Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Robert Manumba akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mchana huu, katika mkutano na waandishi wa habari juu ya wafanyabiashara wanaojihusisha na kuficha sukari nchini, mkutano huo umefanyika makao makuu ya jeshi la polisi nchini.
---
1. Awali ya yote napenda niwashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuelimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali ya maendeleo na hasa suala la kuzuia na kukabiliana na uhalifu hapa nchini.
2. Jambo kubwa lililoko mbele yetu ni wimbi la kuongezeka kwa uhaba wa sukari hapa nchini, ambapo utafiti umeonyesha kuwa uhaba huo umesababishwa na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kuhodhi bidhaa hiyo ili kusababisha upungufu sokoni.
3. Utafiti pia umeonyesha kuzuka kwa soko la bidhaa hiyo kwenye nchi jirani, hivyo wafanyabiashara wasio waaminifu kwa kuvutiwa na bei kubwa katika masoko hayo kuanza kuvusha sukari kinyume cha sheria na kwenda kuiuza nchi za jirani.
4. Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na taasisi zingine kama vile TRA, Bodi ya Sukari, Uhamiaji, Wizara ya Biashara, TBS, Fair Competition Board, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali na TISS, limeandaa oparesheni maalum ili kuhakikisha kwamba sukari inapatikana kwa kiwango cha kuridhisha katika soko la ndani na kwa bei elekezi iliyokubaliwa na wadau wote husika.
5. Tunawaonya wafanyabiashara wote wanaojihusisha na kuficha, kusafirisha sukari nje ya nchi kinyume cha sheria ama kuuza sukari hiyo kinyume na bei elekezi waliyokubaliana kuacha tabia hiyo mara moja, yeyote atakayekaidi na kuendelea kufanya uhalifu huo atakamatwa na hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.
6. Tunawaomba wananchi wote kutuunga mkono ili kuhakikisha kwa pamoja tunakomesha tabia hii ya wafanyabiashara wachache wasio waaminifu wanaojihusisha na biashara za magendo hata katika bidhaa zingine
No comments:
Post a Comment