Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akihutubia wananchi wa kijiji cha Ntandabala kata ya Masoko Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wakati wa hafla ya kugawa Hati Miliki kwa wakulima wa Chai iliyofanyika katika viwanja vya Tarafa ya Pakati. |
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya AbbaS Kandoro akiwa na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Rungwe wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Crispin Meela wakati wa hafla ya kugawa Hati Miliki kwa wakulima wa Chai iliyofanyika katika viwanja vya Tarafa ya Pakati. |
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akimkabidhi mwananchi wa kijiji cha Ntandabala kata ya Masoko Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wakati wa hafla ya kugawa Hati Miliki kwa wakulima wa Chai iliyofanyika katika viwanja vya Tarafa ya Pakati.
Ngoma za asili ya Wanyakyusa zikitoa burudani uwanjani hapo
MKUU wa Mkoa wa Mbeya Abbas
Kandoro ameziagiza Halmashauri za Wilaya kutengeneza mipango mizuri ya matumizi
bora ya Ardhi vijijini ili kuepusha
migogoro ya mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya
kusaidia zoezi la upimaji.
Hayo aliyasema juzi katika
hafla ya kugawa Hati ya Haki miliki za Ardhi za kimila kwa wakulima wa Chai
iliyofanyika katika viwanja vya makao makuu ya Tarafa ya Pakati iliyopo katika Kijiji cha Ntandabala kata ya Masoko
Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Kandoro alisema ili kuepusha
migogoro inayotokana na ardhi ni vema Halmashauri ikatengeneza mpango wa
matumizi bora ya ardhi kama kutenga eneo lawazi, shule, zahanati na maeneo ya
kupitisha miundombinu mapema kabla ya kuanza kuwagawia wananchi.
Aidha amewasihi Wakulima
kuhakikisha wanazitunza vizuri Hati miliki walizopewa kwa kuogopa kutapeliwa na
watu wengine ambao wanaweza kuwanyang’anya hadi mashamba yao na wao kuishia
kuwa maskini kutokana na kutokuwa na haki na ardhi yake.
“ Hakikisheni mnazitunza vizuri
kuepuka matapeli, pia chukueni Hati hiyo kama kielelezo kinachokuhakikishia
kuwa wewe ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo popote utakapokuwepo pia yatunzeni
na kuyaendeleza maeneo hayo” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aliongeza kuwa Hati Miliki pia
husaidia kuepusha migogoro ya mirathi na kunyanyaswa kwa wajane kutokana na kuwepo kwa Hati inayoonesha
mmiliki halali wa Ardhi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
ya Rungwe Crispin Meela akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alisema Jumla
ya wananchi 400 wameitikia wito wa kupimiwa ardhi na kukabidhiwa hati miliki
zao hivyo kuwafanya kuishi maisha bora kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi
inavyotaka.
Meela alisema mradi wa upimaji
wa mashamba kwa wakulima hao umefanywa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na
Biashara za Wanyonge Tanzania( Mkurabita)na kwamba jumla ya vijiji saba
vimenufaika ambavyo ni Bujela, Nsongole, Njugilo, Kyambambembe, Nsyasya,
Ntandabala na Bulongwe.
Naye Mratibu wa Mradi wa
Mkutabita Gwabo Mwansasu alisema Mradi huo umeanza kutekelezwa Novemba Mwaka
jana kwa awamu mbili ambapo mchakato wa awamu ya kwanza ulianza kufanyika mwaka
2004/2005 kwa ufadhili wa Abbott Axio ikiwa na lengo la kuwasaidia wajane na
watoto yatima wa kata ya Kinyala
kumiliki ardhi yao.
Aliongeza kuwa awamu ya pili
ilitekelezwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ufadhili wa
European Union Mwaka 2007/2008 kwa vijiji 16, ambapo Vijiji 8 kutoka Rungwe
Mashariki na Vijiji 8 kutoka Rungwe Magharibi.
Mwansasu alisema katika Mradi
wa sasa wa awamu ya tatu umetekelezwa na Mkurabita kwa kushirikiana na Bodi ya
Chai Tanzania pamoja na wakala wa maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chain a lengo
likiwa ni kupima mashamba ya Chai.
Alisema Mradi huu wa uwezeshaji
wakulima wa Chai skimu ya Segera inayojumuisha vijiji 19 vya Masukulu,
Kyambambembe, Segera, Mpombo, Ijigha, Ntandabala, Matwebe, Busisya, Bulongwe,
Mpumbuli, Nsongola, Nsyasya, Bujela, Njugilo, Lufumbi, Kasyeto, Igembe, Kiloba
na Ngaseke.
Mratibu huyo aliongeza kuwa Mradi
huo ulianza Novemba 19, Mwaka 2012 na
kukamilika Juni 15, Mwaka huu ambapo umegharimu Shilingi 64,078,440/= kwa awamu
mbili fedha zilizotolewa na wafadhili.
Alisema Jumla ya mashamba ya
wakulima 1891 yenye ukubwa wa Hekta 485.12 yamepimwa na kutolewa hati miliki za
kimila 400 zenye ukubwa wa Hekta 160.45 kwa vijiji saba.
Na Mbeya yetu.
No comments:
Post a Comment