MKUU wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela,
amewataka Maafisa na Askari wa Vyombo vya Ulinzi na usalama Mkoa wa Mbeya
kutotumiwa na Wafanyabiashara wakubwa katika kuhujumu duka la bidhaa zenye bei
nafuu(Duty Free Shop) lililozinduliwa hivi karibuni katika Gereza la Ruanda
Mkoani hapa.
Meela alitoa rai hiyo jana wakati
akizungumza na Mbeya yetu Blog mara baada ya kukamilika kwa uzinduzi wa duka hilo
uliofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak
Abdulwakil,ambapo alisema askari wanaweza kuingia tama ya fedha kwa kuwanunulia
bidhaa wafanyabiashara.
Alisema bidhaa zinazouzwa dukani hapo ni
mpango wa Serikali kuhakikisha watumishi wake wanakuwa na maisha mazuri kwa
kuwafungulia miradi itakayowanufaisha lakini baadhi yao wanaweza kuingia tamaa
na kutumika kwa wafanyabiashara wakubwa watakaotaka bidhaa kutoka dukani hapo
na kuziuza mitaani.
Alisema kufanya hivyo kutakuwa ni
kukiuka sheria na utaratibu wa utumishi wa umma ambapo Serikali kupitia Wizara
ya Mambo ya ndani kwa kufungua maduka kama hayo katika Gereza la Ruanda
lililofunguliwa jana Mkoani Mbeya, Ukonga-Dar Es Salaam,Isanga- Dodoma,Karanga-
Kilimanjaro, Chuo KPF-Morogoro na Butimba- Mwanza.
Kwa upande wake Kamishina wa Magereza
Nchini, John Minja, alisema ni ahadi yake kuhakikisha kabla hajaondoka madarakani
atahakikisha anafungua maduka kama hayo katika kila Mkoa kwa lengo la
kutengeneza maisha ya askari wake.
Alisema baada ya kuzindua duka katika
Gereza la Ruanda Mbeya watahamia kanda ya Kusini hususani Mikoa ya Mtwara
na Lindi ambako jitihada za kufungua maduka yenye bidhaa za gharama nafuu
zitaanza katika kipindi kifupi kijacho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment