…..Kama kawaida Mungu anatupenda watanzania…… 
…….Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika…….
   Leo  tunapoadhimisha  siku  ya wajinga duniani nimetafakari kwa kina je kwa Tanzania siku ya  wajinga ni lini? kwa jinsi hali ilivyo kama watanzania tukizama kwenye  fikra zetu tukawaza na kuwazua haina ubishi kuwa sisi hatuna siku  maalumu ya wajinga bali kwetu ni kila uchao.
    Chukulia mfano wa hizo sentensi mbili hapo juu ya kwanza hiyo ya ….kama kawaida Mungu anatupenda watanzania….hupenda  kusemwa na viongozi wetu pale wanapozungumzza mambo ya kitaifa au  wakihojiwa na vyombo vya habari na sentensi ya pili hiyo ya….Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika..inatumika  na waandishi wetu katika kurasa za magazeti yao na siku hizi imeanza  kuwakolea viongozi wetu wakuu wanapotoa hotuba za kitaifa.
   Lakini  hebu tufanye hesabu rahisi tu za kujumlisha na kutoa , tunaposema Mungu  anatupenda tuna maana gani? Mimi nadhani viongozi wetu wanatuchezea kwa  maana kuwa matatizo makubwa ya kitaifa yanayodhuru watu wanayaremba kwa  msemo huo ili yawe madogo kwa maana ya kawaida tu wanapenda kutoa  majibu mepesi kwa hoja nzito halikadhalika wanatoa majibu ya zamani kwa  maswali mapya, Mungu alitupenda watanzania ndio maana katuumba na  utajiri mkubwa wa milima, madini, ardhi nzuri, wanyama, mimea , bahari,  mito na maziwa, sasa kuna haja gani ya viongozi wetu kutumia msemo huu?  Bila shaka sihitaji kuuma maneno wala kupindisha ukweli wanatufanya  wajinga ili watawale mtaji kidogo faida kubwa!
     Tugeukie  upande wa pili wa sarafu tunaposema Mungu ibariki Tanzania tuna maana  gani? Nayo ni hoja iliyo wazi kuwa Mungu ametubariki watanzania kuliko  mataifa yote ulimwenguni ndio maana katupa madini ya Tanzanite ambayo  hayapo popote ulimwenguni isipokuwa Tanzania pekee, ni Mungu katupa  utajiri wa kila aina mito, mabonde, mabwawa, wanyama, misitu na bahari,  sasa kwa haya yote sidhani kama tupo sahihi kusema Mungu ibariki  Tanzania, aibariki kwa lipi tena? Vinginevyo nah ii kauli ni silaha ya  ki-idelogy inayolenga kutufanya wajinga ili tutawalike kirahisi,  tuikatae!
  Ikumbukwe  kuwa wakati mwingine Mungu anachukizwa na uzembe uzembe hivyo hofu  yangu ni kuwa kama tukijizoesha na upuuzi wa hizi kauli huku tukiogelea  kwenye dimbwi la utajiri kuna hatari tukamuudhi Mwenyezi Mungu kisha  akatuadhibu kwa maana haiingii akilini hata kidogo kwa nchi kama  Tanzania kuwa na wananchi maskini na imani hata huko mbinguni malaika  wanaomboleza na kulia jinsi watanzania tunavyolea umaskini wa kujitakia  kabisa.
  Tujiulize  swali rahisi tu kama kweli viongozi wetu wanadai nchi ni maskini wao  mbona matajiri? Au tuhoji basi watupe mbinu za kutajirika walizotumia,  nenda kamwone mwanakijiji wa kule Nyanjilinji Lindi  alivyochoka kwa maisha magumu kisha mfananishe na yule mtoto wa  kibosile pale Masaki anavyong’aa kwa maisha mazuri kisha ndio utabaini  kuwa tunafanywa wajinga na watawala wetu kila uchao, Naam! Kwa  watanzania ujinga sio leo tu bali ni kila siku!.....Tafakari!
 
 
  
 
 
 
 
 
No comments:
Post a Comment