Diwani wa Kata ya Isapulano Wilaya ya Makete Alphonce Mbilinyi akizungumza neno baada ya kupokea msaada wa fedha wa ajili ya ujenzi wa Choo cha Walimu katika Shule ya Msingi Ivilikinge. |
Afisa Mtendaji akipokea Msaada kutoka kwa kiongozi wa Mwapima Forum ndugu Tito Tweve |
Baadhi ya viongozi wa Mwapima forum wakikabidhi mfuko wa saruji kwa viongozi wa Kijiji na Kamati ya Shule ya Ivilikinge kwa ajili ya ujenzi wa Choo cha Walimu |
Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Ivilikinge, Ibrahim Fungo, akipokea kipande cha Malumalu kwa ajili ya kujengea Choo cha Walimu shuleni kwake |
Mwalimu Mkuu akipokea Peni kwa ajili ya matumizi ya walimu |
Baadhi ya viongozi wakikabidhiana vifaa mbali mbali kwa ajili ya ujenzi wa Choo cha Walimu |
Tito Tweve akizungumza na wananchi wa Ivilikinge kuhusu kuguswa na hatimaye kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi wa Choo cha Walimu |
Wanachama wa Mwapima forum wakiangalia mazingira ya Choo cha walimu wa Shule ya Msingi Ivilikinge ambacho kimechakaa na hakifai kwa matumizi ya binadamu |
Wanafunzi wakitoa burudani |
Mazingira na hali halisi ya Choo cha Walimu |
Choo cha Wanafunzi ni bora na cha kisasa tofauti na choo cha Walimu |
VIJANA nchini wameshauriwa kuwa na
utamaduni wa kukumbuka asili yao kwa kurudi kushiriki katika shughuli za
maendeleo katika maeneo waliyotoka badala ya kuwaachia wazazi pekee licha ya
umri wao kuwa mkubwa.
Wito huo ulitolewa na Baadhi ya
Vijana waishio nje ya Kijiji cha Ivilikinge Kata ya Isapulano Wilaya ya Makete
mkoani Njombe waliounda umoja wao unaojulikana kwa jina la Mwapima Forum wakati
wa hafla ya kukabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi wa vyoo vya walimu katika
Shule ya Msingi Ivilikinge.
Akisoma taarifa kwa niaba ya
wenzake, Mratibu wa Mwapima Forum, Award Mpandila alisema umekuwa utamaduni kwa
vijana kutoka katika maeneo waliyozaliwa na kukulia na kuelekea sehemu nyingine
kutafuta maisha lakini pindi wanapofanikiwa hujisahau na kushindwa kurudi
kuchangia shughuli za maendeleo.
Alisema kutokana na hali hiyo baadhi
ya Vijana wapatao 60 waliosoma shule ya Msingi Ivilikinge kutoka maeneo mbali
mbali ya Ndani na Nje ya Nchi walijikusanya kupitia mitandao ya kijamii kwa
lengo la kufahamiana na kupeana taarifa za kijijini kwao kuona kama kuna
changamoto ambazo wanaweza kusaidia kuzitatua.
Mpandila alisema umoja huo ambao
ulianzishwa Disemba 21, mwaka jana baadhi ya wanachama wake walibaini kuwepo
kwa Changamoto ya Choo cha Walimu katika Shule hiyo huku Wanafunzi wakitumia
vyoo vya kisasa vilivyojengwa kwa msaada wa watu wa Marekani(USAID).
Alisema umoja huo uliamua
kuchangishana ili kutatua tatizo la Choo kwani Walimu walikuwa wakitumia Choo
kilichochakaa na wakati mwingine walilazimika kufuata huduma hiyo majumbani
mwao.
Alisema katika makusanyo hayo zaidi
ya shilingi Milioni 1,763,700 zilikusanywa ambazo zitaweza kumudu gharama za
ujenzi wa Choo kimoja chenye matundu mawili hadi kukamilika kutokana na
mahitaji muhimu kununuliwa na kukabidhi kwa serikali ya Kijiji na Kamati ya
Shule kwa ajili ya usimamizi.
Akisoma risala ya Shule katika hafla
hiyo, Mwalimu Atuwene Fungo alisema Walimu walikuwa wakitumia kwa hofu kubwa
choo chao kutokana na kuchakaa kwani kilijengwa muda mrefu bila kuwa na
miundombinu ya kudumu ambapo kilijengwa Mwaka 1976 wakati shule hiyo
ikianzishwa.
Alisema msaada uliotolewa na vijana
hao utasaidia Walimu kuokoa muda wa kufuata huduma ya choo mbali na mazingira
ya shule hivyo itarahisha wao katika ufundishaji kutokana na mwalimu kuwepo
muda wa kutosha katika mazingira ya shule.
Alisema changamoto zingine ni
upungufu wa Walimu, uchakavu wa miundombinu, madawati, upungufu wa Walimu na
vifaa vya kufundishia jambo ambalo Vijana waishio nje ya Kijiji hicho waliahidi
kutatua baadhi kama Madawati na vifaa vya kufundishia pamoja na ujenziwa
madarasa mapya.
Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya
Isapulano ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Alphonce Mbilinyi,
licha ya kuwapongeza vijana hao kwa juhudi walizoonesha za kukumbuka nyumbani
kwao kwa kuwasaidia walimu aliahidi kusimamia ujenzi wa Choo hicho na
kuhakikisha kinakamilika ndani ya siku kumi na nne.
“Sina maneno mengi ya kuongea
nimeguswa na jambo la hawa vijana nawapongeza sana ni mfano wa kuigwa na watu
wengine mkumbuke kuja kutusaidia wazee wenu, nawaahidi ujenzi wa hiki choo
utaanza haraka sana na ndani ya wiki mbili utakuwa umekamilika, Hapa kazi tu”
alisema Diwani Mbilinyi.
Nao baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha
Ivilikinge, Emelite Sanga,Luthi Msigwa,Ezron Tweve na Cosmas Luvanda walisema
wanafarijika kuona watoto wao wanakumbuka nyumbani na kusaidia shughuli za
maendeleo leo kwa jambo hilo litawapunguzia mlundikano wa michango mbali mbali
katika Kijiji chao.
No comments:
Post a Comment