Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Tuesday, October 25, 2011

WALIMU WAPANGA KUANDAMANA MPAKA KWA MKUU WA MKOA WA MBEYA MHESHIMIWA KANDORO KULALAMIKIA WARAKA KANDAMIZI






MKUU WA MKOA WA MBEYA ABBAS KANDORO
Na Gordon Kalulunga
Walimu waliojiendeleza kielimu hapa nchini wamepanga kufanya maandamano ya amani kupinga waraka kandamizi uliotolewa na Katibu Mkuu utumishi George Yambesi ambao unawashusha madaraja walimu hao wenye shahada na stashahada.

Uamuzi huo umefikiwa jana na walimu zaidi ya 122 ambao walitoka katika mikoa sita ambayo ni Mbeya, Iringa, Ruvuma, Kilimanjaro, Rukwa na Dar es Salaam katika kikao cha pamoja kilichoketi Jijini Mbeya katika ukumbi wa Kiwira Motel.

Wakizungumza katika kikao hicho, walimu hao walisema kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na Serikali kuwapuuza walipotoa siku 30 za kuufuta waraka huo hivyo nji pekee wameona ni kufanya maandamano kwenda kwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro hatimaye Ikulu kuonana na Katibu Mkuu kiongozi ama Rais Jakaya Kikwete.
.
Waraka huo ambao unalalamikiwa ulikuwa la kwanza kuuandika, unawalenga walimu pekee hasa wale wenye sifa za kuwa Maafisa elimu daraja la pili ambao wamerejeshwa kwenye daraja D na hakuna kinachoendelea.

Akizungumzia waraka huo ndani ya kikao hicho, Katibu wa Chama cha walimu mkoa wa Mbeya ambaye alikuwa mwalikwa Kasuku Bilago alisema kuwa walimu waliupata waraka huo kwa njia ya kimafia kwasababu si waraka wa wazi bali ni waraka wa Siri.

‘’Nawaombeni waandishi wa habari kuuweka wazi waraka huu hatari kwa walimu maana hata tulivyoupata tuliupata kimafia na kwa njia ya ajabu huku ukiwa umegongwa mhuri wa Siri na sasa si siri tena’’ alisema Bilago huku akionesha waraka huo.

Alisema mbali na waraka huo, CWT mkoa na Taifa wanaendelea kufuatilia haki zote za walimu ikiwa ni pamoja na mapunjo yao ya mishahara na kulalamikia kodi kubwa zinazokatwa katika mishahara yao.

Naye Mwenyekiti wa CWT mkoa wa Mbeya Nelusigwe Kayuni alisema kuwa mbali na madai hayo, aliwaomba walimu kuwatendea haki wanafunzi wao kwa kuwafundisha kwasababu wanafunzi siyo chanzo cha waraka huo hivyo walimu wasitumie nafasi hiyo kuwakomesha wanafunzi.

‘’Walimu wenzangu najua jambo hili wengi wenu hamlipendi kulisikia lakini nawaombeni tuendelee kuwafundisha ipasavyo wanafunzi wetu maana tukiwaacha tutakuwa tunazalisha kizazi cha wapiga nondo kwasababu wao hawahusiki na waraka huu kandamizi na kuwaferisha wanafunzi si njia ya kuikomoa Serikali kwasababu yenyewe haioni uchungu wowote hata watoto wakifeli hivyo tutakuwa tunadhalilisha taaluma yetu’’ alisema Kayuni.

Kwa upande wao viongozi wa wahanga hao, Mwalimu Simon Bukuku na Mwalimu Stantony Lunyembe, baada ya makubaliano ya walimu wote, walitangaza kuwa watafuatilia kibali Polisi na kutoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya kisha kufanya maandamano hayo Novemba 5 mwaka huu.

“Walimu tumekubaliana kuwa wale waliojiendeleza na kuhitimu mwaka jana nchini kote na wale walioko vyuoni, kuungana kutetea haki zetu hizo za kupandishwa vyeo na kuongezewa mishahara na kuthaminiwa vinginevyo Serikali ichukue maamuzi magumu ya kutustaafisha na kutulipa haki zetu ili tuombe ajira mpya,’’ alisema Mwalimu Bukuku kwa waandishi wa habari.

Alisema kuwa suala hilo likiachwa, litakatisha tamaa walimu kujiendeleza kielimu na kwamba hata matatizo ya wanafunzi kushindwa nchini yanasababishwa na hali kama hiyo kwa sababu ya kuwasumbua walimu katika mahitaji yao ya msingi.

No comments: