Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, October 28, 2011

WAKRISTO WATAKIWA KUJIENDELEZA KIELIMU KWA LENGO LA KUUKABILI UTANDAWAZI

Na Ezekiel Kamanga, Mbeya
Mtume Ayubu Msigwa wa Huduma ya World Alive Ministry (WAM) ya Jijini Mbeya amewataka Wakristo nchini kujiendeleza kielimu ili kwenda na wakati wa utandawazi..

Akihubiri katika huduma hiyo iliyopo Sae Jijini Mbeya, Msigwa maarufu kama “Sauti ya Simba” alisema wokovu sio ujinga kama wengine wanavyofikiria.

“Wapendwa wokovu sio ujinga yaani elimu mnaichukulia kama dhambi?”. Alihoji Mtume Msigwa.

Aliongeza kusema walokole wengi wamekuwa wakifanya shughuli zao bila elimu na kujikuta wakitumbukia katika hasara kubwa na mitaji kufilisika.

Mtume Msigwa alisema chimbuko la wengi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji katika biashara zao ni kutokana na ukosefu wa elimu ambayo ni muhimu katika kuendesha biashara, na kwamba wengine wakienda kwa sangoma hao hujikuta wakipewa masharti magumu kwa mfano ya kuua familia zao wakiamini ndio watapata utajiri.

Pia Sauti ya Simba aliwataka wakristo kusoma Biblia kwani katika kitabu hicho ndimo ulimo ukombozi wao na kusisitiza “mshike sana elimu usimwache elimu aende zake kwani ndiye uzima wako”.

Hata hivyo aliwataka wakristo hao kuachana na tabia ya ulegevu pindi wanapokuwa katika masomo kwani wengine hufikiria kuwa ni dhambi wakikazana kusoma huku wakisubiri miujiza katika kila kitu.

Kwa suala la wazazi na watoto wao Mtume msigwa alisema wazazi wamesahau kuweka misingi mizuri kwa kwa watoto wao hasa suala la elimu, na kudai kuwa wazazi wengi wamekuwa wakiaachia watoto wao vitu ambavyo havitawasaidia maishani mwao na baada ya kufa ugomvi baina ya ndugu na watoto hujitokeza.

Wanafunzi kwa upande wao wametakiwa kusoma kwa bidii wanapokuwa masomoni badala ya kujiingiza katika starehe, na kuongeza kuwa wasimsahau Mungu katika masomo yao, na kwamba wao ni vichwa na si mkia.

Aidha Sauti ya Simba katika Ibada hiyo aliihitimisha kwa kufanya maombi kwa wanafunzi waliokuwepo hapo na wengine kufunguliwa baada ya maombi hayo.

Huduma ya WAM imeanzishwa miaka miwili iliyopita ikianza na watu wanane, lakini hivi sasa ikiwa na zaidi ya waamini 400 kutoka mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

No comments: