Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KIKUNDI cha wanenguaji mahiri wanaojulikana kama Khanga Moja Ndembe ndembe na Kitu Tigo wanatarajia kufanya onyesho la aina yake katika Ukumbi wa Arusha City Park Jumamosi ya Julai 30, kuanzia saa tatu za usiku hadi majogoo.
Khanga Moja na Kitu Tigo wanazidi kujipatia umaarufu mkubwa hapa nchini hasa maeneo ya jiji la Dar es Salaam kutokana na aina yao ya uchezaji inayowaacha hoi wadau na mashabiki wa muziki wanaokwenda kuwaona mabinti hao.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa onyesho hilo, Karen , akiwa chini ya Kampuni ya ONE2B Entertainment , alisema shoo hiyo itakuwa ya aina yake kutokana na mikakati yao kabambe, wakiwa na maana ya kuwaonyesha wadau wa jijini Arusha, umakini na vipaji vya wakina dada hao wa Khanga Moja na Kitu Tigo.
Alisema kufanya vema kwa mabinti hao sehemu mbalimbali za Tanzania kumewafanya na wao watamani kuwapatia burudani hiyo mashabiki wa jijini humo, ukizingatia kwamba watakua wakichuana vikali na kuwaona mabinti hao ni burudani tosha.
“Nadhani mashabiki wa muziki wa jijini Arusha hasa kupitia unenguaji wa wakina dada hao wa Khanga Moja na Kitu Tigo wanaotamba nchini wakifanya makubwa katika kulishambulia jukwaa wakivalia vazi la khanga linalotoa macho wadau wengi.
“Nawaomba mashabiki wote bila kujali itikadi zao kuja kwa wingi katika onyesho hilo maalumu kwa ajili yao, likiwa la mwisho kabisa katika kuelekea mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan, hivyo nadhani mashabiki watafurahia burudani hiyo,” alisema Karen.
Khanga Moja wanaofahamika pia kwa jina la Laki si pesa wameibuka katika siku za hivi karibuni na kuchengua wengi wanapokuwa jukwaani wakicheza kwa ubinifu wa hali ya juu, bila kusahau aina yao ya kucheza wakiwa wamevaa khanga. Wakati Kitu Tigo wao wanafahamika zaidi kwa jina wakali wa kuchezesha nyonga .
Kufanyika kwa onyesho hilo la watoto wa khanga moja ndembendembe na Kitu Tigo wakali wa nyonga jijini humo ni nafasi ya kuonyesha makali yao kwa watu wa huko, ikiwa ni baada ya kutokea mkoani Tanga kwa Wagosi wa Kaya, wakifanya shoo pia mjini Korogwe.
No comments:
Post a Comment