Na Mwandishi wetu
Ema Ngwanda mkazi wa RRM mwenye umri wa miaka 36 na Neria Meshaki mwenye umri wa miaka 20 mkazi wa Isanga jijini Mbeya wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za kumchoma moto hadi kufa Hanseni Mtono wakimtuhumu kusababisha hasara ya shilingi elfu hamsini katika baa ya Omega iliyopo Isanga.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa kumi na moja za jioni ambapo watuhumiwa walimfungia marehemu kwenye chumba ambacho kilimwagiwa petroli kisha wakawasha moto.
Naye dada wa marehemu Jackline Mtono amesema kuwa septemba 28 mdogo wake alifungiwa kwenye chumba hicho kwa madai kuwa alisababisha hasara ya shilingi elfu 50 ambazo ni mtaji wa bia na kwamba baada ya mama yeke mzazi kwenda kuongea na wahusika waligoma kumtoa hadi hapo watakapo kuwa wamelipwa fedha zote.
Ameongeza kuwa baada ya siku moja kupita walipata taarifa ya ndugu yao kuchomwa moto akiwa ndani ya chumba alichofungiwa.

No comments:
Post a Comment