Wananchi wa
kijiji cha Totowe Kata ya Totowe wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya wameulaumu
uongozi wa kijiji kwa kutofanya mikutano ya kijiji kwa mwaka mzima hivyo kuamua
kuivunja serikali yote ya kijiji kutokana na kuzorotesha maendeleo ya kijiji
kutokana na ubadhilifu wa zaidi ya shilingi milioni thelathini na sita.
Hayo
yamebainishwa na wananchi hao katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini
hapo ambao ulihudhuriwa na mtendaji Kata Ronward Mwashiuya ambapo Mwenyekiti wa
Kijiji Gido Namwene na serikali yake wanashutumiwa kwa kutofanya vikao na hivyo
kusababisha ufujaji wa fedha za kijiji.
Baadhi ya
miradi inayolalamikiwa ni pamoja na uuzwaji wa tofali 26000 za ujenzi wa nyumba za walimu shule ya msingi Totowe
tofali ambazo zimetoweka katika mazingira ya kutatanisha hivyo kudhoofisha
juhudi za wananchi.
Mbali ya
tuhuma hiyo pia Mtendaji wa kijiji hicho Caristo Mwamanda ambaye ameondolewa
kutokana na ubadhilifu wa shilingi laki moja ambapo Mwenyekiti Gido baada ya
kubanwa alikabidhi jumla ya shilingi laki moja ambazo mtendaji alizitafuna bila
ridhaa ya wananchi.
Hata hivyo
baada ya tuhuma hizo Mtendaji Mwamanda alitimuliwa kijijini hapo na kuhamishiwa
kijiji cha Ifuko na kuletwa Mtendaji mwingine Adamson Mwaitege ambaye ameanza
utaratibu wa kusoma mapato na matumizi mwaka huu.
Aidha
wananchi wamelalamikia kamati mbalimbali za kijiji hicho ikiwemo kamati ya
huduma za jamii ambapo kamati hiyo inatuhumiwa kuuza viwanja kiholela na baadhi
ya viwanja kumilikiwa na viongozi wa kamati ya huduma ya jamii.
Mtendaji
Kata ameonya utaratibu wa ugawaji viwanja haukufuatwa na isipozingatiwa
kutatokea mgogoro mkubwa wa ardhi na kutotolewa stakakabadhi za serikali na
amezitaka kila kamati kuwa na kitabu cha kukusanyia mapato ili kutunza
kumbukumbu sahihi za fedha za serikali.
Mkutano huo
ulishindwa kuafikiana na kamati zote ikiwa ni pamoja na makusanyo ya fedha za
adhabu mbalimbali kama kuzagaa kwa mifugo ambapo fedha za tozo zimekuwa
zikiishia mikononi mwa wachache na waliotozwa wamekuwa hawapewi stakabadhi na
kufanya kijiji kukosa mapato.
Waliotimuliwa
ni pamoja na Mwenyekiti Gido Namwene,Mtunza hazina Benard Kihinda na wajumbe
Charles Jampani,Erasto Darweshi,Oliva Kasekwa,Michael Patrick,Simon Erick na
Doctor Yalinga.
Wengine ni
pamoja na Charles Mnyuzi,Juma Lwamba,Jacob Lupila,Bosco Mnyuzi,Maria Soda na
George Mnyuzi.
Katika
serikali hiyo imebakiwa na Mtendaji wa Kijiji Adamson Mwaitege ambaye wakati wa
matukio hayo yeye alikuwa hajahamia kijijini hapo hivyo hakuguswa na tuhuma
hizo mkutano uliridhia yeye ndiye afanye shughuli za Mwenyekiti katika kipindi
cha mpito.
Mtendaji
Kata Ronward Mwashiuya amesema utaratibu uliotumika katika mkutano huo wa
kuiondoa serikali ya kijiji umekiukwa kutokana na hesabu hizo kutokaguliwa na
mamlaka husika na kama mamlaka hiyo baada ya ukaguzi kama ikibaini ndiyo yenye
dhamana ya kuwafikisha watuhumiwa kwenye vyombo vya sheria.
Mkutano
ulimalizika kwa amani kutokana na hekima za mtendaji Kata kuwaomba wananchi
kupunguza jazba hadi hapo suala lao litakapopatiwa ufumbuzi na ngazi za juu.
Na Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment