WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), unateswa na siasa za makundi na kuutaka utumie muda wake mwingi sasa kutatua matatizo yake.
Juzi, Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa alisema umoja huo kupitia mkutano wake wa Baraza Kuu, umeazimia kwamba utahakikisha vigogo ambao wamekuwa wakizungumza nje ya utaratibu wa vikao vya CCM wanatupwa nje ya ulingo wa siasa za chama hicho tawala.
Hata hivyo, akizungumza kwa simu jana akiwa jimboni kwake, Urambo Mashariki, Sitta alisema: “Nadhani wao wenyewe wana matatizo ya kutosha. Sihitaji malumbano kwa sababu sijui shabaha yao lakini ninachoweza kusema ni kwamba wanateswa tu na siasa za makundi.”
Spika huyo wa Bunge la Tisa, ambaye amekuwa akipinga hadharani ulipaji Sh94 bilioni kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans, aliitaka UVCCM kurejea misingi iliyorithi kutoka Umoja wa Vijana
wa Tanu (TYL), huku akisisitiza kwamba kinachohitajika sasa si malumbano, bali ni watu kufuata misingi ya uongozi bora, jambo ambalo anaamini kuwa litawezesha hata umoja huo kuwa na vijana safi.
“Sasa tukianza kulumbana hapa tutakuwa tunadhihirisha siasa za makundi. Kwa sababu kuna kauli ambazo ukiziangalia unajua kabisa hizi zinatokana na kuteswa na siasa za makundi tu na hakuna jambo jingine lolote,” alisisitiza Sitta.
Alisema uhuru wa kutoa maoni ni mambo ambayo yametajwa ndani ya Katiba ya nchi hivyo, kinachohitajika ni kulinda misingi ya uadilifu ili kuondoa malumbano yanayotokana na msimamo wa kukemea maovu katika chama na Serikali. Sitta ni mwanasiasa wa pili kuzungumzia azimio hilo la UVCCM.
Juzi mara baada ya kutolewa kwa tamko hilo, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema anajiandaa kutoa msimamo wake kuhusu kauli hiyo ya UVCCM.
No comments:
Post a Comment