Wananchi katika jimbo la Songwe wilayani Chunya mkoani Mbeya,wameilalamikia ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya hiyokwa kitendo cha kumlinda mmliki mmoja wa Duka la Dawa muhimu katika kijiji cha Muheza ambaye ameligeuza kuwa zahanati.
Duka hilo kwa muda wa miaka mitatu limekuwa likiendesha huduma za zahanati kinyume na sheria kwa kulaza wagonjwa ambao hufika hapo wakiwa hoi kutokana na maradhi mbalimbali,pia inadaiwa kuwa wahudumu wake hufanya shughuli haramu ya utoaji mimba.
Wakizungumza na timu ya waandishi wa habari waliofika jimboni humo kwa msaada wa Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP),walidai kuwa wanalazimika kwenda hapo kutokana na kutokuwepo kwa zahanati katika vijiji vya kata hiyo ,huku wakishindwa kusafirisha wagonjwa kwenda Hospital Teule ya Mwambani kutokana umbali.
Wananchi hao wameongeza kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaofika katika duka hilo hususani watoto wadogo,wamekuwa wakipoteza maisha na wahudumu wake bila kujali sheria za nchi wamekuwa wakifanya kazi ya kutoa mimba bila kificho.
Pia imebainika kuwa zahanati hiyo bubu inawatumishi wawili tu ambao wote kitaaluma ni wahudumu wa afya ambao wamekuwa wakitoa huduma za kitabibu ikiwemo kulaza wagonjwa.
Jitihada za kumpata mmliki wa zahanati hiyo aliyetambulishwa kwa jina moja tu la Michael hazikufanikiwa ,badala yake alijitokeza mdogo wake aliyejitambulisha kwa jina moja la Scola ambaye hata hivyo hakutoa ushirikiano.
Mganga mkuu wa wilaya ya Chunya Wedson Sichalwe,alikiri kuwepo kwa duka hilo na kwamba tayari lilishafungiwa,maelezo ambayo yanapingana na ukweli kwa kuwa hadi sasa duka hilo linaendelea kufanya kazi hiyo.
No comments:
Post a Comment