26/7/2011SERIKALI imewataka viongozi wa Mchezo wa Pool table nchini kuwaelekeza wachezaji wao ili wajue muda muafaka wa kuchezwa kwa mchezo huo jambo ambalo litawafanya waachane na tabia ya kucheza wakati wa kazi.
Wito huo umetolewa jana na waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja wakati akikabidhi zawadi kwa wabunge washindi wa mchezo huo zilitotolewa na Chama Cha Pool Tanzania (TAPA) katika hafla fupi iliyofanyika nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma.
Waziri Ngeleja alisema kuwa hivi sasa mchezo huo umekuwa ukichezwa muda wowote hasa wakati wa kazi jambo ambalo limewafanya viongozi na baadhi ya wananchi kuulalamikia kuwa unapoteza nguvu kazi ya taifa.
“Nawaomba mfikishe ujumbe kwa wachezaji na mashabiki wenu ili wajue muda muafaka na kupanga ratiba ya kucheza Pool table na si kucheza muda wowote hasa wakati wa kazi na hivyo kupoteza nguvu kazi ya taifa”, Ngeleja akiwaambia viongozi wa TAPA .
Naye Kapteni wa timu ya Bunge Idd Azan ambaye ni Mbunge wa Kinondoni aliwapongeza viongozi wa chama hicho kwa jitihada wanazozifanya za kuutangaza mchezo huo na kuahidi kuwapa ushirikiano zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho Isaack Togocho alisema kuwa anafurahi kuona kuwa wabunge wameupokea kwa moyo mkunjufu mchezo huo na anaamini kuwa watakuwa mabalozi wao wazuri .
Waliokabidhiwa zawadi ni mshindi wa jumla wa mashindano hayo George Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe alikabidhiwa zawadi ya ngao na fimbo ya kuchezea POOL na mshindi wa pili Dkt. Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa alipata zawadi ya fimbo ya kuchezea pia timu ya bunge ilipata zawadi ya ngao kwa ajili ya kukubali kwao kushiriki mashindano hayo.
Mashindano hayo yalidhaminiwa na bia ya Safari Lager ilikuwa ni kati ya timu ya bunge na combine ya TBL na TAPA yalifanyika Jumamosi iliyopita mjini Dodoma.
Na Anna Nkinda – Maelezo, Dodoma.
No comments:
Post a Comment