Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Sunday, March 13, 2011

Mume, mke wafa wakitoka kwa ‘Babu’

Mchungaji mstaafu, Ambilikile Mwaisapile (kulia) akitoa dawa kwa wagonjwa huko Loliondo mkoani,Arusha.

FURAHA ya kurejea nyumbani salama baada ya kupata tiba kutoka kwa Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile `Babu’, imegeuka kilio kwa baadhi ya familia, baada ya jana watu watano kufa katika ajali ya gari.
 

Miongoni mwa waliokufa ni madereva wa magari yaliyogongana, pia kwa upande wa abiria waliokufa ni pamoja na mume na mke waliokuwa wanarejea kwao Lushoto baada ya kuwa wameshakunywa dawa ya babu. 

Aidha, abiria wengine 14 wamejeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea eneo la Makuyuni, Arusha ikihusisha magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser, moja likitokea Loliondo kwenye tiba, na jingine likipeleka watu kwa ajili ya kupata huduma za Mchungaji Mwaisapile. 

Habari kutoka eneo la tukio zinasema kwamba, magari hayo yaligongana uso kwa uso na kupinduka, baada ya gari lenye namba za usajili T681 ABQ kuhama njia kutokana na mwendo kasi na kwenda kuligonga gari jingine lililokuwa likitokea Loliondo, wilayani Ngorongoro, T 606 ABU lililokuwa lililokuwa likiendeshwa na Zakayo ole Laizer (45). 

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Akili Mpwapwa alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kuwataja waliokufa kuwa ni pamoja na madereva wote, Laizer na Beatus Moris (36) ambaye gari lake ndilo lililosababisha ajali. 

Aliwataja wengine waliokufa kuwa ni pamoja na Raphael Kiboa (65) na mkewe ambaye hata hivyo jina lake halikuweza kufahamika. 

Mwingine aliyekufa ni Ismail Mohammed, mkazi wa Tabora. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Monduli na ile ya mkoa wa Arusha, Mount Meru wakati majeruhi walikuwa wanatibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli. 

Pamoja na kutokea kwa ajali hiyo, tiba za dawa ya asili inayosadikika kuwa inatibu Ukimwi na magonjwa mengine sugu inayotolewa na Mchungaji Mwaisapile imezidi kuwavutia watu wengi, wakiwamo vigogo na maofisa wa serikali huku mchungaji huyo akiitaka serikali izuie watu kwa muda kufika katika eneo hilo. 

Miongoni mwa watu ambao gazeti hili lilishuhudia juzi ni timu ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na viongozi wengine wa mashirika ya umma na taasisi nyingine za serikali. 

Tiba ya Mchungaji huyo ni ya magonjwa mengi lakini yeye anasisitiza kuwa magonjwa makuu ni Ukimwi, saratani, kisukari, pumu, kifafa na mengineyo. 

Viongozi wa serikali wa Wilaya ya Ngorongoro tangu wiki iliyopita wamekuwa wanapokea viongozi na maofisa wengi wa kiserikali wanaoenda kupata tiba katika kijiji hicho cha Samunge 
kilichoko kilometa takribani 70 kutoka Loliondo mjini. 

Lengo la kuwaona viongozi wa wilaya hiyo ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo ni kuepusha usumbufu ambao unaweza kuwapata kwa kukaa muda mrefu katika foleni kama ilivyo kwa watu wengine. 

Kwa kutambua hali hiyo Mchungaji huyo amekuwa anapelekew wageni hao wa kiserikali ili 
wapatiwe tiba hiyo bila kupanga foleni. Hivyo ndivyo ilivyokuwa jana baada ya maofisa hao wa Takukuru kufikishwa eneo hilo na mmoja wa viongozi wa wilaya na kuwatambulisha kwa tabibu huyo wa asili. 

Wakati maofisa wa serikali wakipata unafuu wa kutopanga foleni, watu wengine wameendelea kusota kwenye misururu ya foleni huku wakiwa ndani ya magari yao baada ya Mchungaji huyo kubadilisha utaratibu wa kutoa dawa. 

Katika utaratibu huo mpya, watu wanapatiwa dawa wakiwa kwenye gari lao ili kuepusha fujo ambazo awali zilikuwa zinafanywa na watu wanaopanga foleni kusubiri dawa hiyo. 

Utaratibu huo umesaidia watu wengi kupatiwa tiba hiyo kwa haki kwani hakuna gari linaloweza kuvuka na kwenda mbele ya gari lingine. 

Machi 12 watu waliopatiwa tiba ni wale ambao walifika eneo hilo siku ya Jumatatu na wamekaa katika eneo hilo kwa siku nne hadi tano hadi jana ilipofika zamu yao. 

Mmojawapo wa viongozi wa CCM ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini aliliambia gazeti hili kuwa yeye ana siku ya tatu na zamu yake haijafika. 

“Niko hapa siku ya tatu na gari letu liko huko nyuma.” Ili watu wengi watibiwe kwa wakati mfupi baadhi ya watu walioenda kupata tiba akiwemo kiongozi huyo wa CCM wamechukua jukumu la kumsaidia Babu kugawa dawa kwa watu walioko kwenye magari. 

“Tumelazimika kumsaidia babu ili foleni iende kwa kasi, wasaidizi wake tu hawatoshi,” alisema kiongozi huyo. 

Mchungaji huyo akizungumza jana nyumbani kwake alisema eneo hilo linazidi kufurika watu hivyo ni wajibu wa Serikali kuzuia magari yasiingie katika kijiji hicho ili kumpa fursa ya yeye kuwatibu na kuwapunguza watu waliojazana katika eneo lake. 

Alisema yeye hana uwezo wa kuwazuia kwenda kwani ushuhuda unaotolewa na watu ambao wamepona maradhi kama Ukimwi baada ya kutumia dawa hiyo ndio inaowavutia watu wengi kwenda kupata tiba hiyo kwake. 

“Mimi sina uwezo wa kuwazuia nitaendelea kutoa tiba kadiri ya uwezo wangu…ila Serikali ingeandaa utaratibu wa kuzuia magari yasizidi kuingia katika eneo hili kwa muda,” alisema Mwaisapile. 

Alisema watu wakikaa kwa siku zaidi ya moja katika eneo hilo wanachafua mazingira kwa kujisaidia ovyo kutokana na kutokuwepo vyoo eneo hilo huku wengine wakiishiwa fedha za matumizi kutokana na wafanyabiashara kutumia mwanya huo kuuza vitu kwa bei ghali. 

Kuhusu wasiwasi unaoneshwa na serikali kuwa maji anayotumia si salama, Mchungaji Mwaisapile alisema si kweli kwani maji yanayotumika ni ya bomba na yanatosha umati wa idadi yoyote ya watu, na dawa hiyo inachemshwa hivyo kuwa salama zaidi. 

Pia Mchungaji huyo aliwahakikishia wateja wake kuwa mgonjwa wa Ukimwi aliyekuwa anatumia dawa za kuongeza nguvu hana haja tena ya kuendelea kutumia dawa hizo iwapo atakunywa kikombe cha dawa yake. 

“Ninawaambia hawana haja ya kuendelea kutumia hizo dawa za kuongeza siku za kuishi, hili Mungu amenihakikishia kuwa wanapona kabisa,” alisema mchungaji huyo. 

Mwandishi alishuhudia msururu mrefu wa magari huku magari mengine yakiendelea kuingia kila dakika. Kufikia juzi, serikali iliripoti kuwapo kwa magari zaidi ya 800. 

Watu waliozungumza na gazeti hili walishauri kuboresha mazingira ya eneo hilo na si kupiga marufuku tiba hiyo. 

Wapo pia watu ambao walikuwa wanasumbuliwa na magonjwa ya kisukari ambao wameshuhudia mbele ya mwandishi kupona kabisa kwani walienda katika eneo hilo wakiwa hawajiwezi.

IMETOKA HABARI LEO

1 comment:

Goodman Manyanya Phiri said...

Ya sikitisha


Mungu awaweke pema peponi!