Kwa muda sasa kumekuwapo na tuhuma zinazohusu
"wizi" wa fedha za akaunti ya escrow iliyofunguliwa katika Benki Kuu
ya Tanzania mwaka 2006. Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha
zilizokuwa zikilipwa na Shirika la Umeme Tanzania {TANESCO} kwa kampuni ya
kufua umeme ya IPTL. Chimbuko la akaunti hiyo ni mgogoro wa tozo hiyo kwamba
iligubikwa na utata baada ya kudaiwa kwamba Tanesco ilikuwa ikitozwa fedha
nyingi kuliko inavyostahili.
Tuhuma
za huo "wizi" hata hivyo hazikuishia tu kwa wahusika wakuu yaani
makampuni ya umeme, bali zimetiririshwa hadi kwa watu binafsi ambao kimsingi
hawana uhusiano wowote na mgogoro huo wa malipo na wala kuhusika kwa njia
yoyote na hicho kinachodaiwa kwamba ni uporaji wa fedha za akaunti hiyo ya
Escrow.
Akaunti Escrow ni akaunti ya amana ambayo
inawekwa chini ya uangalizi wa mtu wa tatu ili huyo mwangalizi aikabidhi kwa
mlengwa pale tu masharti kadhaa yatakapokuwa yamekamilishwa. Hivyo basi akaunti
hiyo maalum ya amana ilifunguliwa na kuwekwa chini ya Benki Kuu kama wakala
anayesubiria kutekelezwa kwa masharti maalumu ili aikabidhi kwa wenye kumiliki
fedha hizo watakapomaliza tofauti zao.
Ni
vizuri kuliangalia suala hili la akaunti maalum ya amana kwa namna ambayo
itawafanya wale wenye kiu ya kutaka kujua ukweli kukidhi hamu yao.
Fedha iliyokuwa ikiwekwa katika akaunti hiyo ni
tozo ya uwezo wa mitambo ya kufua umeme ambayo kampuni ya IPTL ilikuwa ikiitoza
Tanesco. Baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Utatuzi wa Migogoro ya Uwekezaji
(ICSID) kupunguza tozo ya IPTL kutoka USD 3.6million kila mwezi mpaka USD
2.6million kila mwezi baadaye TANESCO ilishauriwa vibaya na wanasheria kwamba
tozo hiyo bado ni kubwa kuliko mkataba baina ya IPTL na TANESCO Mei 26, 1995
unavyo eleza.
Ubishani
uliozuka kati ya mtoa huduma ya umeme yaani IPTL na mtumia huduma ya umeme
yaani Tanesco ndio uliosababisha kufunguliwa kwa akaunti hiyo maalum ya amana
yaani escrow account katika Benki Kuu ya Tanzania {BoT} kama njia salama ya
kutunza fedha hizo hadi mgogoro utakapokuwa umetatuliwa.
Ni muhimu kufanya hivyo ili kuhakikisha kwamba
mtoa huduma yaani IPTL hasitishi kufua umeme na mtumiaji wa umeme yaani Tanesco
naye hakosi umeme wa kuuza kwa walaji wake. Hiyo ni busara ya kibiashara. Fedha
hizo zililipwa katika akaunti hiyo maalum kutokana na hati za madai au ankara
kutoka kwa mtoa huduma na si vinginevyo.
Kitu kimoja kilichojitokeza wazi ni kwamba suala
la akaunti hiyo maalum limekuwa likibeba sura mpya kila kukicha na la
kusikitisha zaidi ni kwamba vyombo vya habari vilivyo vingi ama vimekuwa
vikipotosha kwa makusudi au kwa kutokuelewa mada yenyewe ipasavyo. Vipo vyombo
vya habari kwa mfano ambavyo vimedai kwamba "Benki ya Standard Chartered
ndiyo mmiliki wa mitambo ya IPTL baada ya kupewa mamlaka hayo na mahakama -
Deed of Assignment- inayoiruhusu kuchukua na kumiliki mali za IPTL kutokana na
kushindwa kulipa mkopo.
Aidha kwa mujibu wa gazeti la Mawio la Alhamisi
Novemba 20-26, 2014 mkataba huo uliipatia benki ya SCB haki za IPTL ndani ya
mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na kumiliki mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Mawio Benki ya
Standard Chartered inaidai Tanesco dola za Marekani 258.7 milioni kama deni
linalotokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na dola za Marekani 138 milioni
zinazotokana na mkopo pamoja na riba. Kwa mujibu wa uchambuzi wa Mawio madai
hayo ni halali kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa gazeti hilo "nyaraka za
serikali zinaonesha kuwa PAP iliamuriwa kulipa wadai wote wa IPTL lakini
haikuilipa Benki ya Standard Charted ambayo inajitangaza kuwa ni moja ya wadai.
Ni
vyema na busara kuanza uchambuzi huu kwa kufanya nukuu hiyo muhimu sana kutoka
katika gazeti la kila wiki la Mawio kwa sababu inatusaidia kuonyesha waziwazi
kwamba hiki kinachodaiwa kwamba ni kashfa ya fedha za Escrow kina sura nyingi
sana kulingana na maslahi yanayolengwa kutetewa.
Katika muktadha huu ni wazi kwamba anayetetewa
hapa ni Benki ya Standard Chartered ambayo inadaiwa kwamba ndiyo yenye haki ya
kulipwa fedha kutoka katika akaunti ya Escrow na kwa mantiki hiyo imeishitaki
Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Uingereza.
Deni linalodaiwa kwamba Tanesco inadaiwa na
Standard Chartered la dola za Marekani linatokana na gharama za umeme
uliozalishwa na IPTL na nyingine ni mkopo na riba. Inashangaza kwamba Tanesco
inawezaje kudaiwa na Benki ya Standard Chartered wakati aliyezalisha umeme ni
IPTL? Abrakadabra hiyo ndiyo inayomfanya ye yote yule mwenye akili timamu
kutambua kwamba kuna mchezo wa kiini macho unaochezwa na benki hiyo dhidi ya
Tanzania.
Ni wazi kabisa kwamba benki hiyo inalazimisha
kuwapo na mgogoro wa kuhusu akaunti ya Escrow kwa lengo moja tu nalo ni
kuhakikisha kwamba wanapata nafasi ya kukwapua hizo fedha wanazodai kwamba sio
halali kuchukuliwa na IPTL. Kwamba zikichukuliwa na Benki ya Standard Chartered
ambayo haijazalisha umeme wala kuwa na ushahidi wowote wa kushiriki katika
kuzalisha umeme ni halali kabisa na zikichukuliwa na IPTL ambayo imezalisha
umeme na inayo mikataba ya kuuziana umeme na Tanesco si sahihi, ni wizi, ni
ujambazi ni hila na kashfa. Hii inahitaji maelezo zaidi kushinda haya
yanayotolewa hivi sasa.
Ukweli wa mambo ni kwamba mazungumzo kuhusu fedha
za Escrow na hususan habari za kujaribu kuonyesha kwamba umiliki wake ni batili
una lengo moja tu nalo ni kuandaa mazingira kwa ajili ya Benki ya Standard
Chartered hatimaye kuzichukua fedha hizo kwa kutumia kigezo cha kwamba
imemilikishwa mitambo ya IPTL na kwamba ndiyo iliyokuwa na haki ya kulipwa tozo
ya uzalishaji umeme na si kampuni nyingine yoyote. Hivyo ndivyo kampuni hiyo
inavyodai katika kesi iliyofungua dhidi ya Serikali ya Tanzania huko Uingereza.
Benki
ya Standard Chartered inatumia mbinu mbalimbali ili kuhakikisha inafikia lengo
lake la kukwapua fedha za kigeni si chini ya dola milioni 200 kutoka kwa
serikali ya Tanzania. Moja ya njia inayotumia ni propaganda ambayo hupenyezwa
katika vyombo vya habari kwa kutumia majukwaa mbalimbali.
Moja ya njia zinazotumika ni kujaribu kuufanya
umma uamini kwamba fedha zilizotoka katika ufungaji wa akaunti hiyo ya Escrow
zimeibwa na kwamba wahusika katika huo wizi ni pamoja na viongozi kadhaa wa Serikali.
Kinachosikitisha zaidi ni kwamba kuhusishwa kwa
watu hao kunafanyika bila hata ya kuwataka wajieleze kama wanaelewa kile
wanachotuhumiwa nacho. Wafadhili wa propaganda hizo hawakubali kujitokeza
hadharani moja kwa moja kwa kuhofia kuumbuliwa. Matukio huchukuliwa si kwa
ujumla wake bali upande mmoja na kuyatangaza kwa namna ya kukidhi matakwa na
matarajio yao tu.
Tumezoea kuambiwa kwamba wakati suala linapokuwa
mahakamani kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi basi si sahihi kuendelea kulijadili
kwenye vyombo vya habari kwani kwa kufanya hivyo ni sawa kabisa na kuingilia
uhuru wa mahakama. Ni wazi kwamba hata suala linapokuwa katika uchunguzi au
upelelezi uwe kwa kutumia tume maalum au makachero basi ni muhali kulizungumzia
hadharani na kuwatuhumu na hata kuwahukumu watu kwa ujasiri usio na kikomo
kwamba ni wezi au mafisadi au wakumbatiaji wa madhila hayo yote. Hili
linafanyika kila siku kupitia vyombo vya habari na chimbuko lake ni baadhi ya
wabunge na wanasiasa ambao hufanya hivyo huku wakitumia kila aina ya takwimu za
kweli na za kughushi au kubuni tu kichwani.
Nini
kinachowafanya au kuwapa jeuri hawa watu wanaowatuhumu na kuwahukumu wengine
bila ya kujali kwamba hilo halitakiwi wala kupaswa kufanyika bila ya kupitia
katika vyombo vya sheria ili kutoka fursa kwa wengine kujitetea? Swali hilo
linastahili kujibiwa kwa umakini mkubwa ili kubaini kama kweli hao wanaodai
kwamba wanapigania haki ya kiuchumi ya Watanzania ni kweli wanafanya hivyo kwa
dhati ya moyo wao kabisa bila ya kuwa na nia nyingine iliyojificha ambayo
hawathubutu kuiweka hadharani kwani kwa kufanya hivyo watageuka viroja.
Pamoja na kwamba kuna kesi mahakamani dhidi ya
Serikali ya Tanzania ni wazi kwamba ukiwauliza Standard Chartered
kilichowapeleka mahakamani wanasema kwamba wanaionea nchi yetu huruma, Hata
hivyo, kamwe hakuna atayekuambia kwamba amekuja hapa kwa ajili ya kujaribu
bahati yake kama wanaweza kufanya mbinu wakatengeneza fedha ya bure. Ili
kufanikisha malengo yao tuhuma hurushwa kwa yeyote na popote. Ili kufanikisha
malengo hayo mtu yeyote yule aweza kuunganishwa katika lolote lile ili kufikia
lengo.
Ni
kwa utaratibu huo huo ndio tunashuhudia jinsi jitihada za Profesa Anna
Tibaijuka za kuendeleza mtoto wa kike kielimu zinavyopakwa matope na kukejeliwa
mno kwa sababu tu ameomba msaada mahali na akaupata.
Tujiulize
inakuwaje wanasiasa wetu wanathubutu kumhukumu Profesa Tibaijuka na kumuita
kila aina ya majina machafu. Ametuhumiwa kwamba ni mwizi eti kwa sababu aliomba
msaada kwa ajili ya shule ya Babro Johansson ambayo ni kwa madhumuni ya
kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu.
Profesa Tibaijuka aliomba msaada kwa barua rasmi
miaka kadhaa iliyopita na kampuni hiyo haikuweza kumsaidia mapema kutokana na
ukata na ni hivi majuzi hali ilipokuwa njema ndipo ikatoa msaada huo.
La kustaajabisha ni kwamba msaada huo haukuwa ni
siri na ulitolewa kwa uwazi mkubwa bila ya kificho. Sasa huo ujambazi wa
Profesa Tibaijuka umetokea wapi? Kosa lake ni kupatiwa fedha alizoomba kwa
ajili ya kuisaidia shule ambayo aliianzisha?
Tunajiuliza hapa, baada ya
VIP kuuza hisa zake kwa PAP na kulipwa na PAP stahili yake, ilifanya kosa gani
kutoa msaada kwa shule ya Babro Johansson?
Mahitaji na umuhimu wa elimu yanajulikana.
Viongozi wanahimiza kila leo umuhimu wa Watanzania kubadilika kuchangia
Maendeleo ya Elimu badala ya harusi na sherehe nyinginezo. Leo hii anatokea
Mtanzania anaomba msaada wa kuendeleza elimu na anapatikana Mtanzania anakubali
kuchangia vizuri maendeleo ya elimu, wawili hawa baadhi ya wanaojiita viongozi
wa siasa tena wenye kutaka kuchukua madaraka ya juu kuiongoza nchi,
wanalalamika na hata kutamani kutoa roho ya mtu! Watanzania tuzipime dhamira
zao. Ni wadanganyifu wasio na uelewa halisi wa matatizo na vipaumbele vya taifa
na hivyo kukosa dhamira thabiti ya kuyashughulikia. Wanasukumwa zaidi na tamaa
zao binafsi.
Kwa
wanaong'ang'ania kudai damu za baadhi ya watu kutokana na hukumu ambayo wao
wameipitisha baada ya kufanya kila kitu wao ikiwa ni pamoja na kutuhumu,
kupeleleza, kufungua mashitaka, kusikiliza kesi na hatimaye kuhukumu na sasa
kutaka kukaza hukumu kwa njia yoyote ile hakuna jambo zuri na jema kama kufanya
kile wanachotaka wao yaani kukubali kwamba fedha zote katika akaunti maalum ya
escrow ni za serikali na kwamba lazima zirudi serikalini.
Hata hivyo, wakubwa hao hawataki kurudi nyuma na
kujiuliza ni kwa njia gani fedha hizo zimeingia katika akaunti hiyo. Aidha,
hawataki kujiuliza kwamba kama Tanesco ndio ilikuwa ikitumbukiza fedha katika
akaunti hiyo, ilikuwa ikifanya hivyo kwa kutumia vigezo gani. Swali linguine la
kujiuliza, je Serikali hutunza pesa zake kwenye Account zake Benki Kuu au
kwenye Escrow Account?
Hawaoni
mantiki ya kutulia na kujibu swali la msingi kwamba kama Tanesco ingelikuwa
inatumbukiza fedha katika akaunti hiyo kwa ajili ya kugharamia tozo la uwezo wa mitambo kuzalisha umeme sasa
inakuwaje fedha hizo zirudi tena Tanesco? Ni maswali ambayo wanaojiamini kwamba
ukweli wanao wao tu hawataki kuyajibu hata kidogo kwani kwa kufanya hivyo
watakuwa wanaumaliza utamu wa mchezo wao wa kuigiza.
Fedha hizo zinatakiwa zirudi Tanesco ili Benki ya
Standard Chartered izichukue kwa madai kwamba ndiye mmiliki halali wa IPTL na
kwamba kuna deni kama ilivyoainishwa awali katika makala haya.
Kutokana na ufafanuzi huo hapo juu ni wazi basi
kwamba Tanesco ilikuwa ikilipia gharama za huduma ambayo ilikuwa inaipata
kutoka kwa IPTL. Hilo halina ubishi.
Lakini pia suala lingine ambalo sasa halina
ubishi japo halisemwi makusudi kwa sababu za upotoshaji ni kwamba katika
makampuni yote ambayo yanauzia umeme TANESCO, IPTL ndiyo kampuni pekee
inayotoza kiwango kidogo cha malipo ya uwekezaji (capacity charges). Suala la kujiuliza
hapa ni inawezekanaje IPTL ambayo inatoza kiwango kidogo cha capacity charges
ionekane “kuiibia” Serikali kwa kulipwa halali yake wakati makampuni mengine
yanatoza capacity charges kwa kiwango cha juu zaidi ya IPTL na hakuna
malalamiko.
Swali la kujiuliza ni kwamba ni kitu gani kinachowasukuma watuhumu
kutafuta kila njia ya kuonyesha kwamba kuna hitilafu kubwa sana kwa namna
ambavyo suala la akaunti hiyo lilivyohitimishwa?
Ukifuatilia
kwa karibu na umakini jinsi ambavyo tuhuma zimekuwa zikitolewa ni kwamba
kinacholengwa ni fedha zilizokuwa katika akaunti maalumu ambazo ni tozo ya
uwezo wa ufuaji wa umeme. Fedha hizo zinagombewa na Benki ya Standard Chartered
ambayo ina matawi yake hapa nchini.
Benki hiyo inatumia kila njia kujaribu kuonesha
kwamba fedha zilizokuwapo katika akaunti ya Escrow ni fedha ya Serikali. Kwa
mantiki hiyo inachojaribu kufanya Benki hiyo ni kuonyesha kwamba fedha akaunti
ya escrow si kwa ajili ya kulipia gharama za uwezo wa mitambo kufua umeme la
hasha. Bali ni fedha za Tanesco na kamwe hakuna anayestahili kuzipunguza kwa
njia yoyote ile.
Cha kushangaza, hata hivyo, ni kwamba benki hiyo,
inayodai kuwa iliikopesha fedha IPTL, katika madai yake yaliyopo mahakamani,
inadai kuwa yenyewe ndiyo ilistahili kupata fedha zilizokuwa kwenye escrow
account! Swali hapa ni je, hiyo asasi ndiyo Serikali? Je, fedha zilizokuwa
kwenye escrow account zinakuwa za Serikali na siyo IPTL kwa sababu benki hiyo
haijalipwa?
Jitihada za kutaka kuhalalisha kwamba fedha hizo
ni mali ya Tanesco na kwamba haziwezi kumegwa hata kidogo zinafanywa na Benki
ya Standard Chartered ambayo inataka kutengeneza mazingira ya kuchota fedha
kutoka Tanesco kwa madai kwamba ndiyo inayostahili kuwa mlipwaji wa fedha hizo
kutokana na deni ambalo kwa mujibu wa madai yao ndio walioikopesha IPTL fedha
kwa ajili ya mradi huo wa umeme.
Mchezo ambao benki hiyo inafanya hapa nchini ni
kuhakikisha kwamba vyombo vya habari vinaandika habari za kuigonganisha
serikali na wananchi kwamba Serikali ni ya mafisadi na inayokumbatia ufisadi,
na haina ubavu wowote wa kupambana na rushwa. Aidha, asasi hiyo imevirubuni
baadhi ya vyombo vya habari kuandika habari kwamba Mahakama za Tanzania
haziaminiki na zinakumbatia ufisadi na kwamba zimekubuhu kwa rushwa.
Cha kushangaza, tuhuma hizi za rushwa kwa
Mahakama za Tanzania zinakuja muda mfupi tu baada ya benki ya Standard
Chartered kuiambia mahakama New York, nchini Marekani iliposhitakiwa na VIP
kuwa Mahakama za Tanzania ndizo zenye uwezo wa kusikiliza na kutatua migogoro
ya IPTL.
Mchezo ambao Standard Chartered Bank inaufanya ni
kutumia vyombo vya habari kutoa habari zisizo za kweli na za upotoshi ili
kuwachochea watu dhidi ya Serikali yao kutokana na nini kinaendelea ndani ya
IPTL. Mambo mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusiana na Mahakama na
watendaji wa Serikali kula rushwa. Madhumuni ya kufanya hivyo ni kutaka
kuonyesha kwamba nchini Tanzania haki haiwezi kutendeka.
Madai hayo yote, yanatokea wakati Standard
Chartered Bank imefungua kesi London, kwa kisingizio kwamba Mahakama za
Tanzania haziwezi kutenda haki
Kwa vipi Standard Chartered Bank inatoa madai
kulipwa dola za kimarekani 208 milioni kutoka TANESCO (katika kesi
ilivyofunguliwa Mahakama ya usuluhishi (ICSID)) kwa mkopo wa dola milioni 84
kwa IPTL, wakati Serikali ya Tanzania na TANESCO tayari walikwishalipa
takribani dola 200 milioni kwa IPTL kufikia mwaka 2006. Kiasi hicho
kingelitosha kulipia mkopo uliokuwa umechukuliwa na kulipa gawiwo kwa VIP na
MECHMAR. Mpaka mwaka 2013 VIP ilikuwa haijalipwa hata senti moja kwa jina
lolote.
Kampuni ya Mechmar ilitumia fedha zilizodaiwa na
IPTL kutoka Serikali ya Tanzania na TANESCO kwa kujilipa yenyewe na Kampuni ya
Wartsila madeni hewa (kwa makubaliano na benki ya Danaharta na baadaye Standard
Chartered Bank (Hong Kong) Ltd.
Standard Chartered Bank (Hong Kong) Ltd inajaribu
kutekeleza mpango haramu dhidi ya IPTL kwa kutumia dhamana ya Serikali ya
Tanzania na hivyo Serikali ina sababu za kutaka Standard Chartered Bank
ithibitishe kama inaidai IPTL.
Mpaka sasa ukweli ni kwamba Standard Chartered Bank imekwepa kutoa ushahidi
kuwa ina madai yoyote dhidi ya IPTL na kwa sababu hiyo na zingine VIP na
IPTL/PAP wameifungulia kesi za madai ya fidia na hasara ya TZS 787bilioni na
USD 3bilioni katika Mahakama Kuu ya Tanzania. (Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com)
1 comment:
Kwa jinsi hii.tanzania itakua masikini miaka 1000.
Post a Comment