Na Tiganya Vincent, Dodoma
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, ametoa wito kwa wakulima na wafugaji kuzingatia utunzaji wa mazingira na matumizi ya teknolojia ya kisasa ili uzalishaji uwe endelevu.
DKT Sheni alitoa kauli hiyo leo mjini Dodoma katika kilele cha sherehe za wakulima za nane Nane.
Alisema kuwa ni vema wakulima na wafugaji kutumia maarifa waliyopata katika maonyesho ya mwaka huu katika kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika shughuli zao.
Dkt Sheni aliongeza sekta hizo zinapaswa kuibua vikundi vya ushirika ili kutoa fursa za ajira kwa wananchi ili kusaidia katika juhudi za Serikali za kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
Alisema lengo la kuwafanya wakulima na wafugaji kuwa na ushirika ni kutaka wengi wao washiriki katika mashindano ya kilimo na ufagaji wa kisasa unaolenga kulea tija zaidi.
Dkt Sheni alitoa wito kwa waandaji wa sherehe za wakulima nane nane kuanzisha shughuli hizo kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa ili kuwashirika wananchi wengi na hivyo kuchochea maendeleo
Katika hatua nyingine Dkt Sheni amesema sekta ya kilimo na ufugaji nchini imekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia pato la taifa.
Alisema sekta hiyo katika kipindi cha mwaka jana, sekta ya kilimo ilichangia kwa asilimia 24.1
Alisema mchango wa sekta hiyo umekuwa ukikuwa mwaka hadi mwaka tangu uhuru, na kwamba kuanzia mwaka 1961, mchango wa sekta ya kilimo kwenye pato ghafi ulikuwa asilimia 70.
Hata hivyo, Rais huyo wa Zanzibar, alisema katika mapato ya fedha za kigeni, sekta ya kilimo nchini ilichangia zaidi ya asilimia 75 kwenye pato ghafi (GDP).
Akifafanua, Dk. Sheni alisema sekta hiyo imekuwa na mafanikio makubwa, ambapo katika miaka ya 1970 hadi mwishoni mwa miaka ya 1990, kilimo kilikuwa kwa wastani wa asilimia 3.1.
Aidha, alisema kati ya mwaka 1995 na 2005, kilimo kilikuwa na kufikia asilimia sita, na kwa mwaka 2010, kilikuwa kwa asilimia 4.2, ikilinganishwa na asilimia 3.2 mwaka 2009.
Kuhusu migogoro ya wakulima ya wakulima na wafugaji nchini, Dk. Sheni alitaka kutengwa kwa maeneo maalumu kati ya wakulima na wafugaji kwa kuwafanya waendeleze shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Alisema hata pale inapojitokeza migogoro baina ya makundi hayo, vyombo husika vya serikali vichukue hatua za haraka ili kukabiliana na matukio ya uvunjifu wa amani, ambapo mara kadhaa yamesababisha uharibifu wa mali na hata vifo.
Awali, katika hotuba yake, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, alisema serikali inafanya jitihada za kukifanya kilimo nchini kuwa na tija kwa wakulima na wananchi kwa jumla.
Profesa Maghembe alisema japokuwa sekta ya kilimo imekuwa ikikuwa mwaka hadi mwaka, jitihada zinazofanyika hivi sasa ni kuhakikisha ukuaji huo unakuwa na tija kwa mkulima wa kawaida.
Alisema mojawapo ya changamoto hizo ni kuwa pamoja na kilimo kuhusisha idadi kubwa ya wananchi, lakini uzalishaji wa mazao ya kilimo ni mdogo na hivyo kutokuwa na tija inayotarajiwa.
Waziri huyo alitoa mfano wa kilimo cha mahindi, ambapo alisema wakulima wamekuwa wakipata kilogramu 300 hadi 600 kwa hekta, tofauti na nchi nyingine ambapo mkulima huvuna kati ya kilogramu 3,000 hadi 6,000 kwa hekta kwa mwaka.
Alisema hali hiyo ni changamoto kubwa kwa wakulima na serikali kwa jumla, ingawa jitihada zimekuwa zikichukuliwa kwa kuwahimiza wakulima kufuata kanuni bora, matumizi bora ya mbegu na pembejeo ili kuinua kiwango cha mavuno kwa eneo.
Hata hivyo, Profesa Maghembe alisifu juhudi za wakulima nchini za kujitosheleza kwa chakula, na kwamba lengo ni kuhakikisha ziada ya chakula hicho kinauzwa nje ya nchi ili kuiingizia taifa fedha zaidi za kigeni. |
No comments:
Post a Comment