu wa wilaya umelishwa vitu ambavyo huvifahamu na watendaji wako hivyo lazima uwe makini na Mbalizi usije kukosana na watu bure wakati jambo halikuhusu, maana tatizo hili limesababishwa na Mkurugenzi wa wilaya na watu wake akiwemo Minja anayesimamia maji hapa Mbalizi katika mradi wetu ulioporwa’’ alisema Kissman Mwangomale.
Mwananchi huyo na wenzake walihoji na kutaka kujua kuwa tangu mradi huo uporwe Mkurugenzi na wapambe wake wamekusanya kiasi gani na wamefanyia nini na walimtaka Mkuu huyo wa wilaya kuamuru fedha hizo zirejeshwa kwenye Kijiji hicho kwa ajili ya kuendesha mradi wao na kwamba mradi huo urejee mikononi mwa Serikali ya Kijiji.
Naye Elia Kabholile alisema kuwa alishangaa kuona Mkurugenzi ameambatana na Mkuu wa wilaya wakati alikuwa ameitwa na wananchi akawapuuza kutokanana hulka yake ya kuwa na kiburi.
Sanjari na hayo walisema kuwa matatizo yanayowakumba wananchi huku viongozi wa Serikali wakiyapuuza ni kutokana na viongozi wa wilaya hiyo kuishi katikati ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya hivyo taabu zinazowapata hawazioni na kuendelea kuwapuuza.
Alisema yeye alikuwa hana uwezo wa kumfukuza kazi Mkurugenzi wala Meneja wa mamlaka ya maji kwasababu ni Mamlaka zilizoundwa kisheria na Waziri mwenye dhamana na maji.
Kabla hajamalizia hilo huku wananchi wakiwa wamebaini kuwa lilikuwa jibu la kisiasa, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Andason Kabango aliinuka jukwaani na kuchukua kipaza sauti kwa Mkuu huyo wa wilaya na kusema kuwa kwasababu alisema hana mamlaka ya kumfukuza kazi Baraza la Madiwani litaandika barua kwa Waziri mwenye dhamana.
Baada ya hapo Mkuu wa wilaya alimwita Mkurugenzi wake Juliana Malange ili ajibu yale yanayomuhusu na shutuma alizokuwa akitupiwa ana kwa ana na wananchi hali iliyozua mtafaruku baada ya Mkurugenzi huyo kukataa kujibu shutuma zake akiwa juu ya jukwaa la meza.
Kutokana na hali hiyo huku wananchi wakimtaka apande katika meza iliyokuwa ikitumiwa na viongozi wenzake kujibu hoja na kuhoji ndipo akaanza kubembelezwa na viongozi wenzake huku akizomewa na wananchi wakisema kuwa amekuwa sharobaro hivyo aondoke.
Hali hiyo ilileta mzozo mkubwa, huku Mkuu wa wilaya hiyo akiamua kuchukua makarabrasha yake na kuondoka bila mkutano kufungwa huku wananchi wakiendelea kumzomea Mkurugenzi na kutaka kumpiga mawe Meneja wa maji Andason Minja waliyemwita ‘’Ninja’’ aliyekuwa amefishwa katika gari STK 7534 huku msafara huo ukiokolewa na Polisi waliokuwa wakiongozwa na Kamanda wa polisi wa wilaya hiyo Silvester Ibrahim.
Kutokana na ubabe huo wa baadhi ya watendaji wa Serikali ya wilaya hiyo kupora mradi wa maji, hivi karibuni wananchi wa Kijiji hicho walifunga ofisi za mamlaka hiyo ambayo mpaka sasa haijafunguliwa mpaka hapo mradi utakaporejeshwa mikononi mwa Serikali ya Kijiji.
No comments:
Post a Comment