Afisa tawala na Mwanzilishi wa Shule za St. Marys Mkoa wa Mbeya, Anuciatha Ngonyani akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania (TAJATI). |
Wanafunzi wa darasa la Sita wakijifunza Kompyuta |
Afisa tawala akionesha maktaba ya vitabu shuleni hapo |
Baadhi ya Wanachama wa TAJATI wakiwa katika picha ya pamoja na Afisa tawala wa Shule za St. Marys Mbeya |
Mmoja wa Wanachama wa TAJATI, Joachim Nyambo akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi ya Afisa tawala wa Shule za St. Marys Mbeya, anayeshuhudia ni Naibu Katibu Mkuu wa TAJATI, Patrick Kossima. |
Mtunza hazina wa TAJATI, Brandy Nelson akimfuatilia kwa ukaribu mwanafunzi wa darasa la sita alipokuwa akitumia kompyuta. |
SERIKALI inapoelekea kutoa ada
elekezi kwa ajili ya shule binafsi imetakiwa kufanya utafiti kabla ili
kujiridhisha kulingana na gharama za uendeshaji wa baadhi ya shule kuwa kubwa
zinazoendana na huduma zake.
Rai hiyo ilitolewa jana na
Afisa tawala na mwanzilishi wa Shule za St. Marys mkoani Mbeya, Anuciatha
Ngonyani, alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kutoka Chama cha
Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania(TAJATI) waliofanya ziara
katika shule hizo zilizopo Forest jijini Mbeya.
Ngonyani alisema pamoja na
kwamba serikali imesema haitafanya haraka katika kutoa ada elekezi kwa shule
binafsi bado inapaswa kufanya utafiti
kwa kuzitembelea shule moja moja ili kujionea namna shule hizo zinavyoendeshwa
na gharama zinazotumika.
Akitolea mfano shule zake zenye
mikondo mitatu kuanzia Shule ya awali, Shule ya Msingi na Sekondari zenye
mchepuo wa kiingereza, Ngonyani alisema wanafunzi wa kutwa hupata huduma ya chakula mara mbili kwa
siku pamoja na usafiri wa kwenda na kurudi majumbani kwao hivyo kutumia gharama
kubwa kuendesha.
“Naiomba Serikali inapoendelea
na mchakato ije kutembelea shule zetu ili pindi watakapotoa ada elekezi
zisiumize shule zingine zikashindwa kujiendesha, binafsi sipingi kuwa na ada
elekezi lakini tumetofautiana kwenye uendeshaji mimi natoa chakula na usafiri
jambo ambalo shule zingine hazifanyi” alisema Ngonyani.
Alisema endapo kiwango cha ada
kitakuwa chini sana ni dhahiri baadhi ya shule zitayumba zikiwemo St. Marys
kwani watashindwa kutoa huduma nzuri kwa kununua chakula, kuwasafirisha
wanafunzi, kununua vitabu na vifaa vya kufundishia pamoja na kuwalipa walimu
wanaofundisha shule binafsi.
Aliongeza kuwa sambamba na kuwa
na ada elekezi pia Serikali iangalie namna itakavyoweza kupunguza mlundikano wa
kodi kwa shule binafsi jambo lililochangia kuwa na kiwango kikubwa cha ada ili
kuweza kufidia kodi ambazo mmiliki wa shule anapaswa kulipia.
“Pia tunaviwango vikubwa na
mlundikano wa kodi, hili ndo limechangia ada ziwe kubwa kwa baadhi ya
shule,mfano tu hapa nalipa ada ya taka kila baada ya miezi sita shilingi laki
tatu,kupima afya kila mfanyakazi elfu kumi, kodi ya majengo shlingi laki nne
kwa mwaka, zimamoto laki tano kwa mwaka na kodi ya SDL kwa malipo ya
wafanyakazi hivyo ukipiga hesabu ni hela nyingi tunatoa”alisema Ngonyani.
Aliongeza kuwa mbali na kodi
hizo pia anatumia fedha nyingi kulipia Ankara za maji na umeme ambapo kila
mwezi hulazimika kulipia zaidi ya shilingi Milioni tatu kwa matumizi ya maji na
umeme pekee bila mahitaji mengine.
Aidha aliongeza kuwa hivi sasa
anapata usumbufu kwa baadhi ya wazazi waliosikia kuwa kutakuwa na ada elekezi
jambo linalowafanya kutolipa kwa wakati na wengine kujipangia viwango kulingana
na taarifa za upotoshaji kutoka kwenye mitandao ya kijamii kwamba ada elekezi
tayari imeshatolewa.
No comments:
Post a Comment