Na Esther Macha, Mbeya
WATU wawili wakazi wa kijiji cha Italazya kata ya Ilembo Wilaya ya Mbeya wameuwawa kikatili kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali baada ya kuiba Jenereta lenye thamani ya sh. 150,000.
Imeelezwa kuwa vijana hao ambao ni wezi sugu waliiba jenereta hilo june 18 mwaka huu majira ya saa 11 alfajiri katika kijiji cha Italazya baada ya kuboa nyumba ya Mkazi wa kijiji hicho aitwaye Hyera Kanani na kufanikiwa kuiba Jenereta hilo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Italazya Bw. Aloni Omary alisema kwamba watuhumiwa baada ya kuiba jenereta hilo walikamatwa na mwenye mali ambapo alipiga kelele za kuomba msaada kwa majirani na hivyo kujitokeza wananchi na kuanza kuwashambulia .
Alisema kuwa baada ya mwenyekiti kuzidiwa nguvu na wananchi hao waliendelea kuwapiga kisha kuwachoma moto watuhumiwa hao kisha wananchi kutokomea kusikojulikana.
Aidha Mwenyekiti huo aliwataja wezi waliochomwa moto na wananchi kuwa ni Frank Jonas (26), Fikiria Lyarambo(33) wote wakazi wa kijiji cja Itarazya kata ya Ilembo wilayani Mbeya.
Alisema kuwa katika kijiji cha Italazya kumekuwepo na wimbi kubwa la ujambazi kiasi kwamba kuwafanya wananchi waishi bila amani kijijini hapo , na kuwa hata vijana waliochomwa moto wamekuwa wakihusishwa katika matukio kadhaa Wilayani Mbozi.
Akithibitisha tukio hilo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Bw.Anecletus Malindisa alisema jeshi la polisi linafanya uchunguzi wa tukio hilo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
No comments:
Post a Comment