Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Saturday, August 13, 2011

Mkakati wa Ngeleja wawakuna wabunge



MPANGO wa dharura wa Serikali wa kumaliza mgawo wa umeme nchini utakaowezesha kuzalisha megawati 572 za nishati hiyo kati ya sasa hadi Desemba mwaka huu utagharimu Sh bilioni 523.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amelieleza Bunge leo mjini Dodoma kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limekopa fedha hizo kwa kudhaminiwa na Serikali.

Ngeleja amewaeleza wabunge kuwa, katika kipindi hicho, Tanesco watapata Sh. bilioni 115 kwa kuuza umeme, hivyo Serikali imeamua kutoa Sh bilioni 408 ili kufikia kiasi hicho cha fedha kinachohitajika kuutekeleza mpango huo.



“Mpango huu ni aghali, ni wa gharama” amesema Ngeleja wakati akiutangaza mkakati wa dharura wa kumaliza mgawo wa umeme sanjari na kutoa majumuisho ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012.


“Ukweli ni kwamba tutafika mbali” amesema Ngeleja na kusisitiza kuwa, mpango huo ni kwa ajili ya manufaa ya taifa. Amewaomba Watanzania wawe na imani na pia wabunge waamini kwamba, Serikali inafanya kazi.


“Nishati ya umeme ni nyenzo muhimu sana katika ustawi wa taifa lolote lile” amesema Ngeleja na kubainisha kwamba, Tanesco wamekopa kwa kuzingatia gharama za kibiashara za mikopo hiyo.


Wabunge wameelezwa kuwa, endapo mpango huo utaendelea kutekelezwa hadi mwakani, gharama za kuanzia Januari hadi Desemba 2012 zikijumlishwa na za sasa zitafikia Sh. Trilioni 1.2


Ngeleja amewaeleza wabunge kuwa, Serikali imeamua kwa dhati kuutekeleza mpango huo kwa kuwa, gharama za kutokuwa na umeme ni kubwa zaidi kuliko zile za kuwa na umeme ghali.


Amesema, awali Serikali ilidhamiria kuongeza uzalishaji wa umeme hadi kufikia megawati 300, hivyo mkakati huo wa kumaliza mgawo Tanzania ukitekelezwa kutakuwa na ziada ya megawati 272 kati ya sasa hadi Desemba mwaka huu.


Bunge limeelezwa kuwa, sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo utahusu uzalishaji wa megawati 112 za umeme hadi mwishoni mwa mwezi huu kwa kuzingatia mkataba kati ya Serikali na kampuni ya Symbion Power.


Ngeleja amesema, wakati bajeti ya Wizara hiyo ilipokuwa ikiahirishwa Julai 18 mwaka huu, kampuni ya IPTL ilikuwa ikizalisha megawati 100 za umeme lakini sasa wanazalisha megawati 100.


Amesema, Tanesco na kampuni ya Aggreco International wamesaini mkataba wa kuzalisha megawati 100 za umeme, mitambo imeshaletwa nchini, imeanza kufungwa, na kwamba, wahusika wametakiwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuharakisha utekelezaji.


Kwa mujibu wa Ngeleja, kampuni ya Symbion imesaini mkataba na Serikali ili izalishe megawati 205 za umeme kati ya sasa hadi Desemba zikiwemo megawati 45 zitakazozalishwa Septemba, 110 Oktoba na megawati 50 Desemba.


Ngeleja amesema, katika mkakati huo wa dharura, Serikali imesaini mkataba na Shirika la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF) ili lizalishe jumla ya megawati 150 katika ya sasa hadi Desemba zikiwemo 50 zitakazozalishwa Septemba, 50 Oktoba, na 50 Novemba.


Amewaeleza wabunge kuwa, megawati 572 zitakazozalishwa katika mpango huo wa dharura kati ya sasa hadi Desemba mwaka huu zitaliwezesha taifa kuwa na jumla ya megawati 1,100.


Amesema, ongezeko hilo litaongeza ukubwa wa mahitaji ya nishati hiyo kwa kuwa, kwa mujibu wa wataalamu, ukizalisha umeme kwa kiasi kikubwa, na ukiwa na mfumo mzuri wa kuwafikishia watumiaji, matumizi nayo yanaongezeka.


Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Serikali imedhamiria kwa dhati kuacha kuzalisha umeme kwa maji, na kwa sasa asilimia 55 ya umeme unaotumika nchini unazalishwa kwa maji.


Amesema, Serikali itawekeza kwenye umeme unaozalishwa kwa gesi kwa kuwa, unapunguza zaidi ya asilimia 50 ya gharama zinazotumika kuzalisha nishati hiyo kwa mafuta.


Ngeleja amesema, ili kutekeleza mkakati huo, Serikali imesitisha utekelezaji wa baadhi ya miradi ili fedha zigharamie utekelezaji, na pia Wizara ya Nishati na Madini imepunguza Sh. Bilioni 10.3 katika bajeti yake zilizokuwa zitumike katika masuala mengine zikiwemo posho.

Habari Leo

No comments: