Kalou akishangilia goli lake |
Chelsea wamefanikiwa kukwea hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ya Uingereza baada ya kuibuka na ushindi mnono wa bao 3-1 dhidi ya Birmingham huku Arsenal wakishuka hadi nafasi ya tatu baada ya kuambulia sare ya bao 3-3 dhidi ya wapinzani wao wa jadi Tottenham.
Katika pambano lililofanyika kule WHL, uwanja wa nyumbani wa Tottenham, mabao sita yalishuhudiwa, katika pambano ambalo lilijaa kila aina ya ushindani na burudani.
Kama ilivyotarajiwa, mechi hiyo ilianza kwa kasi kubwa na kunako dakika ya tano tu Arsenal wakachukua uongozi wa mechi baada ya bao maridadi la Theo Walcot, bao ambalo lilidumu kwa muda wa dakika mbili tu kwani dakika ya saba ya mchezo, Van der Vaart, aliwasawazishia wenyeji bao hilo.
Samir Nasri akazama nyavuni na kuwarejeshea Arsenal uongozi wa mechi hiyo kunako dakika ya 12, kisha Robin Van Persie akaongeza bao la tatu kunako dakika ya 40 na kushusha presha za mashabiki wa Arsenal ambao wakaamini kuwa huenda ukawa ni usiku wao wa kuikaribia Man United kileleni. Lakini furaha yao ikaanza kutumbukia nyongo kunako dakika ya 44 pale Huddlestone alipoisawazishia Spurs bao hilo na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa 2-3.
Kipindi cha pili ambacho kilishuhudia timu zote zikifanya mabadiliko kwa kutoa wachezaji kadhaa na nafasi zao kujazwa na wengine, kikawa na manufaa zaidi kwa wenyeji ambao walisawazisha goli la tatu kupitia kwa Van der Vaat kwa njia ya penalti kunako dakika ya 70, na matokeo kuwa 3-3 hadi mwisho wa mchezo.
Matokeo hayo yameifanya Arsenal kushindwa tena kuikaribia Man United ambao wana pointi 70 kileleni mwa ligi na mbaya zaidi yamewapa mwanya Chelsea kushika nafasi ya pili huku wenyewe Arsenal wakishuka hadi nafasi ya tatu. Timu zote zina pointi 64 baada ya kushuka dimbani mara 33, lakini Chelsea wana uwiano mzuri wa mabo ya kufungwa na kufunga.
Matajiri hao wa darajani, walifanikiwa kushika nafasi hiyo baada ya kuwatandika Birmingham kwa mabao 3-1 katika mechi nyingine iliyopigwa usiku huu ambapo mabao ya Chelsea yaliwekwa kimiani na Malouda aliyefunga mabao mawili katika dakika ya 3 na ya 62, huku jingine likiwekwa kimiani na Kalou kunako dakika ya 26 ya mchezo. Bao pekee la kufutia machozi kwa wageni lilifungwa na Larsson kunako dakika ya 76 kwa njia ya penalti.
Bonyeza hapa kujua jinsi ilivyokuwa katika mechi zote hizo hatua kwa hatua. au bonyeza hapa kujua kuhusu mechi ya Spurs na Arsenal, na hapa kwa mechi ya Chelsea na Birmingham.
No comments:
Post a Comment