MBEYA YETU,
Napenda kuchukua fursa hii kwanza kuwapa pole Wananchi wa Jiji la Mbeya na vitongoji vyake kwa hari iliyotokea, pili napenda kutoa shukrani zangu na pongezi kwa wamiliki wa hii blog 'MBEYA YETU' kwa kazi kubwa ya kuifanya dunia ione nini kinaendelea jijini MBEYA, natambua kuwa haikuwa kazi rahisi kupata picha za matukio katika uwanja wa mapambano kwa kuwa rungu na risasi za POLISI, mawe yaliorushwa na vijana katika harakati zao hayakuchagua nani zimlenge, binafsi nawapongeza sana.
Binafsi nimekuwa nikifuatilia toka Campinas, Sao Pual- Brasil kwa karibu sana, na nimeona jinsi dunia ilivyokuwa ikifuatilia kwa kuangalia reports on map kwenye hii blog, ukweli inasikitisha sana sana, hakuna atayebisha ukweli MBEYA ni jiji la aina yake sio kama Arusha kuwa utalii unajenga jiji, sio Dar kwamba maofisi, viwanda, Airport na bandari vinamchango mkubwa katika uchumi wake, MBEYA ni biashara ya maduka tena yenye mitaji midogo, na juzi tumetoka kuunguliwa kwa Soko ambalo kwa namna moja au nyingine mitaji iliyotokana na mikopo imepotea na watu kubaki na madeni.
Sasa hizi vurugu katika ukweli wa dhati mimi binafsi nimeteseka sana sana na kuona huruma ya dhati, hata kama napata fursa ya kuandika waraka huu nikiwa nje ya nchi, bado kama mkazi wa ISYESYE Block HH ni lazima tutafute suluhu ya haya. Hakuna biashara inaweza kufanyika kwenye vurugu, na hakuna atakaye faidika na vurugu kati ya VIJANA wala Serikali balini kuwa na mahusiano mabaya na kujenga historia mbaya. Serikali lazima ichukue hatua kwa kuangalia na kuandaa mbadala katika mipango yake hasa inapodili na VIJANA, ukweli usio shaka kabisa kuna tatizo la Ajira kwa Vijana Tanzania.
Bado nina imani na uongozi uliopo katika kutatua tatizo hili, lakini napata mashaka nikitafakari zaidi naona picha ya jazba ilitawala busara katika utekelezaji wa zoezi zima kwani nguvu imetumika na watu wameumia sana kwa pande zote mbili. Mhe Abas Kandoro nategemea utaonyesha uwezo wako na ubobevu wa kuongoza majiji, historia inaonesha wazi umekuwa mkuu Arusha, Dar es Salaam kama kisima cha Wamachinga walikuwepo na waligoma vile vile suluhu ikapatikana na Machinga ComplexIkajengwa, Mwanza alkadhalika machinga waligoma wakati upo pale na sasa hatua za kumaliza hili zinaendelea na Mwanza shwari sasa, sasa hata Mbeya pia nina imani utafanya vizuri kwa kutumia busara na hekima zaidi, ili siku za usoni mkionana na Wamachinga badala ya kuogopana muanze Kutaniana. Ila nakupa pole sana katika hili yangu kwako ni busara na hekima ndio pekee itakuwa tija kwa JIJI la MBEYA.
Hari ya maisha duni, choyo, Upendeleo, ubinafsi, mishahara midogo isiyokizi mahitaji ya maisha[ purchasing power] ndio madhara ya yote haya, kunusuru hali hii serikali jijini Mbeya lazima itafakari kwa kina swala hili bila ya kujali itikadi za kisiasa, ni vema mipango iwe ya wazi na yenye tija kwa maslahi ya jamii ya jiji la MBEYA kwa kuwa 'JIJI LA MBEYA LENYE NEEMA, MSHIKAMANO, KUHESHIMIANA, KUTHAMINIANA, UCHUMI THABITI BILA VURUGU INAWEZEKANA ' Kila mmoja atimize wajibu wake kwa kuzingatia sheria na taratibu.
Imeandikwa na,
Ndugu: Edwin Richard Mwakyembe
1 comment:
daaah wapi kandoro maana namuona DC wa mbeya tuu everywhere huu msala wake ajitokeze hongera pia DC kwani ni mfano wa kiongozi thabiti hujaacha kuwa bega kwa bega hata kama wanakuzomea baba umo tuu
Post a Comment