Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, October 13, 2011

RAIS JAKAYA KIKWETE APOKEA TAARIFA YA MRADI KABAMBE NA MKUBWA WA UMEME

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
----
· Mradi kabambe wa umeme kujengwa · Rais Kikwete apokea ripoti ya maandalizi · Utagharimu mabilioni ya fedha · Utaunganisha mikoa yote kwenye Gridi ya Taifa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo,(Jana) Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye gridi hiyo.

Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China National Machinery&Equipment Import&Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.

Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300 kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.

Umeme kutokana na mradi huo utaunganishwa kwenye gridi ya taifa na kutoka Singida hatimaye utavutwa kupelekwa katika mikoa ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania ya Kagera, Kigoma na Rukwa ambako pia utaongeza upatikanaji wa umeme katika machimbo ya madini yaliyoko katika mikoa hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mbali na mikoa hiyo mitatu, pia mikoa ya Lindi na Mtwara ambayo nayo haiko katika Gridi ya Taifa nayo itaunganishwa katika Gridi hiyo kupitia umeme huo.

Kuunganishwa kwa mikoa hiyo sita katika Gridi ya Taifa kupitia umeme wa mradi huo pamoja na Mkoa wa Ruvuma ambao utaunganishwa katika Gridi hiyo kwa mradi unaogharimiwa na Serikali ya Sweden kutakamilisha mpango wa Serikali ya Awamu ya Nne kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye umeme wa Gridi ya Taifa.

Kwa sasa Mkoa wa Kagera unahudumiwa na umeme kutoka Uganda, wakati Mikoa ya Kigoma na Rukwa inahudumiwa na umeme wa mafuta ya dizeli. Mikoa ya Mtwara na Lindi inapata umeme wake kutoka kampuni ya Wentworth ambao haujaunganishwa kwenye gridi ya taifa.

Kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.

Akipokea ripoti hiyo, Rais Kikwete ameishukuru Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi zao zilizofanikisha makubaliano ya kujengwa kwa mradi huo mkubwa wa umeme ambao utachangia kuongeza wingi wa umeme nchini katika kipindi ambacho kwa miezi kadhaa Tanzania imekabiliwa na mgawo wa umeme kutokana na ukame uliokausha maji kwenye mabwawa makubwa ya uzalishaji umeme nchini.

Rais Kikwete pia ameitaka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki ya EXIM ya China kuhakikisha kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zinapatikana haraka iwezekanavyo na pia ameitaka TANESCO na makampuni ya CMEC na Siemens baada ya kupatikana kwa fedha kuanza ujenzi wa mradi huo kwa kasi na kuukamilisha katika muda na ubora unaotarajiwa.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,
DAR ES SALAAM.
12 Oktoba, 2011

No comments: